Papa Francisko: Ujumbe wa Pasaka: Urbi et Orbi: Matumaini Papa Francisko: Ujumbe wa Pasaka: Urbi et Orbi: Matumaini 

PASAKA YA BWANA 2019: Ujumbe wa Pasaka: Urbi et Orbi: Matumaini

Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni chemchemi ya upyaisho wa maisha unaokita mizizi yake katika moyo na dhamiri ya mtu. Pasaka ni mwanzo wa ulimwengu mpya uliokombolewa kutoka katika dhambi na mauti; ulimwengu ambao hatimaye, umejifunua kwa ajili ya Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: upendo, amani na udugu. Kristo anaishi ndani na kati ya waja wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi”, Jumapili ya Pasaka ya Bwana, 21 Aprili 2019 anasema, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo anatangaza kwa nguvu zote kwamba, Yesu Amefufuka kweli kweli aleluiya Aleluiya. Jumapili ya Pasaka ni mwanzo wa ujana endelevu wa Kanisa na binadamu katika ujumla wao. Kiini cha Habari Njema ni hiki Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu katika Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anasema, Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana na kwa kila Mkristo ni kwamba, “Kristo anaishi anataka kila mtu aishi na kuambatana naye daima katika maisha. Kristo Mfufuka yuko kandoni mwako, anakuita na kukusubiri ili kuanza upya. Pale watu wanapojisikia kuzeeka hata kabla ya wakati kutokana na huzuni, chuki, woga au kushindwa katika maisha, Kristo Mfufuka yuko hapo ili kuwakirimia nguvu na matumaini! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ujumbe wa Kristo Mfufuka unaobubujika matumaini ni kwa ajili ya kila mtu na ulimwengu katika ujumla wake. Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni chemchemi ya upyaisho wa maisha unaokita mizizi yake katika moyo na dhamiri ya mtu.

Pasaka ni mwanzo wa ulimwengu mpya uliokombolewa kutoka katika dhambi na mauti; ulimwengu ambao hatimaye, umejifunua kwa ajili ya Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: upendo, amani na udugu. Kristo anaishi ndani na kati ya waja wake. Mwanga wa Kristo Mfufuka unawaambata waja wake na kamwe hauwezi kuwatelekeza wale wanaoishi kwenye majaribu, mateso na majanga ya maisha. Kristo Mfufuka ni matumaini ya watu wa Mungu nchini Siria; waathirika wa vita ambayo inaendelea kuwakatisha watu tamaa kiasi hata cha kutaka kuanza kuwageuzia kisogo kwa kutojali tena! Ujumbe wa Pasaka iwe ni changamoto ya kutafuta suluhu ya kisiasa ili kuzima kiu na matamanio ya wananchi wa Siria wanaolilia: uhuru, haki na amani.

Changamoto za huduma za kiutu ziangaliwe kwa mwanga wa matumaini ili wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao, wanaporejea tena nchini mwao kutoka Lebanon, Yordani pamoja na nchi jirani! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Pasaka inawaelekeza huko Mashariki ya Kati, Ukanda ambao umejeruhiwa kwa vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii. Hata katika changamoto zote hizi, Wakristo bado wanaendelea kuwa ni mashuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka na kielelezo cha ushindi wa maisha dhidi ya kifo.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa Yemen, hasa watoto ambao wanateseka sana kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha pamoja na vita. Mwanga wa Pasaka uweze kuwang’aria viongozi wa Serikali na wananchi huko Mashariki ya Kati, kwa kuanzia na Waisraeli na Wapalestina, awahimize ili waanze kuwaondolea wananchi hawa matatizo mengi yanayowasibu, tayari kuanza kujikita katika leo na kesho inayosimikwa katika msingi wa amani na utulivu. Mtutu wa bunduki na makombora huko Libya yasitishwe, kwani watu wasiokuwa na hatia, kwa siku za hivi karibuni wameendelea kupoteza maisha yao kutokana na mapambano ya silaha yanayoendelea nchini humo. Familia nyingi zimelazimika kuyaacha makazi yake na kukimbia ili kutafuta hifadhi na usalama.

