Papa Francisko awataka walinzi wa Vatican kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka wakati wanapotekeleza dhamana na wajibu wo wa ulinzi na usalama mjini Vatican. Papa Francisko awataka walinzi wa Vatican kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka wakati wanapotekeleza dhamana na wajibu wo wa ulinzi na usalama mjini Vatican. 

Papa akutana na wanajeshi wapya wa "Swiss Guards": Mashuhuda wa imani!

Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wanajeshi hawa wapya kuwaendea watu kwa maneno ya faraja; kukutana nao katika alama ya udugu, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni mashuhuda hai wa Kristo Mfufuka; Alfa na Omega, nyakati zote ni zake! Hii ndiyo njia muafaka ya kuishi kikamilifu wito wao wa Kikristo unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, chemchemi ya imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu bila hata ya kujibakiza. Jumatatu, tarehe 6 Mei 2019 wanajeshi wapya 23 wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss watakula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni siku ambayo wanawakumbuka askari 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Khalifa wa Mtakatifu Petro kunako mwaka 1527. Kiapo cha utii, kitatanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu, itakayoadhimishwa na Kardinali Angelo Comastri, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 4 Mei 2019 amekutana na kuzungumza na wanajeshi hawa wapya, waliokuwa wameandamana na wanafamilia wao kutoka Uswiss. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa ukarimu na sadaka yao kwa ajili ya ulinzi na usalama kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Kanisa. Kila siku, anaonja majitoleo yao, weledi na upendo unaobubujika kutoka katika shughuli zao! Baba Mtakatifu anawapongeza wana familia wa wanajeshi hawa ambao wameridhia uamuzi wao wa kujisadaka kwa ajili ya Vatican na kuendelea kuwasindikiza kwa upendo na sala zao.

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, mwaka huu, wanajeshi hawa wanakula kiapo cha utii wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kushangilia Fumbo la Pasaka, changamoto na mwaliko hata kwa wao kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka, kwa kutangaza furaha ya Pasaka; kwa kueneza utamaduni wa Ufufuko wa wafu dhidi ya utamaduni wa kifo, unao onekana kutaka kuwameza watu wengi. Katika maisha na utume, hata wao wamewahi kukutana na watu ambao “wanaelemewa na makaburi”; watu wasiokuwa na dira wala mwelekeo wa maisha; watu wenye shida na mahangaiko makubwa. Hawa ni wale wanaotarajia kuona mwanga utakaopyaisha maisha na hatimaye, kuzaliwa upya!

Baba Mtakatifu anawasihi wanajeshi hawa wapya kuwaendea watu wote hawa kwa maneno ya faraja; kukutana nao katika alama ya udugu, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni mashuhuda hai wa Kristo Mfufuka; Alfa na Omega, nyakati zote ni zake! Hii ndiyo njia muafaka ya kuishi kikamilifu wito wao wa Kikristo unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, chemchemi ya imani! Wakati wote watakapokuwa hapa Roma, wanahimizwa kushuhudia imani yao kwa furaha, ili mahujaji na wageni wanaotembelea mjini Vatican waweze kuonja na kuguswa na ari pamoja na sadaka ya maisha yao inayofumbatwa na upendo wa Mungu kwa kila binadamu. Huu ndio wito wa kwanza kabisa kwa kila mwamini!

Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi wapya kuwa jasiri, huku wakiendelea kuimarishwa na imani kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Wawe ni mashuhuda na mitume wa upyaisho wa maisha binafsi na yale ya kijumuiya, kama kielelezo cha utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika huduma na maisha ya kijumuiya. Watu wanataka kuona utakatifu wa maisha kutoka kwa wafanyakazi wa Vatican! Kambi ya Jeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na kuelewana.

Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi. Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwadani wa safari ya pamoja. Tabia hii itawawezesha kuishi katika Jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru wanajeshi hawa wapya kwa sadaka na majitoleo yao na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Papa: Swiss Guards

 

05 May 2019, 15:37