Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Wosia wa Kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana na Sinodi za familia! Baba Mtakatifu Francisko: Wosia wa Kitume "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi" ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana na Sinodi za familia! 

Papa Francisko: Wosia wa Kitume: Christus vivit: Kristo anaishi!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Sinodi ya vijana na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka sahihi kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Wosia huu umezinduliwa rasmi, tarehe 2 Aprili 2019. Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana!

Wosia huu wa kitume umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018.

Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anakita tafakari yake kwenye Neno la Mungu kuhusu vijana tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya. Sura ya Pili inamwonesha Kristo Yesu ambaye daima ni kijana na chemchemi ya ujana wa Kanisa kama ilivyo hata kwa Bikira Maria, msichana wa Nazareti. Sura ya tatu, Vijana wanaambiwa kwamba, wao ni leo ya Mungu inayofumbatwa katika matamanio halali ya vijana, madonda wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao pamoja tafiti endelevu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya ujana. Baba Mtakatifu anagusia changamoto za ujana zinazoibuliwa katika ulimwengu wa kidigitali, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na kuonesha mwanga unaoweza kuwaokoa vijana kutoka katika giza hili la maisha.

Sura ya nne ni mbiu kwa vijana wote kwamba, “Mungu ni upendo”, Kristo Yesu anaokoa na kwamba, yu hai kabisa na kwa njia ya Roho Mtakatifu, vijana wanaweza kuboresha maisha yao. Sura ya tano inaonesha mapito ya ujana katika makuzi na ukomavu; vijana wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Vijana wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kama wamisionari jasiri, ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao katika ukweli, hii ni changamoto kwa vijana wote! Sura ya sita, inawaonesha vijana waliokita mizizi yao katika mambo msingi ya maisha. Hawa ni wale vijana wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na wazee; ili kumwilisha ndoto na maono, ili kwa pamoja, wazee na vijana waweze kuthubutu!

Sura ya saba ni kuhusu utume wa Kanisa kwa vijana, kwa kuwasindikiza na kuwaongoza, wao wenyewe wakionesha kipaji cha ubunifu. Mkazo katika utume kwa vijana: tafiti na ukuaji! Kanisa linapaswa kujenga mazingira yatakayosaidia kumwilisha vipaumbele hivi. Kanisa pia linapaswa kuwekeza zaidi katika utume wa vijana kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu; kwa kuendesha pia utume wa vijana katika “vijiwe vya vijana” ili kuwatafuta na kuwaendea huko huko waliko, daima kwa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu. Daima vijana wakumbuke kwamba, wao ni wamisionari, kumbe, utume kwa vijana unapaswa kujikita katika umisionari, huku vijana hawa wakiwa wanasindikizwa na watu wazima na wakomavu, ili kujitambua na kwamba, wanapaswa kutembea bega kwa bega, huku wakiheshimu na kuthamini uhuru wao!

Sura ya nane, Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu miito, kwa kukazia upendo na familia, ili kujisadaka bila ya kujibakiza katika kazi na hatimaye, ujenzi wa familia bora! Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, lakini wawe wepesi kusoma alama za nyakati kwa kuondokana na kishawishi cha kutaka kuchagua kazi, jambo la msingi kwanza ni huduma! Baba Mtakatifu anahitimisha sura ya nane kwa kuangalia wito maalum unaowasukuma vijana kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kipadre na kitawa, kama utimilifu wa maisha yao! Sura ya tisa ni kuhusu: Mang’amuzi ambao ni mchakato unaomwezesha kijana kutambua wito wake katika maisha! Hii ni dhamana inayohitaji ukimya na tafakari ya hali ya juu, ili kuweza kutoa maamuzi mazito katika maisha.

Mang’amuzi ya miito yanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu: kusikiliza kwa makini; kufanya maamuzi ya busara na hatimaye, kusikiliza kutoka katika undani wa maisha, ili kutambua ni mahali gani ambako Mwenyezi Mungu anamtaka kijana huyu kwenda. Baba Mtakatifu anahitimisha Wosia huu wa kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” kwa kuonesha hamu ya furaha ya moyo wake kwani anataka kuwaona vijana ambao wanaonekana kwenda taratibu na waoga katika maisha, kuanza kutimua mbio na kumwendea Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linahitaji ari na mwamko wa vijana wa kizazi kipya; maoni yao, lakini zaidi imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa matendo! Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu anawakumbusha vijana kwamba, wakifanikiwa kwenda mbio na kufika mwishoni mwa safari, wawe na uvumilivu ili kuwasubiria wazee wanaojikongoja!

Christus vivit: utangulizi
02 April 2019, 16:06