Vatican News
Papa Francisko: Mapambano dhidi ya baa la njaa duniani yanaanza kwa utunzaji na matumizi bora ya chakula, kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu! Papa Francisko: Mapambano dhidi ya baa la njaa duniani yanaanza kwa utunzaji na matumizi bora ya chakula, kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Baa la njaa duniani: Utunzaji bora wa chakula

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutokuthamini chakula ni dalili za kutowathamini binadamu. Ni kashfa kubwa kwa watu kushindwa kutambua umuhimu na haki ya chakula kwa binadamu, kiasi kwamba, watu wanathubutu kukimwaga bila ya kuwa na uchungu hata kidogo! Mapambano dhidi ya baa la njaa yaanze na utunzaji pamoja na matumizi bora ya chakula, kwa ajili ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Benki ya Chakula Italia unaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na umekuwa ni msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani, kwa watu kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Mfuko umesaidia kuokoa chakula ambacho kingetupwa kwenye mashimo ya taka kutokana na utamaduni wa watu kutoguswa wala kujali mahangaiko ya jirani zao. Mfuko wa Benki ya Chakula Italia umekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wenye njaa duniani.

Hii ni sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la njaa duniani, kwa kuhifadhi vyema chakula kilichopo, tayari kuwagawia wenye njaa na maskini kama Yesu alivyowaamuru wafuasi wake kufanya baada ya kuwalisha watu elfu tano. Kutokuthamini chakula ni dalili za kutowathamini binadamu. Ni kashfa kubwa kwa watu kushindwa kutambua umuhimu na haki ya chakula kwa binadamu, kiasi kwamba, watu wanathubutu kukimwaga bila ya kuwa na uchungu hata kidogo! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 18 Mei 2019 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na watu wa kujitolewa wa Benki ya Chakula Ulaya, “Food Bank of Europe”, tawi la Italia.

Tabia ya matumizi mabaya ya chakula inaweza kupenya hata katika huduma ya upendo, kutokana na ukiritimba, matumizi makubwa ya fedha na kwamba, ni huduma isiyokuwa na tija inayowafanya watu kuwa ni tegemezi badala ya kuwawezesha kusonga mbele kimaendeleo. Hapa kuna haja anasema Baba Mtakatifu, kutumia akili, kuwa na sera na utekelezaji endelevu wa miradi, kwa kupanga na kutekeleza kwa pamoja. Huduma zote hizi zisukumwe na upendo, mshikamano na umoja, ili kweli ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yaweze kupatikana, kwa ajili ya utu na heshima ya jirani zao. Huu ndio unaopaswa kuwa ni mfumo mpya wa uchumi fungamani.

Ni uchumi unaokita mizizi yake katika mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yao, ili kuhakikisha kwamba, nafasi za kazi na ajira zinapatikana; utu na heshima ya binadamu vinaendelezwa na watu wanakuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni uchumi unaoangalia na kukidhi mahitaji ya familia sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uchumi unaowaweka watu huru badala ya kuwakandamiza kwa kuangalia idadi yao na wala si nyuso, maisha na mahitaji yao. Mfumo wa uchumi wa aina hii, unafumbata utamaduni wa kifo, badala ya kujenga utamaduni unaosimikwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mwelekeo mpya wa uchumi kimataifa ujenge mshikamano, usawa wa kijamii, utu na heshima ya binadamu. Uwe ni chemchemi ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji na matumizi bora ya chakula, iwe ni fursa ya kujenga mshikamano wa udugu kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu anasema, haya ni mawazo yake yanayoonesha wasi wasi na hofu kuu, lakini pia yamefumbata matumaini ya kwamba, Mfuko wa Benki ya Chakula Italia utaendelea kuwashirikisha watu wengi zaidi, hasa vijana wa kizazi kipya, ili kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Papa: Benki ya Chakula
18 May 2019, 15:12