Tafuta

Papa Francisko na Mfalme Mohammed VI, tarehe 30 Machi 2019 wameweka sahihi kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu. Papa Francisko na Mfalme Mohammed VI, tarehe 30 Machi 2019 wameweka sahihi kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu. 

Hija ya Papa Francisko Morocco: Tamko la Mji wa Yerusalemu 2019

Papa Francisko na Mfalme Mohammed VI: Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu na Mahali Pa Kuwakutanisha watu! Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Mji wa Yerusalemu  kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 pamoja na Mfalme Mohammed VI wa Morocco wametia sahihi kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu na Mahali Pa Kuwakutanisha watu! Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu.

Ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano. Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na udugu duniani!

Tamko Kuhusu Mji wa Yerusalemu
01 April 2019, 12:13