Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuunga mkono juhudi za Uekumene wa Sala: Pentekoste 2019: Ufalme wako ufike! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuunga mkono juhudi za Uekumene wa Sala: Pentekoste 2019: Ufalme wako ufike!   (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko: Pentekoste: Ufalme wako ufike!

Watu wa Mungu wanaitwa na kuhamasishwa kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Sherehe ya Pentekekoste kwa mwaka 2019, aliomtumia Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury , kama sehemu ya ushiriki wake kwenye Utume wa Sala ya Kiekumene ijulikanayo kama “Ufalme wako ufike”. Uekumene wa sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anafundisha na kusadiki kwamba, Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. “Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana, Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana; aliyenena kwa vinywa vya Manabii.” Sherehe ya Pentekoste ni ukamilifu wa Fumbo la Pasaka ya Kristo na Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofunuliwa katika ukamilifu wake. Pentekoste, inawafanya Wakristo wote kuwa ni sehemu ya watu wa Mungu, taifa lake jipya na teule, yaani Kanisa.

Watu wa Mungu wanaitwa na kuhamasishwa kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani! Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya Sherehe ya Pentekekoste kwa mwaka 2019, aliomtumia Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani , kama sehemu ya ushiriki wake kwenye Utume wa Sala ya Kiekumene ijulikanayo kama “Ufalme wako ufike”. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua, “Uje Roho Mtakatifu” hii ndiyo mbiu ya Wakristo wote wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste.

Roho Mtakatifu ni utimilifu wa ahadi ya Baba na zawadi ya Baba kwa njia ya Mwanae wa pekee Kristo Yesu. Mama Kanisa anakiri na kufundisha kuhusu Nafsi tatu za Fumbo la Utatu Mtakatifu zinazoonesha uwamo mmoja na Baba na Mwana. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya nyoyo zao, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu. Huu ndio Ufalme ambao Wakristo wanaitwa na kutumwa kuutangaza kwa maneno na matendo yao adili.

Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaungana na Askofu mkuu Justin Welby kuwasindikiza katika Sala hii ya “Ufalme wako ufike”. Utume wa Sala ya Kiekumene ulianzishwa kunako mwaka 2016, kwa mwaliko wa Askofu mkuu Justin Welby. Tangu wakati huo, utume huu umekuwa ni mwaliko wa Wakristo Kimataifa wa kushirikiana na kushikamana katika uekumene wa sala. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, baada ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, Mitume walirejea na kwenda Yerusalemu, wakawa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu na ndugu zake! Wakati wote huu, walikaa kusubiri Ujio wa Roho Mtakatifu, Siku ile ya Pentekoste.

Kanisa lina imani na matumaini ya zawadi ya Ujio wa Roho Mtakatifu, ili aweze kukoleza ari na moyo wa kiekumene. Pasipo na nguvu ya Roho Mtakatifu, waamini hawawezi kufanya lolote. Hii ni sala ambayo Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wameisali ili kumwita Roho Mtakatifu na hivyo Ufalme wa Mungu uweze kufika. Katika kipindi cha miaka mitatu, utume huu wa sala umepanuka na kuchukua mwelekeo wa kimataifa. Ni Sala ambayo waamini wanasali kati ya Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni hadi Sherehe ya Pentekeste, Roho Mtakatifu anapowashukia Mitume, tayari kutangaza, kushuhudia na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani unaosimikwa katika msingi ya: haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Papa: Ufalme Wako Ufike
21 May 2019, 09:28