Tafuta

Jean Vanier katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Injili ya uhai, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa watu wote! Jean Vanier katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Injili ya uhai, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa watu wote! 

Papa: Jean Vanier: Alitangaza Injili ya uhai, huruma na upendo!

Jumuiya hizi, ziendelee kuwa ni chemchemi ya maisha mapya; kwa kuonjeshana ile furaha ya Injili, Upendo, Huruma na Msamaha, kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, kila mtu licha ya ulemavu na udhaifu wake wa mwili anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Wote hawa wanaitwa kushiriki katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Marehemu Jean Vanier, muasisi wa Jumuiya ya “L’ Arche” ambayo kwa sasa ina matawi 130 sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wagonjwa wa afya ya akili, amezikwa tarehe 16 Mei 2019 kwenye Jumuiya ndogo ya Trosly-Breuil, nchini Ufaransa. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na viongozi wa kidini na Jumuiya za Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi wakati wa mazishi ya Marehemu Jean Vanier, aliyejitahidi sana katika maisha yake, kuishi akiwa ameungana na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, alijitwalia, udhaifu na mahangaiko ya binadamu. Jean Vanier katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote waliokuwa wanateseka kutokana na udhaifu wa miili yao. Akawatambua watu hawa kuwa ni ndugu zake katika Kristo Yesu; akawathamini na kuwaheshimu, bila ubaguzi wa aina yoyote ile! Aliona ndani mwao, ile sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuilinda na kuitunza Familia la “L’Arche” ili iweze kudumu katika kutekeleza ari na mwamko huo wa Kiinjili kama ulivyobuniwa na Jean Vanier.

Jumuiya hizi, ziendelee kuwa ni chemchemi ya maisha mapya; kwa kuonjeshana ile furaha ya Injili, Upendo, Huruma na Msamaha, kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, kila mtu licha ya ulemavu na udhaifu wake wa mwili anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Wote hawa wanaitwa kushiriki katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, haki na amani! Askofu mkuu Pierre D’Ornellas wa Jimbo kuu la Rnnes, nchini Ufaransa katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa ya Mazishi ya Jean Vanier amesema kwamba, urithi mkubwa ambao amewaachia watu wa Mungu ni tafakari ya Neno la Mungu, inayopaswa kuzamishwa katika maisha ya watu, kwa ajili ya huduma kwa maskini, wagonjwa, wafungwa na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni mwamini aliyependa kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa kidugu. Kwake tofauti za kidini na kiimani, ulikuwa ni utajiri na amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Alitafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu; changamoto inayohitaji toba na wongofu wa ndani ambao ni endelevu! Neno la Mungu lilikuwa ni taa na mwanga katika mapito yake dhidi ya baa la umaskini na udhaifu wa mwili, kiasi cha kuwa ni silaha ya huduma ya upendo, msamaha, imani na matumaini kwa wale waliokata tamaa. Neno la Mungu, likawa wake, chemchemi ya huduma na upya wa upendo unaopata utimilifu wake kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama alama ya kutambua kwamba, kila mtu ni maskini na dhaifu mbele ya Mungu, lakini wenye thamani kubwa machoni pake!

Jean Vanier ni chombo na shuhuda wa umoja na udugu wa kibinadamu, aliyejitahidi kutengeneza mazingira ya amani na utulivu wa ndani kwa maskini na wale wote waliobahatika kutembelea Jumuiya alizozianzisha, kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa upendo. Kwa njia ya maskini hawa, watu waliweza kumwona Mungu kati yao, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa unabii katika ulimwengu mamboleo Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 8 Mei 2019 alimkumbuka na kumwombea Hayati Jean Vanier, muasisi wa Jumuiya ya L’Arche, ambayo ilianzishwa tarehe 5 Agosti 1964. Kwa sasa Jumuiya hii ina matawi 130 sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya huduma ya upendo kwa wagonjwa wa afya ya akili. Baba Mtakatifu anasema, Jean Vanier, mwamini mlei ni kati ya ni watu mashuhuri sana ndani ya Kanisa waliojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jean Vanier katika maisha na utume wake, alikazia sana utamaduni wa watu kujenga mahusiano thabiti yanayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili na Kiutu! Haya ni mahusiano yanayofanywa wakati watu wakiwa mezani, kwa kuangaliana uso kwa uso na wala si mawasiliano yanayowagawa na kuwatenga watu kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia. Watu wanakuwa mezani, lakini kila mtu akiwa anabofya bofya kwenye simu yake ya kiganjani. Ni mwamini aliyethamini sana siku kuu muhimu kama alama ya kupyaisha tena maisha na hivyo kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Alitilia mkazo umuhimu wa watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kama kielelezo cha utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.

Ni mwamini mlei, ambaye maisha yake yalirutubishwa kwa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu sanjari na Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya utajiri na amana ya maisha yake ya kiroho. Hizi ni tunu msingi zilizomwezesha kuwahudumia wagonjwa wa afya ya akili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza! Ndiyo maana, wagonjwa wa afya ya akili, wamesikitika sana, kuondokewa na Baba, rafiki na mwenza wa safari ya matumaini katika maisha! Jean Vanier ni mwamini mlei, aliyesimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, akawa ni chachu ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, hasa kwa watoto ambao walikuwa wanahukumiwa adhabu ya kifo, hata wakiwa wangali tumboni mwa mama zao! Aliwasaidia sana watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika ataendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Itakumbukwa kwamba, Jean Vanier alizaliwa kunako tarehe 10 Septemba 1928 huko Geneva, Uswiss. Amefariki dunia tarehe 7 Mei 2019, akiwa na umri wa miaka 90. Ni mwamini mlei, aliyetangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, akawa kweli ni mfano wa unabii na imani inayomwilishwa katika matendo. Aliwapenda na kuwathamini wagonjwa wa afya ya akili kama kielelezo makini cha imani na mwanga angavu wa maisha, kwani wao walikuwa kwa hakika ni mashuhuda wa Mungu.

Hawa ni watu ambao walikuwa wanawaongoza jirani zao, kumwelekea Mwenyezi Mungu, mpaji wa yote! Katika maisha yake, alitamani sana kuwaona, waamini na watu wenye mapenzi mema wakijenga na kudumisha Jumuiya ambazo zingekuwa ni kielelezo cha tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu; kwa kujitahidi kuzimwilisha Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Jean Vanier alikuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili kwa wagonjwa wa afya ya akili katika Jumuiya yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kupambana na dhambi pamoja na ubaya wa moyo, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Hii ni changamoto ya kujenga madaraja ya mawasiliano na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wanaopaswa kuthaminiwa na utu pamoja na haki zao msingi kudumishwa!

Papa: Jean Vanier
17 May 2019, 15:38