Tafuta

Papa Francisko: Wenyeheri wapya kutoka Argentina ni mashuhuda wa imani, haki na upendo wa Kiinjili! Papa Francisko: Wenyeheri wapya kutoka Argentina ni mashuhuda wa imani, haki na upendo wa Kiinjili! 

Papa: Wenyeheri wapya Argentina: Mashuhuda: Imani, Haki & Upendo

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, kwa niaba ya Papa Francisko, amewatangaza: Askofu Enrique Angel Angelelli, Mtawa Carlos de Dios Murias, Padre Gabriel Longueville pamoja na Wenceslao Pedernera, Katekista na Baba wa familia, kuwa Wenyeheri. Ibada ya kuwatangaza wenyeheri hawa kutoka Argentina waliouwawa kikatili kunako tarehe 27 Aprili, 1976 imeadhimishwa Jimboni Rioja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi, tarehe 27 Aprili 2019, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amewatangaza Watumishi wa Mungu: Askofu Enrique Angel Angelelli, Mtawa Carlos de Dios Murias, Padre Gabriel Longueville pamoja na Wenceslao Pedernera, Katekista na Baba wa familia, kuwa Wenyeheri. Ibada ya kuwatangaza wenyeheri hawa kutoka Argentina waliouwawa kikatili kunako tarehe 27 Aprili, 1976 imeadhimishwa Jimboni Rioja, nchini Argentina.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu ambamo amebainisha zawadi kuu tatu kutoka kwa Kristo Mfufuka yaani: amani, furaha na utume, aliyaelekeza mawazo yake nchini Argentina. Baba Mtakatifu anasema, hawa ni mashuhuda wa imani, walioteseka kwa sababu ya haki na upendo wa Kiinjili. Mfano na sala zao, ziwatie shime wale wote wanaoendelea kujisadaka, ili kweli dunia iweze kusimikwa katika misingi ya haki na mshikamano. Hawa ni waamini waliouwawa kutokana na chuki za imani na kwamba, Mahakama kuu nchini Argentina kunako mwaka 2014 ilijiridhisha kuwa, vifo vya mashuhuda hawa wa imani vilisababishwa na Bwana Benjamin Menèndez na Luis Fernando Estrella, waliopatikana na hatia na hatimaye, kuhukumiwa kifungo cha maisha!

Askofu Enrique Angeli Angelelli alizaliwa kunako mwaka 1923, akapewa Daraja ya Upadre mwaka 1949, mwaka 1960 akateuliwa kuwa Askofu na hatimaye, akabahatika kushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ukawa ni chemchemi ya ari na mwamko wake wa shughuli za kitume nchini Argentina. Akiwa Jimboni Rioja, Askofu Enrique Angeli Angelelli, akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa miongoni mwa wananchi mahalia. Akatoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa waamini walei, aliowachangamsha kuhakikisha kwamba, wanayatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko; akasimamia haki, amani, ustawi na maendeleo ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Msimamo huu wa kichungaji ulisababisha mpasuko mkubwa hata miongoni mwa viongozi wa Kanisa. Lakini, watu wengi wanamkumbuka kama shuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, msamaha na upendo kwa maskini! Katika maisha na utume wake, watu wengi wakabahatika kukutana na Kristo Mfufuka! Kama inavyoeleweka kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki kwamba, mwamini anaweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa njia ya kifo dini, kielelezo cha pekee katika kumfuasa Kristo, lakini, ikumbukwe kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake ni upendo kwa Mungu na jirani.

Kifodini kadiri ya ufahamu wa Kanisa ni kupokea kwa hiyari kifo kama kielelezo cha upendo kwa Kristo! Ni kupokea kifo kutokana na chuki za kiimani, au fadhila nyinginezo za Kikristo. Kifodini ni kielelezo cha unyenyekevu kwa mwamini anayesamehe kama njia ya kumuiga Kristo Yesu, ambaye alipokuwa pale juu Msalabani aliwaombea watesi wake msamaha kutoka kwa Baba yake wa mbinguni!

Papa: Mashuhuda wa imani

 

29 April 2019, 16:00