Alhamisi Kuu: Karamu ya Mwisho: Papa Francisko amekazia Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma makini ili kujenga umoja, urafiki na udugu! Alhamisi Kuu: Karamu ya Mwisho: Papa Francisko amekazia Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma makini ili kujenga umoja, urafiki na udugu! 

Alhamisi Kuu: Karamu ya Mwisho: Injili ya upendo na huduma!

Baba Mtakatifu amekazia: Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma, kama alivyofanya Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha Mitume wake miguu! Katika historia, hili ni tendo ambalo lililofanywa na watumwa! Lakini, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu alijinyenyekesha ili kuonesha mfano na kuwataka wafuasi wake wawe ni mashuhuda na vyombo vya huduma makini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni, tarehe 18 Aprili 2019 ameadhimisha Ibada ya Karamu ya Mwisho, “Coena Domini” kwenye Gereza la Velletri lililoko nje kidogo ya mji wa Roma pamoja na kuwaosha miguu wafungwa kumi na wawili kutoka mataifa mbali mbali wanaotumikia adhabu zao gerezani hapo!

Hii ni huduma ya unyenyekevu na upendo inayopaswa kumwilishwa hata katika maisha ya wafungwa hawa gerezani. Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanajenga na kudumisha utamaduni wa Injili ya huduma ya upendo kwa maskini, mwaliko hata kwa wafungwa wenyewe kuhudumiana. Gereza hili lilifunguliwa kunako mwaka 1991 na kwa sasa linawahudumia wafungwa na mahabusu 577, kati yao asilimia 60% ya wafungwa ni kutoka nje ya Italia. Baba Mtakatifu alipowasili gerezani hapo amelakiwa na Kamanda Maria Donata Iannatuono, Mkuu wa Gereza la Velletri pamoja na wawakilishi wa askari magereza na wafungwa!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma, kama alivyofanya Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha Mitume wake miguu! Katika historia, hili ni tendo ambalo lililofanywa na watumwa! Lakini, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu alijinyenyekesha ili kuonesha mfano na kuwataka wafuasi wake wawe ni mashuhuda na vyombo vya huduma ya upendo kati yao! Wadumishe udugu katika huduma bila kutafuta masilahi ya mtu binafsi na kwamba udugu wa kweli unafumbatwa katika huduma.

Hii ni mara ya tano Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha Ibada ya Karamu ya Mwisho gerezani, utamaduni ambao amekuwa nao kwa miaka mingi kama sehemu ya maisha na utume wake, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa anawataka Maaskofu kuiga mfano wa Kristo Yesu, walau mara moja kwa mwaka, hasa wakati wa Karamu ya Mwisho, kuwakumbusha kwamba, Uaskofu ni daraja ya huduma! Kila mwamini anapaswa kujenga na kudumisha utamaduni, ari na moyo wa huduma kwa jirani zake.

Kanuni ya Injili ya Kristo Yesu ni huduma ya upendo inayomwilishwa katika unyenyekevu! Ukuu na umaarufu wa kiongozi utambulikane kwa njia ya huduma ya upendo na unyenyekevu kama ilivyo kwa watoto wadogo. Yesu aliwaonya wafuasi wake wasiwe watawala kama viongozi wa Mataifa, bali wao ni mashuhuda na vyombo vya huduma. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha yana matatizo na changamoto zake; kukosa na kukoseana ni sehemu ya maisha, kusamehe na kusahau ni mwanzo wa hija ya utakatifu wa maisha! Kumbe, huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha upendo unaomwilishwa katika huduma ili kujenga na kuimarisha udugu na urafiki katika Injili ya huduma ya upendo! Baba Mtakatifu amewaosha wafungwa miguu yao, akaibusu na kupeana mikono ya amani.

Katika Sala ya waamini, Baba Mtakatifu amewaonesha wafungwa barua waliyomwandikia, wakimwomba, awakumbuke katika Ibada hii, wale wafungwa ambao wametangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele! Baba Mtakatifu amewataka wafungwa kudumisha umoja, mshikamano na udugu kama huu hata kwa njia ya sala, ili kufarijiana na kusaidiana katika maisha! Baba Mtakatifu ameshiriki pia kuwakomunisha wafungwa wengi, waliokuwa wamejiandaa kwa toba. Amewapatia wafungwa zawadi ya Pasaka na wao pia wamemkumbuka kwa moyo wa ukarimu na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Papa: Coena Domini
19 April 2019, 12:40