Vatican News
Papa Francisko kutembelea Parokia ya Mt. Giulio ili kutabaruku Altare na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa! Papa Francisko kutembelea Parokia ya Mt. Giulio ili kutabaruku Altare na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa!  (ANSA)

Papa Francisko: Parokia ya Mt. Giulio: Kutabaruku Altare!

Liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho ya kweli ya Kikristo. Jumapili, tarehe 7 Aprili 2019, Baba Mtakatifu atatembelea Parokia ya Mtakatifu Giulio iliyoko Jimbo kuu la Roma, ili kutabaruku Altare ya Kanisa hili pamoja na kuadhimisha mafumbo ya Kanisa. Masalia ya watakatifu kadhaa yatawekwaAltareni hapo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja wa Taifa la Mungu ambalo hulifanya Kanisa liwepo. Ekaristi Takatifu ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la waamini kuliabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa ni mahali patakatifu panapowawezesha waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu, Kusali na Kutafakari Matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, liturujia ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho ya kweli ya Kikristo.

Jumapili, tarehe 7 Aprili 2019, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea Parokia ya Mtakatifu Giulio iliyoko Jimbo kuu la Roma, ili kutabaruku Altare ya Kanisa hili pamoja na kuadhimisha mafumbo ya Kanisa. Masalia ya watakatifu yatakayowekwa Altareni hapo ni ya Mtakatifu Yohane Bosco, Margherita Maria Alacoque pamoja na Mtakatifu Maria Goretti. Waamini wa Parokia hii, katika kipindi cha miaka mitatu, wamejifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanachangia na hatimaye, kukamilisha ukarabati mkubwa uliofanywa kwenye Kanisa hili baada ya paa kuporomoka na kuharibu Altare iliyokuwepo hapo awali! Hii ni Parokia ambayo inahudumiwa na Mapadre wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kujionea mwenyewe hali halisi Parokiani hapo, kwa kukutana na kuzungumza na watoto na vijana; kuwatembelea na kuzungumza na wagonjwa pamoja na wazee!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” anawaalika waamini kuendelea kushuhudia na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa, hasa Liturujia na Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu, Matendo ya huruma kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa ni Sakramenti za huruma ya Mungu. Ni mahali pa kuonja upendo, toba, wongofu wa ndani na msamaha kwani huruma yake ni kuu na huvuka kila vikwazo na vizingiti katika maisha ya mwanadamu! Kwa njia ya huruma, waamini wataweza kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha yao! Parokiani hapo, Baba Mtakatifu atapata pia nafasi ya kuwaungamisha waamini waliojiandaa ili kuadhimisha vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu!

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Giulio wanataka kujimega na kujitoa kuwa Ekaristi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Katika kipindi chote cha Kwaresima, wamefunga, wakasali na kujinyima. Majitoleo na sadaka yote hii, wanataka kumkabidhi Baba Mtakatifu Francisko ili uwe ni mchango wao kama ushuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini. Hii ni kati ya Parokia 19 za Jimbo kuu la Roma zinazotoa hifadhi kwa watu wasiokuwa na makazi Jijini Roma. Waamini hawa pia wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wazee na wagonjwa, si bure kuona kwamba, ushuhuda huu wa imani katika matendo umeleta mvuto hata Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwenda kuwatembelea na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja nao! Hadi rahaa!

Papa: Parokiani
05 April 2019, 16:11