Papa Francisko: Jean Vanier, Mwamini mlei aliyejipambanua kwa kutetea: utu, heshima ya maskini na wanyonge ndani ya jamii! Papa Francisko: Jean Vanier, Mwamini mlei aliyejipambanua kwa kutetea: utu, heshima ya maskini na wanyonge ndani ya jamii! 

Papa Francisko: Jean Vanier: Mtetezi wa wanyonge!

Papa anasema: Jean Vanier, mwamini mlei ni kati ya ni watu mashuhuri sana ndani ya Kanisa waliojisadaka kwa ajili ya kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Katika maisha na utume wake, alikazia sana utamaduni wa watu kujenga mahusiano thabiti yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili na Kiutu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 8 Mei 2019 amemkumbuka na kumwombea Hayati Jean Vanier, muasisi wa Jumuiya ya L’Arche, ambayo ilianzishwa takribani miaka 50 iliyopita. Kwa sasa Jumuiya hii ina matawi 130 sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wagonjwa wa afya ya akili. Baba Mtakatifu anasema, Jean Vanier, mwamini mlei ni kati ya ni watu mashuhuri sana ndani ya Kanisa waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Jean Vanier katika maisha na utume wake, alikazia sana utamaduni wa watu kujenga mahusiano thabiti yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili na Kiutu!

Haya ni mahusiano yanayofanywa wakati watu wakiwa mezani, kwa kuangaliana uso kwa uso na wala si mawasiliano yanayowagawa na kuwatenga watu kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Watu wanakuwa mezani, lakini kila mtu akiwa anabofya bofya kwenye simu yake ya kiganjani. Ni mwamini aliyethamini sana siku kuu muhimu kama alama ya kupyaisha tena maisha na hivyo kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Alitilia mkazo umuhimu wa watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kama kielelezo cha utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Ni mwamini mlei, ambaye maisha yake yalirutubishwa kwa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya utajiri na amana ya maisha yake ya kiroho.

Hizi ni tunu msingi zilizomwezesha kuwahudumia wagonjwa wa afya ya akili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza! Ndiyo maana, wagonjwa wa afya ya akili, wamesikitika sana, kuondokewa na Baba, rafiki na mwenza wa safari ya matumaini katika maisha! Jean Vanier ni mwamini mlei, aliyesimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, akawa ni chachu ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, hasa kwa watoto ambao walikuwa wanahukumiwa adhabu ya kifo, hata wakiwa wangali tumboni mwa mama zao! Aliwasaidia sana watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika ataendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Itakumbukwa kwamba, Jean Vanier alizaliwa kunako tarehe 10 Septemba 1928 huko Geneva, Uswiss. Amefariki dunia tarehe 7 Mei 2019, akiwa na umri wa miaka 90. Ni mwamini mlei, aliyetangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, akawa kweli ni mfano wa unabii na imani inayomwilishwa katika matendo. Aliwapenda na kuwathamini wagonjwa wa afya ya akili kama kielelezo makini cha imani na mwanga angavu wa maisha, kwani wao walikuwa kwa hakika ni mashuhuda wa Mungu. Hawa ni watu ambao walikuwa wanawaongoza jirani zao, kumwelekea Mwenyezi Mungu, mpaji wa yote!

Katika maisha yake, alitamani sana kuwaona, waamini na watu wenye mapenzi mema wakijenga na kudumisha Jumuiya ambazo zingekuwa ni kielelezo cha tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu; kwa kujitahidi kuzimwilisha Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Jean Vanier alikuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili kwa wagonjwa wa afya ya akili katika Jumuiya yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kupambana na dhambi pamoja na ubaya wa moyo, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Hii ni changamoto ya kujenga madaraja ya mawasiliano na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wanaopaswa kuthaminiwa na utu pamoja na haki zao msingi kudumishwa!

Jean Vanier
11 May 2019, 14:44