Tafuta

Vatican News
Papa Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano amekazia umuhimu wa waamini kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na huduma ya upendo kwa maskini! Papa Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano amekazia umuhimu wa waamini kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na huduma ya upendo kwa maskini!  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko Morocco 2019: Yaliyojiri kwa ufupi!

Waamini wanapaswa kuwa ni wahudumu wa matumaini hapa duniani kwa kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu. Baba Mtakatifu anasema, amefurahia sana kuwa mhudumu wa matumaini kwa kukutana na familia ya Mungu nchini Morocco pamoja na viongozi wake wakuu. Imekuwa ni fursa ya kufanya rejea kwenye matukio makuu ya kimataifa yaliyoadhimishwa Morocco.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wakati wa katekesi yake, Jumatano, 3 Aprili 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amegusia hija yake ya kitume nchini Morocco, kwa kumshukuru Mfalme Mohammed VI wa Morocco, kwa ushuhuda na uwepo wake wa karibu kama ndugu na rafiki. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kukutana na ndugu zake waamini wa dini ya Kiislam ili kuwasha tena moto wa matumaini katika ulimwengu mamboleo. Hii ni hija inayofuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyoifanya takribani miaka 800 iliyopita, kwa kukutana na kuzungumza na Sultan Al Malik al Kamil.

Hija hii anasema Baba Mtakatifu Francisko ni mwendelezo wa hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985, baada ya kuwa amekutana na Mfalme Hassan II mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema hija zake katika nchi zenye waamini wengi wa dini ya Kiislam ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mzee Ibrahim, Baba yao katika imani. Haya ni mapenzi ya Mungu kwamba, kuwepo na dini pamoja na tamaduni mbali mbali, lakini daima waamini wakimwangalia Mwenyezi Mungu anayetaka waamini kukuza na kudumisha umoja na udugu. Hakuna sababu ya msingi, kwa waamini kuwa na wasi wasi kutokana na tofauti zao msingi, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini katika tofauti zao, wanashikamana na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, ili kusonga mbele katika hija ya maisha hapa duniani.

Waamini wanapaswa kuwa ni wahudumu wa matumaini hapa duniani kwa kujenga na kuimarisha madaraja yanayowakutanisha watu. Baba Mtakatifu anasema, amefurahia sana kuwa mhudumu wa matumaini kwa kukutana na familia ya Mungu nchini Morocco pamoja na viongozi wake wakuu. Imekuwa ni fursa ya kufanya rejea kwenye matukio makuu ya kimataifa yaliyoadhimishwa hivi karibuni nchini Morocco. Lakini, jambo ambalo limepewa kipaumbele cha kwanza ni umuhimu wa dini kulinda, kutunza na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni wajibu wa dini kudumisha, haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anakaza kusema ni katika muktadha huu, Mfalme Mohammed VI wa Morocco pamoja naye, wametoa Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu na Mahali Pa Kuwakutanisha watu! Anasema, wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu. Mji Mtakatifu wa Yerusalemu ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano. Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa.

Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na udugu duniani! Baba Mtakatifu anasema, amepata nafasi ya kutembelea Taasisi ya Mohamed V, Makaburi ya viongozi wakuu wa Morocco pamoja na kukazia umuhimu wa kukuza na kudumisha amani, umoja na udugu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, alitoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi na wahamiaji, kwa kukumbukaMkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 “Global Compact 2018”.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji kujibiwa kwa kuwekeza zaidi katika elimu na uchumi fungamani, kwa kuzingatia na kutekeleza kwa pamoja mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji”, muhtasari wa sera na mikakati ya Kanisa Katoliki katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama njia ya kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii na udugu wa kibinadamu! Kanisa nchini Morocco linaendelea kujipambanua kwa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, kama sehemu ya utekelezaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumapili, tarehe 31 Machi 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kukazia Injili ya Baba mwenye huruma anayetaka kuwashirikisha watoto wake wote amana na utajiri wa maisha ya kiroho: huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka! Nimwelekeo unaovuka mipaka ya kimaadili, kijamii, kikabila au kidini na kwamba, ni hali inayowashirikisha wote huruma na upendo wa Mungu anayetaka kuwafanyia watoto wake sherehe, ili hatimaye, wawe ni wajenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ibada hii imehudhuriwa na waamini kutoka katika mataifa 60, kielelezo makini cha ufunuo wa Mungu kati kati ya nchi ya Kiislam!

Papa: Morocco

 

03 April 2019, 16:36