Alhamisi Kuu: Baba Mtakatifu Francisko amebariki Mafuta Matakatifu yatakayotumika kwa ajili ya Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa Mwaka 2019-2020 Alhamisi Kuu: Baba Mtakatifu Francisko amebariki Mafuta Matakatifu yatakayotumika kwa ajili ya Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa Mwaka 2019-2020 

Juma kuu 2019: Papa: Ibada ya Kubariki Mafuta Matakatifu: Neema!

Hii ni neema ya kumfuasa Kristo, kushangaa na kujazwa furaha; ili kuweza kufanya mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Maskini na wale wote walioelemewa na mifumo ya umaskini, walitangaziwa Habari Njema ya Wokovu; mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni Wasamaria wema, ili kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Alhamisi Kuu, Mama Kanisa anakumbuka Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Sakramenti ya Sadaka: Shukrani, sifa na utukufu kwa Baba wa milele; Ni Kumbukumbu ya mateso yaletayo wokovu na kwamba, hii ni sadaka ya uwepo wa Kristo kwa Neno na Roho wake Mtakatifu. Mama Kanisa anakumbuka pia Siku Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa kuwateuwa baadhi ya waamini na kuwaweka wakfu kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Hawa ni Makuhani waoliopewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, katika Nafsi ya Kristo ambaye ni kichwa cha Kanisa lake! Hii ni Siku ambayo Kristo alikazia huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu, kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, tarehe 18 Aprili 2019, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kubariki Mafuta Matakatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amebariki Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na pamoja na Krisma ya Wokovu; Mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kama mapadre na maaskofu. Hii ni siku ambamo wakleri wamerudia tena ahadi za utii kwa Baba Mtakatifu Francisko kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake, amekazia neema ambazo waamini wanapata kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu katika maisha yao.  Hii ni neema ya kumfuasa Kristo, kushangaa na kujazwa furaha kwa kukutana naye katika maisha, ili kuweza kufanya mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Maskini na wale wote walioelemewa na mifumo ya umaskini, walitangaziwa Habari Njema ya Wokovu; mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni Wasamaria wema, ili kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Kristo Yesu alipakwa mafuta na kutumwa na Baba yake wa mbinguni kwenda kuwapaka mafuta watu wa Mungu na kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akawaondolea dhambi, akawaganga na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao; akawafundisha na kuwarejeshea tena matumaini wale wote waliokata tamaa na kusukumizwa pembezoni mwa maisha. Kristo Yesu alidumisha ile neema ya kuwa karibu sana na watu, tangu siku ile alipozaliwa, alipotolewa Hekaluni na hatimaye, alipoinuliwa juu Msalabani.

Kristo Yesu alikuwa ni kiongozi mwenye mvuto kwa watu na wale wote waliobahatika kukutana naye mubashara, walipata neema na utulivu wa ndani. Hawa ni akina Veronika, Simoni Mkirene, wale wevi waliokuwa wametundikwa msalabani pamoja na Yesu bila kumsahau yule Akida aliyekiri ukuu na utukufu wa Yesu kama Mwana wa Mungu. Kwa watu wote hawa, Kristo Yesu alikuwa ni mchungaji mwema, kiasi hata aliweza kuamsha ndani mwao ile kiu ya kutaka kumfuasa katika maisha yao, wakashangazwa na hatimaye baada ya kusikiliza mafundisho yake, wakafanya mang’amuzi ya maisha!  Maandiko Matakatifu yanaonesha kwamba, neema ya kwanza ambayo Kristo amewajalia wale wote waliobahatika kukutana naye katika safari ya maisha yao ni neema ya ufuasi, pasi na masharti, ingawaje, Mitume wake, wangelipenda kuona Yesu, akiwaaga na kuwaacha watokomee mbali na uwepo wao.

Mitume walitaka kujihakikishia usalama wa chakula na nafasi zao, bila kuwajali watu waliokuwa wanawazunguka. Huu ni mwelekeo potofu wa Ukasisi, “Clericalism”. Lakini, Yesu anawataka Mitume wake kujibidisha na kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula na ndivyo ilivyokuwa! Watu waliokuwa wanamfuasa Kristo Yesu walikirimiwa neema ya mshangao na kujazwa furaha, kwa kuona miujiza aliyotenda, lakini zaidi, kwa uwepo wake mwanana. Watu walitamani kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao, ili waweze kumsalimia na kupata baraka kutoka kwake! Yesu naye kwa upande mwingine, alishangazwa sana na imani iliyoshuhudiwa na wale aliokutana nao, kiasi cha kuwapongeza na kuwashukuru, kama ilivyotokea kwa yule Mwanamke aliyempongeza Bikira Maria aliyemzaa na kumnyonyesha Yesu!

