Tafuta

Vatican News
Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, Patriaki Mstaafu wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite, amefariki duniani tarehe 12 mei 2019 akiwa na umri wa miaka 99. Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, Patriaki Mstaafu wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite, amefariki duniani tarehe 12 mei 2019 akiwa na umri wa miaka 99.  (ANSA)

Papa Francisko asikitishwa na kifo cha Patriaki Nasralla Peter Sfeir

Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, Patriaki mstaafu wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite alizaliwa tarehe 15 Mei 1920. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Mei 1950 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Na kunako mwaka 1961 akateuliwa kuwa Askofu na tarehe 26 Novemba 1994, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali. Amefariki dunia 12 Mei 2019 huko Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na taarifa za kifo cha Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, Patriaki mstaafu wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite, kilichotokea, tarehe 12 Mei 2019 huko kwenye Hospitali ya “Hôtel-Dieu de France”, nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 99. Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi alizomtumia Kardinali Béchara Boutros Raï, Patriaki wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite pamoja na familia ya Mungu nchini Lebanon, ana mkumbuka sana Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, aliyeliongoza Kanisa hili kwa muda wa miaka mingi, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu.

Kardinali Nasrallah Peter Sfeir alikuwa ni mtu huru na jasiri aliyetekeleza majukumu yake kwa kujiamini sana, akawa ni mjenzi wa amani na upatanisho wa kitaifa. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa nchi yake na kwa hakika ataendelea kukumbukwa sana katika historia ya Lebanoni. Baba Mtakatifu Francisko anamwombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ili aweze kumpokea katika makao yake ya milele na kumjalia amani pamoja na kumwangazia mwanga wa milele.

Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa familia ya Hayati Kardinali Nasrallah Peter Sfeir pamoja na wale wote walioguswa na msiba huu mzito, wakati wa kushiriki maziko yake. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Nasrallah Peter Sfeir, Patriaki mstaafu wa Kanisa la Antiokia la Wamaronite alizaliwa tarehe 15 Mei 1920. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Mei 1950 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Na kunako mwaka 1961 akateuliwa kuwa Askofu na tarehe 26 Novemba 1994, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali.

Papa: Kifo
14 May 2019, 15:01