Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, matokeo mapya ya kisayansi, uhandisi na sera ni mada muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu na kwa kazi nzima ya uumbaji! Papa Francisko asema, matokeo mapya ya kisayansi, uhandisi na sera ni mada muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu na kwa kazi nzima ya uumbaji!  (ANSA)

Papa: Changamoto mamboleo zinahitaji mshikamano wa wote!

Matokeo mapya ya kisayansi, uhandisi na sera ni tema hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu na kwa kazi nzima ya uumbaji. Ulimwengu mamboleo umegubikwa na uchu wa kupata faida kubwa, kiasi hata cha kutothamini uhai na familia ya binadamu. Hizi ni dalili za walimwengu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili katika shughuli za kifedha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mawaziri wa fedha kutoka katika nchi mbali mbali duniani, Jumatatu, tarehe 27 Mei 2019 wamekutanika mjini Vatican ili kujadiliana kuhusu mabadiliko ya tabianchi, matokeo mapya ya kisayansi, uhandisi na sera. Mkutano huu umeandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Tema hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu na kwa kazi nzima ya uumbaji. Ulimwengu mamboleo umegubikwa na uchu wa kupata faida kubwa, kiasi hata cha kutothamini uhai na familia ya binadamu. Hizi ni dalili za walimwengu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili katika shughuli za kifedha, hali inayotishia kusababisha maafa makubwa kwa siku za usoni!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 27 Mei 2019 alipokutana na kuzungumza na mawaziri wa fedha wanaojadili kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, matokeo mapya ya kisayansi, uhandisi na sera. Kutokana na mwingiliano na mafungamano ya kijamii, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwa na mpango mkakati wa pamoja kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo. Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21, Vatican inapenda kukazia zaidi kuhusu: Kanuni maadili, utu wa mwanadamu, mapambano dhidi ya umaskini; sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu na: pamoja na kuweka mipango thabiti itakayokidhi mahitaji msingi ya binadamu.

Mwaka 2015, Jumuiya ya Kimataifa ilifikia makubaliano makuu mawili yaani: Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu pamoja na Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kuhakikisha kwamba, Malengo haya yanafikiwa, kwa ajili ya binadamu, ustawi na maendeleo kwa siku za usoni. Huu ni wajibu wa kimaadili uliofikiwa na unapaswa kutekelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini, hali bado ni tete kwani kuna nchi ambazo zinaendelea kuwekeza zaidi katika nishati ya makaa ya mawe na teknolojia rafiki kwa mazingira bado inaendelea kuwa ni kitendawili.

Wanasayansi wanasema, nishati ya upepo, jua na maji ni rafiki sana katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira; lakini kutokana na rushwa, ubadhilifu na mafao binafsi, watu wanaendelea kuchuma faida huko licha ya kutishia kusababisha maafa makubwa ya binadamu. Wanasayansi wanasema, kiasi kikubwa cha hewa ya ukaa angani ni kati ya vyanzo vinavyochangia ongezeko la joto duniani. Hizi ni shughuli zinazofanywa na binadamu na kwamba, kiwango chake kwa sasa ni zaidi ya asilimia 415 kwa milioni, kiwango cha hali ya juu kabisa, kuwahi kufikiwa. Matokeo yake ni ongezeko kubwa la joto duniani, ukame wa kutisha, majanga ya moto, mafuriko, kuongezeka kwa kiwango cha maji baharini, magonjwa ya milipuko na kwamba, hizi ni dalili tu, lakini makubwa yanaweza kujitokeza, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitaweza kuchukua hatua madhubuti.

Ushauri wa wataalamu wa hali ya hewa ni wazi kwamba kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa, ili kulinda na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kwa kutumia gharama kidogo. Jambo hili linawezekana kwa kuwekeza katika teknolojia rafiki pamoja na maboresho ya nishati. Baba Mtakatifu Francisko anasema, jambo hili linawezekana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo msingi; kwa kuondokana na shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kukomesha kabisa matumizi ya nishati ya mkaa na kuanza kufungua ukurasa mpya wa matumizi ya nishati safi na salama kama vile nishati ya upepo, nguvu za jua na maji.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera na mikakati ya kiuchumi kuhakikisha kwamba, inakidhi mahitaji msingi ya binadamu; inalinda na kuheshimu utu wa binadamu; kwa kuonesha mshikamano na maskini pamoja na watu kuondokana na tabia ya kuabudu sana fedha, hali inayosababisha mateso na mahangaiko makubwa ya watu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kama viongozi wa masuala ya fedha na uchumi wanapaswa kuzingatia utu, heshima na uhai wa binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mawaziri wa fedha wataweza kuridhia utekelezaji wa ushauri wa wanasayansi kuhusu utunzaji bora wa mazingira, kwa kuwa na uhandisi unaozalisha nishati salama pamoja na kuzingatia utu na heshima ya binadamu.

Ushirikiano kati ya watunga sera na mikakati pamoja na wanasayansi duniani, usaidie kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu pamoja na Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume, akitumaini kukutana nao tena ili kumshukuru Mungu kwa kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kurekebisha kasoro kabla mambo hayajaharibika sana.

Papa: Mawaziri
28 May 2019, 15:24