Tafuta

Vatican News
Papa Francisko wakati akirejea kutoka Morocco, 31 Machi 2019 amezungumzia kuhusu: Majadiliano ya kidini, wakimbizi na wahamiaji, uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri! Papa Francisko wakati akirejea kutoka Morocco, 31 Machi 2019 amezungumzia kuhusu: Majadiliano ya kidini, wakimbizi na wahamiaji, uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri!  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Morocco: Majibu kwa waandishi wa habari!

Baba Mtakatifu kama hujaji wa amani, udugu na mhudumu wa matumaini, wakati “akichonga na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake amegusia yafuatayo: Majadiliano ya kidini, Tamko kuhusu Mji wa Yerusalemu, Wakimbizi na Wahamiaji, Haki Msingi za Binadamu, Uhuru wa dhamiri na hatari ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za kifo laini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea mjini Vatican baada ya kukamilisha hija yake 28 ya kimataifa nchini Morocco kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 iliyoongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Baba Mtakatifu kama hujaji wa amani, udugu na mhudumu wa matumaini, wakati “akichonga na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake amegusia yafuatayo: Majadiliano ya kidini, Tamko kuhusu Mji wa Yerusalemu, Wakimbizi na Wahamiaji, Haki Msingi za Binadamu, Uhuru wa dhamiri na hatari ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za kifo laini.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kujibu maswali sita kutoka kwa waandishi wa mashirika mbali mbali ya habari waliokuwa kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu anasema, hija yake nchini Morocco kwa sasa imeanza kutoa maua, matunda yatakuja kwa wakati wake: Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ni: amani, umoja na udugu mambo ambayo yamebainishwa kwenye Hati ya Udugu wa Kibinadamu iliyotiwa mkwaju kati yake na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019, huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu.

Huu ni umoja unaofumbatwa katika ukarimu, kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Haya ndiyo maua ambayo yatazaa matunda kwa wakati wake na wala hakuna sababu ya kukata tamaa! Baba Mtakatifu anatambua changamoto ambazo bado zipo kutokana na uwepo wa baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani; makundi yanayotafuta kuchochea vita, kinzani na hofu! Lakini mchakato wa majadiliano ya kidini ni fursa ya kupandikiza mbegu ya matumaini, kwa kujenga utamaduni wa watu wa kukutana katika ukweli na uwazi, ili kukuza na kudumisha mawasiliano. Ujenzi wa kuta za utengano ni mwanzo wa kukwamisha mawasiliano, kujitenga na hatimaye, watu kubaki wakiwa wamejifungia katika ubinafsi wao kama wafungwa!

Kuhusu Majadiliano ya Kidini, Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchakato unaotekelezwa katika ngazi mbali mbali za maisha ya waamini, kwa kufumbata utu na heshima yao! Haya ni matunda ya tafakari ya kina kutoka moyoni na akilini; tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Haya ndiyo yaliyojitokeza katika “Tamko Kuhusu Mji wa Yerusalemu”, tamo ambalo limetiwa sahihi kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Mfalme Mohammed VI wa Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019. Ni majadiliano yanayosimikwa katika udugu, kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu huko Yerusalemu. Ni matamanio halali ya waamini na watu wenye mapenzi mema kuona Wayahudi, Waislam na Wakristo wakiishi kwa amani, kwa kutambua kwamba, waamini wa dini mbali mbali ni wenyeji wa mji wa Yerusalemu.

Kuhusu Uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na uhuru wa mtu kujieleza kadiri ya sheria, taratibu na kanuni za nchi unaendelea kukua na kupanuka nchini Morocco anasema Baba Mtakatifu Francisko. Imani inakua na kuchanua, pale waamini wanapoifahamu na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao; kwa kuwa ni dira na mwongozo wa kanuni maadili na utu wema. Imani inaendelea kukua na kuimarika kadiri ya muda unavyozidi kusonga mbele. Kanisa Katoliki limefuta adhabu ya kifo katika Mafundisho na Mapokeo yake, kwa kukazia njia zinazotetea na kulinda: maisha ya watu, amani na usalama wao dhidi ya adui; kwani hizi ni njia zinazodumisha utu, ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, miaka 300 iliyopita, wazushi waliokamatwa na kutiwa hatiani, walikuwa wanachomwa moto wangali hai! Hata ndani ya Kanisa Katoliki, kuna baadhi ya watu ambao bado wanaendelea kupinga kuhusu uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama unavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kumbe, Morocco inaendelea kujiimarisha katika utekelezaji wa uhuru wa kuabudu. Kuna baadhi ya nchi za Kiislam ambamo wananchi wao hawaruhusiwa kubatizwa na kama wanataka kubatizwa, basi waende nje ya nchi wakabatizwe na kurejea wakiwa wamebatizwa.