Baba Mtakatifu anawasihi wadau wanaohusika katika mgogoro huu wa kivita nchini Libya kujielekeza zaidi katika majadiliano badala ya mtutu wa bunduki, ili kuzuia kuamsha tena madonda ya vita na machafuko ya kisiasa yaliyotokea takribani miaka kumi iliyopita! Kristo Mfufuka alijalie Bara la Afrika amani na utulivu kwani hadi wakati huu bado kuna: vita, kinzani za kisiasa pamoja na misimamo mikali ya kidini na kisiasa inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; ukosefu wa ulinzi na usalama pamoja na vifo hasa huko Burkina Faso, Mali, Niger, Nigeria na Cameroon. Baba Mtakatifu anaikumbuka Sudan Kongwe ambayo kwa sasa inakabiliana na hali ngumu katika historia na maisha yake, kutokana na machafuko ya kisiasa.

Baba Mtakatifu anawasihi wahusika wote kujadiliana na kusikilizana, ili kweli uhuru, ustawi na maendeleo ya muda mrefu yaweze kupatikana. Baba Mtakatifu anaiombea Sudan ya Kusini ili juhudi za viongozi wakuu wa Serikali zilizofikiwa hivi karibuni, baada ya mafungo ya kiroho yaliyofanyika mjini Vatican ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Wawe na ujasiri wa kufungua ukurasa mpya wa historia ya Sudan ya Kusini, ili wadau mbali mbali wa kisiasa, kijamii na kidini waweze kuwa na ushiriki mkamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayosimikwa katika upatanisho wa kitaifa. Baba Mtakatifu ameikumbuka familia ya Mungu nchini Ukraine, inayoendelea kuteseka kutokana na uwepo wa vita.

Kristo Mfufuka awatie shime katika juhudi za kibinadamu na kuanza mchakato wa utafutaji wa amani ya kudumu. Furaha ya Kristo Mfufuka ijaze nyoyo za wananchi wa Bara la Amerika linalokabiliana na hali ngumu ya kisiasa na kiuchumi. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa Venezuela, wanaoishi katika hali tete na mazingira magumu kutokana na hali tete ya kisiasa nchini humo! Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Mfufuka awawezeshe wahusika wa kisiasa kuanza kujielekeza ili kukomesha ukosefu wa haki jamii, nyanyaso mbali mbali pamoja na ghasia, kwa kujikita katika mchakato wa kuganga na kuponya kinzani na mipasuko iliyiopo, ili hatimaye, misaada mbali mbali iweze kuwafikia wananchi wanaoteseka sana.

Papa Francisko amewakumbuka pia wananchi wa Nicaragua, ili Kristo Mfufuka aweze kuwaangazia viongozi wahusika, ili juhudi zinazoendelea kufanyika nchini humo ziweze kusaidia hupatikanaji wa amani ya kudumu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Nicaragua! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa “Urbi et Orbi” kwa Pasaka ya Mwaka huu, anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na mshikamano kwa watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Awawezeshe wawe kweli ni madaraja ya kuwakutanisha watu na wala si kuta zinazowagawa na kuwatenganisha watu. Awajalie amani, ili mtutu wa bunduki uweze kukoma katika uwanja wa vita, katika miji mbali mbali na awawezeshe viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete hasa kwenye nchi tajiri zaidi duniani, ili hatimaye, kusitisha mashindano ya utengenezaji, ulimbikizaji na usambazaji wa silaha unaotishia amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mwishoni wa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anasema, Kristo Mfufuka aliyefungua malango ya kaburi, aweze kufungua nyoyo zao ili kuguswa na mahitaji msingi ya: maskini na wanyonge; watu wasiokuwa na fursa za kazi na ajira; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu wanaobisha hodi kwenye malango wakitafuta chakula, hifadhi na usalama pamoja na kutambuliwa utu na heshima yao kama binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ni chemchemi ya matumaini na ujana wa kila mtu na kwa ajili ya ulimwengu katika ujumla wake. Anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwachia nafasi Kristo Yesu, ili aweze kuwapyaisha tena!

Papa: Urbi et Orbi 2019
21 April 2019, 14:57