Vatican News
Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kikatili yaliyofanyika nchini Burkina Faso, tarehe 28 Aprili 2019. Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kikatili yaliyofanyika nchini Burkina Faso, tarehe 28 Aprili 2019.  (ANSA)

Papa Francisko asikitishwa na mauaji huko Burkina Faso

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano na kamwe tofauti zao msingi zisiwe ni sababu ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii isiyokuwa na mvuto wala mashiko! Huu ni wakati wa kujenga udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama watoto wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa kuhusu shambulizi la kigaidi lililofanyika huko mjini Silgadji, karibu na Jimbo la Soum nchini Burkina Faso na kusababisha waamini sita waliokuwa wakisali Kanisani hapo kupoteza maisha.  Majambazi hao walikuwa wamepanda piki piki na walipofika Kanisa hapo, Jumapili, tarehe 28 Mei 2019 wakawafyatulia risasi waamini waliokuwemo Kanisa hapo kwa sala na ibada. Dr. Alessandro Gisoti, Msemaji mkuu wa muda wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa sala waamini waliofariki dunia, ndugu zao pamoja na Jumuiya ya Kikristo nchini Burkina Faso.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano na kamwe tofauti zao msingi zisiwe ni sababu ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii isiyokuwa na mvuto wala mashiko! Huu ni wakati wa kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama watoto wa Mungu! Kwa upande wake, Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, amelaani shambulizi la kigaidi lililofanywa huko Burkina Faso.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wasiokuwa na hatia, wakiwa katika sala, wanashambuliwa kutokana na chuki za kidini! Mashambulizi katika nyumba za Ibada kwa miaka ya hivi karibuni yameongezeka maradufu sehemu mbali mbali za dunia. Dr. Olav Fykse Tveit, anasema, Kanisa litaendelea kukuza na kudumisha Injili ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa mambo msingi yanayoweza kuleta mageuzi makubwa katika akili na nyoyo za watu! Misimamo mikali ya kidini na kiimani ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii!

Papa: Burkina Faso
02 May 2019, 14:53