Tafuta

Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima. Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima. 

Papa Francisko: Kimbilieni tunza ya Bikira Maria wa Fatima!

Bikira Maria wa Fatima anawapenda sana watoto wake na kwamba, kila mmoja wao anayo thamani kubwa machoni pake na kwamba, anatambua fika yale yaliyofichika katika sakafu ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria wa Fatima, kulinda maisha ya watoto wake wote na kuwaongoza kuelekea kwenye hija ya utakatifu wa maisha kwa njia ya toba na wongofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima ambaye ameacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, anatambua kwamba, Bikira Maria wa Fatima anawapenda sana watoto wake na kwamba, kila mmoja wao anayo thamani kubwa machoni pake na kwamba, anatambua fika yale yaliyofichika katika sakafu ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria wa Fatima, kulinda maisha ya watoto wake wote na kuwaongoza kuelekea kwenye hija ya utakatifu wa maisha!

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, alikuwa na uhusiano wa pekee na Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima si tu kwa sababu ya maombezi ya Bikira Maria wakati wa jaribio la kutaka kumwondolea uhai kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican, kunako tarehe 13 Mei,1981, bali kwake, Bikira Maria, alikuwa kwa hakika ni mama mlinzi na mwongozi wa maisha. Ni kwa maombezi yake tu, aliweza kusalimika na majaribu mbali mbali katika maisha yake. Ile risasi, leo hii inahifadhiwa kwenye Kikanisa cha Bikira Maria wa Fatima. Kuna baadhi ya watu bado wanadhani kwamba, kuna sehemu ya nne ya Siri ya Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, lakini si kweli na hakuna sababu zozote za kimsingi. Kuna baadhi ya watu wanafanya hivi kwa mafao yao binafsi.

Bikira Maria aliwatokea Watoto wa Fatima kunako mwaka 1917, wakati walimwengu walipokuwa wanateseka kutokana na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na kuwapatia ujumbe wa matumaini uliokuwa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani; sala na kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea katika historia ya maisha ya watu wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kumtumainia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwani yeye ameushinda ulimwengu.

Kumbe, ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumalia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea: haki, amani na maridhiano duniani! Hii ni changamoto endelevu hata kwa walimwengu wa nyakati hizi!

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita, kinzani na majanga katika maisha; tawala za kifashisti na kikomunisti; tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea!

Waamini wanaalikwa kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili; ili kujiachilia wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, tayari kujazwa na upendo wake usiokuwa na kifani, upendo unaowaambata wote pasi na ubaguzi. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, imani inapaswa kukua na kukomaa na matunda yake ni toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!

Kimsingi, ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto wa Fatima unafumbatwa katika matumaini, toba na wongofu wa ndani; mambo msingi yanayowawezesha waamini kutambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Familia na Parokia ni mahali ambapo waamini wanaweza kurithishana ujumbe wa Bikira Maria, ili Moyo Safi wa Bikira Maria uweze kuheshimiwa na kuthaminiwa! Watoto wa Fatima yaani yaani: Mtakatifu Francis na MtakatifuYacinta Marto pamoja na Sr. Lucia dos Santos wamesaidia kwa kiasi kikubwa kueneza Ibada ya Bikira Maria wa Fatima hasa kwa mwezi Mei.

Leo hii kuna majanga makubwa yanayoendelea kumwandama mwanadamu lakini upendo wa Mungu ni mkubwa sana kwa waja wake, changamoto kwa waamini ni kujiaminisha kwa Yesu ili aweze kuwapatia ulinzi na tunza yake kwa maombezi ya Bikira Maria, kwani daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Ujumbe huu uwe ni changamoto na mwaliko wa kuzama zaidi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Lugha aliyotumia Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ilikuwa ni lugha ya upendo inayoeleweka na kufahamika na wengi, changamoto na mwaliko kwa waamini ni kuwa kweli vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Toba na wongofu wa ndani pamoja na maisha ya sala ni mambo msingi ambayo yalikaziwa sana na Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima!

Fatima: Ureno
13 May 2019, 14:32