Hofu kubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ni kuona kwamba baadhi ya nchi zinazodai kuwa ni za Kikristo, zinapowanyima wananchi wake uhuru wa dhamiri, kwa kupandikiza utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika “kifo laini au eutanasia”. Kuna baadhi ya serikali ambazo zinawanyima wananchi wake uhuru wa dhamiri, ambao ni hatua muhimu katika kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini! Vitendo hivi vinatia huzuni na kuleta aibu kubwa!

Kuhusu Kardinali Philippe Barbarin, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lyon nchini Ufarasa, kuanzia mwaka 2002 aliyetiwa hatiani kwa kutoshirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, aliwasilisha ombi la kutaka kung’atuka kutoka madarakani, lakini Baba Mtakatifu Francisko anasema, akamkatalia hadi pale rufaa ya hukumu yake itakapotolewa! Kwa sasa Kardinali Philippe Barbarin, ameachia shughuli zote za uongozi wa Jimbo chini ya usimamizi wa Makamu wa Askofu.

Changamoto kubwa ya wakimbizi na wahamiaji duniani, anasema Baba Mtakatifu Francisko kamwe haiwezi kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga kuta za kuwatenganisha watu. Wajenzi wa kuta hizi, watajikuta wakiwa wafungwa kwenye kuta zao wenyewe kwani huu ni ukatili, ambao umemtoa chozi la uchungu. Wakimbizi na wahamiaji, wengi wao wanatumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji inapaswa kushughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika umoja wake!

Papa Francisko anasema aliwahi kuambiwa na Bwana Alexis Tsipras, Waziri mkuu wa Ugiriki kwamba, haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko mikataba ya kimataifa! Huu ni ujumbe unaobeba uzito wa hali ya juu kabisa! Changamoto inayotolewa na Mama Kanisa katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inakumbana na vikwazo kutokana na baadhi ya wanasiasa kutaka kutumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa ajili ya kujijenga kisiasa, kwa kupandikiza hofu kwa wananchi wao na huo ndio mwanzo wa utawala wa mabavu duniani kama ilivyojitokeza katika historia ya mataifa mengi! Bara la Ulaya ni kielelezo cha utajiri mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji! Hivi ndivyo ilivyo hata kwa Amerika ya Kaskazini na Kusini. Ni kweli kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanayo haki ya kubaki katika nchi zao wenyewe! Lakini, ikumbukwe kwamba, hawa ni watu wanaokimbia: vita, njaa, umaskini, dhuluma, nyanyaso pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji kujibiwa kwa kuwekeza zaidi katika elimu na uchumi fungamani, kwa kuzingatia mambo makuu manne: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji”, muhtasari wa sera na mikakati ya Kanisa Katoliki katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama njia ya kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii na udugu wa kibinadamu! Kuna nchi ambazo ni mfano bora wa kuigwa katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia; huduma inayotekelezwa kwa ukarimu na upendo mkubwa!

Kwenye Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, Baba Mtakatifu alikazia kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto wadogo, adhabu kali kutolewa; toba na wongofu wa ndani; malezi makini; uimarishaji na mapitio ya miongozo ya Mabaraza ya Maaskofu; Umuhimu wa kuwasindikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia pamoja na kuangalia ulimwengu wa kidigitali na madhara yake pamoja na kupambana na Utalii wa ngono duniani na kwamba, vitendo hivi ni kazi ya Shetani, Ibilisi! Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo hazitaweza kufahamika vyema, bila kutambua na kukiri uwepo wa dhambi duniani!

Nyanyaso za kijinsia kwa njia ya mitandao ni janga linaloenea kwa kasi kubwa, kiasi cha Jumuiya ya Kimataifa kuanza kulivalia njuga kwa mikutano wa kimataifa iliyofanyika huko Roma na Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Hii ni changamoto inayoweza pia kushughulikiwa kikamilifu na viongozi wa Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbali mbali! Utalii wa ngono na biashara yake ni mfumo unaowatajirisha watu wengi, lakini kwa kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Dhambi ya utalii wa ngono inaweza kukabiliwa kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kufunga na kusali; kwa kupambana na Shetani, Ibilisi pamoja na kuepuka nafasi za dhambi.

Nyanyaso za kijinsia zinapaswa kuangaliwa kisayansi na katika maisha ya kiroho. Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji kwa kukazia: nidhamu, toba na wongofu wa ndani; kufunga na kusali, kama silaha za mapambano dhidi ya dhambi ya nyanyaso za kijinsia! Baba Mtakatifu amehitimisha mazungumzo na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kusema, kuhusu siasa za Italia, kwa kweli hazifahamu sana, kumbe ni bure kumtwanga kwa maswali kuhusu sehemu hii!

Papa: Msawali na Majibu

 

01 April 2019, 11:44