Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka ya Sherehe ya Pasaka, Wakristo wote wa Makanisa ya Kiorthodox. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka ya Sherehe ya Pasaka, Wakristo wote wa Makanisa ya Kiorthodox. 

PASAKA YA BWANA 2019: Makanisa ya Kiorthodox: Imani & Matumaini!

Kanisa linatangaza furaha kuu, kwani Kristo Mfufuka amewashinda adui wakuu wa mwanadamu ambao ni: dhambi na mauti, huzuni, shida na mahangaiko. Lakini, bado kuna: vita, majanga, misimamo mikali ya kidini na kiimani, vitendo vya kigaidi; magonjwa, njaa na umaskini wa hali na kipato. Haya ni mambo yanayomnyima mwanadamu furaha ya kweli kutoka kwa Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 28 Aprili 2019 ameungana na Wakristo wa Kanisa la Kiorthodox, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2019 kadiri ya Kalenda ya Julian. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, waliomtumia salam na matashi mema katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia!

Kwa upande wake, Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima, anawaalika Wakristo kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kweli kweli! Huu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kristo Yesu kabla ya mateso yake, alikwisha waambia Mitume wake kwamba, wakati wa mateso yake, watalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; watahuzunishwa, lakini huzuni yao, itageuka kuwa furaha inayodumu milele yote! Wanawake walikuwa ni watu wa kwanza kabisa kushuhudia na kutangaza furaha ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Leo, Kanisa linatangaza furaha kuu, kwani Kristo Mfufuka amewashinda adui wakuu wa mwanadamu ambao ni: dhambi na mauti, huzuni, shida na mahangaiko. Hata katika ulimwengu mamboleo bado watu wanashuhudia mashambulizi ya kigaidi, vita, majanga, misimamo mikali ya kidini na kiimani; magonjwa, njaa na umaskini wa hali na kipato. Haya ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kumnyima mwanadamu furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Kumbe, ni wajibu wa kila mwamini kubeba vyema Msalaba wa maisha yake, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu Mfufuka mbaye ni: Njia, Ukweli na Uzima; Furaha na Amani ya watu wake, anaendelea kuambatana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Kristo alikwisha kuwaambia wafuasi wake kwamba, hatawaacha yatima, bali ataendelea kuwa pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Wafuasi wake, wataendelea kumtambua kwa kuumega Mkate! Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima, anawaalika Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo, pamoja na kuendelea kujiaminisha kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwenye ujumbe wake, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka na kwamba, viumbe vyote vinapaswa kushangilia mwanzo mpya wa kazi ya uumbaji! Wanawake wakamwona na kumwamini, Tomaso alitwaye Pacha, akasita kuamini, hadi alipokutana na Kristo Mfufuka na hatimaye, kuungama imani yake kwa Kristo kama Bwana na Mungu wake! Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni msingi wa imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa walimwengu wote.

Kwa njia hii, mwanadamu amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni Mwana kondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa, changamoto na mwaliko kwa waamini kuenenda katika nuru ya Kristo mfufuka, kwa kutenda wema, kwa kusimamia haki na kweli! Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox anawasihi waamini waendelee kujenga na kuimarisha: Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume, ili Mwenyezi Mungu aweze kupewa kipambele cha kwanza katika maisha ya walimwengu. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Mfufuka sehemu mbali mbali za dunia, kwa njia ya Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi!

Papa: Ujumbe wa Pasaka
30 April 2019, 10:21