Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi yakuze na kudumisha amani, mshikamano na huduma kwa maskini! Papa Francisko: Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi yakuze na kudumisha amani, mshikamano na huduma kwa maskini!  (ANSA)

Papa Francisko: Majadiliano ya kidini yakuze: amani duniani!

Papa asema, lengo la majadiliano ya kidini liwe ni kutoa huduma ya pamoja kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kupambana na watu wenye misimamo mikali dhidi ya wayahudi; dhuluna na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu uendeleze majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi nchini Italia na Israeli, ili hatimaye, kuvuka mipaka ya nchi hizi mbili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 15 Mei 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya Washauri wa Kimataifa wa Majadiliano ya Kidini kati ya Wakatoliki na Wayahudi, IJCIC, pamoja na wajumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI wanaoshiriki katika mkutano wao wa ishirini na nne kimataifa! Tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua mchakato wa majadiliano ya kidini na katika Tamko lao la “Nostra aetate” yaani “Nyakati Zetu”, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa binadamu!

Baba Mtakatifu anasema, mkutano huu unapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mambo wanayowaunganisha ili kukuza na kudumisha: umoja, mshikamano na ushirikiano wa dhati. Lengo ni kutoa huduma ya pamoja kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na kupambana na watu wenye misimamo mikali dhidi ya Wayahudi; dhuluna na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano huu uendeleze majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi nchini Italia na Israeli, ili hatimaye, kuvuka mipaka ya nchi hizi mbili.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kuendeleza majadiliano ya kidini, ili kuweza kufahamiana vyema zaidi na hivyo kujenga mazingira ya maridhiano pamoja na waamini wa dini hizi mbili kuthaminiana. Wajenge utamaduni wa waamini wa dini hizi mbili kukutana, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini. Maandiko Matakatifu yanasema: “Hila imo moyoni mwa wafikirio uovu, bali wafanyao mashauri, amani, kwao kuna furaha” (Mit 12: 20). Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amesema, mkutano huu uwe ni wa amani kwa ajili ya amani ulimwenguni!

Papa: Wayahudi

 

15 May 2019, 15:33