Wale waliomfuasa Kristo Yesu, walishangazwa na kuguswa sana na mafundisho yake, kwani alifundisha kwa mamlaka. Kristo Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anayeamsha ndani ya watu mang’amuzi ya kufanya maamuzi mazito katika maisha. Aliweza kuzungumza, kujadiliana na kulumbana na makundi mbali mnbali ya watu, jambo la kushangaza ni kuona kwamba, makundi yote yalitambua umuhimu, ukuu na nguvu iliyokuwa inabubujika kutokana na mafundisho yake. Kwa njia hii, Neno la Mungu likaweza kupenya katika sakafu ya nyoyo za watu; pepo wachafu wakapigwa kikumbo na “kupotelea kule kusikojulikana”. Wale walioanzisha mijadala ya kejeri na dharau, walinyamazishwa kama risasi majini na watu wakayaona yote haya kwa mshangao mkubwa!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwinjili Luka anakazia makundi makuu manne katika Injili yake, kuwa ndio walengwa wakuu: Maskini, wafungwa, vipofu pamoja na wajane. Hawa walikuwa na upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Maskini walielemewa sana na umaskini pamoja na mifumo yote iliyozalisha umaskini; wajane ni watu waliokuwa wanateseka na kunyanyasika kutokana na mfumo dume na kwamba, katika mazingira yao, walikuwa si “mali kitu”. Yesu alitumwa kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, hata wajane katika ujane wao, waliweza kuonekana mbele ya macho ya Kristo Yesu na kupongezwa kwa mchango na ushuhuda wao. Hawa ni mifano bora ya kuigwa ya watakatifu wanaowazunguka kama majirani wema. Watu wanaoteseka walikuwa na nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kiasi hata cha kujifananisha na Msamaria mwema aliyejitaabisha kuwahudumia watu kwa mafuta ya faraja na kuwaganga kwa divai ya matumaini. Kwa hakika Kristo Yesu ni mganga wa kweli: kiroho na kimwili.

Yesu alitumwa kuwatangazia wafungwa wa vita kufunguliwa kwao! Hawa ni wafungwa waliokuwa magerezani huko Yerusalemu baada ya vita! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, leo hii, Yesusalemu imefungwa kwenye ukoloni wa kiitikadi na kwamba,  wanaweza kukombolewa tu, kwa kuzingatia utamaduni wao asilia unaosimikwa katika kazi na sanaa! Mambo haya msingi yanaweza kuikomboa miji ambayo kwa sasa imetopea katika utumwa mamboleo! Baba Mtakatifu anawakumbusha wakleri kwamba, waamini walei ni mifano bora ya kuigwa; watu ambao wanapaswa kupakwa mafuta, ili waweze kusimama tena kuimarishwa kwa uwepo endelevu wa Roho Mtakatifu aliyewapaka mafuta, ili nao wakawapake watu wanaowahudumia. Mapadre ni watu waliotwaliwa kutoka kati ya watu na kuwekwa wakfu kwa ajili ya mambo matakatifu. Waamini walei ni sura, mfano, kiini cha maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anawataka wakleri kusimika maisha yao katika ufukara, ili kuonja mateso na mahangaiko ya maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Mapadre wawe na upofu kama ule wa Bartimayo mwana wa Timayo kipofu, ili kila mwanapoamka wamwombe Mwenyezi Mungu neema ya kuweza kuona tena. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapotoa Daraja Takatifu ya Upadre anapenda kuwapaka vyema Mafuta ya Krisma ya Wokovu, ili nao waweze kuwapaka mafuta ya imani wale watakaowahudumia; ili waguse: dhambi, mahangaiko na madonda ya waamini wao.

Mafuta Matakatifu yawawezeshe Mapadre kugusa imani, matumaini, mapendo, uaminifu, sadaka na majitoleo yao bila ya kujibakiza hata kidogo. Mapadre wajifunze kupaka mafuta na kubariki, ili kuganga na kuponya mfumo dume, nyanyaso, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na ukatili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka Mapadre wawe ni vyombo vya kupyaisha utakatifu wa watu wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mapadre wawe ni chemchemi ya sala na msamaha kwa waamini wao na ulimwengu katika ujumla wake, ili makundi mbali mbali yanayomfuasa Kristo yaweze kuunganika na kuwa ni watu waaminifu na wateule wa Mungu na kwamba utimilifu wao ni katika Ufalme wa Mungu!

Mwishoni wa Ibada ya Kubariki Mafuta Matakatifu, Baba Mtakatifu amewapatia Mapadre wote waliokuwepo Kanisa hapo Kitabu kijulikanacho kwa lugha ya Kiitalia ‘La nostra fatica è preziosa per Gesù. Omelie nelle Messe crismali". Huu ni mkusanyo wa mahubiri yote yaliyokwisha kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi kuu wakati wa kubariki Mafuta Matakatifu kuanzia mwaka 2013.

Papa: Krisma ya Wokovu
18 April 2019, 15:20