Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume "Verbum Domini" anakazia: Umuhimu wa Neno la Mungu katika Liturujia, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume "Verbum Domini" anakazia: Umuhimu wa Neno la Mungu katika Liturujia, Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.  (Vatican Media)

Wosia wa Kitume: Neno la Mungu: Liturujia, Kanisa & Ulimwengu

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa Neno la Mungu katika Kanisa “Verbum in Ecclesia”. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kitovu cha: Liturujia ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti na mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira na mwongozo katika maisha na utume wa Kanisa. Lipewe msuko wa pekee katika majiundo ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na limeeneza utume wake katika nchi 68 duniani. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 27 Aprili 2019 amezungumza na wajumbe wa Kongamano la Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia. Katika hotuba yake, amekazia: utume wa Shirikisho hili katika kuhakikisha kwamba, linaeneza Neno la Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kwa sababu Neno la Mungu ni maisha na ni chemchemi ya maisha na kamwe haliwezi kuzeeka wala kupitwa na wakati!

Neno la Mungu ni chombo kinachotumiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa na kamwe halina mbadala. Baba Mtakatifu anawahimiza wakleri kuhakikisha kwamba, wana andaa vyema mahubiri yao kwa kutambua kuwa mahubiri yao si maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali ni dalili za Roho na nguvu, ili kuimarisha imani, isibaki katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu. Kanisa la Kristo linajengwa na kuimarishwa kwa njia ya Neno la Mungu, kumbe, kila mwamini anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Biblia na maisha ni chanda na pete na kamwe zisiwe ni mapambo kwenye makabati ya vitabu majumbani!

Kwa upande wake, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Kikatoliki vya Biblia katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko amegusia mambo msingi yaliyojiri katika kongamano hili ambalo ni matunda ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Verbum Domini” yaani “Neno la Mungu” uliochapishwa Septemba 2010. Katika Wosia huu, alikazia umuhimu wa Neno la Mungu “Verbum Dei” linalobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwitikio wa waamini kwa Neno la Mungu pamoja na tafsiri sahihi ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa Neno la Mungu katika Kanisa “Verbum in Ecclesia”. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kitovu cha: Liturujia ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti na mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira na mwongozo katika maisha na utume wa Kanisa. Lipewe msukumo wa pekee, katika hatua mbali mbali za malezi, makuzi na majiundo ya kipadre na kitawa bila kuwasahau waamini walei. Familia zijenga utamaduni wa kusoma, kusali na kulitafakari Neno la Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia huu wa Kitume anagusia umuhimu wa Neno la Mungu Ulimwenguni, “Verbum Mundo”. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Neno la Mungu liwe ni chachu ya haki, amani na upatanisho. Liwe ni chombo cha huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji, faraja na amani kwa maskini na wagonjwa. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji, yaani mazingira nyumba ya wote. Neno la Mungu liwe ni chachu ya majadiliano ya kitamaduni, kiekumene na kidini. Waamini wajitahidi kutamadunisha Neno la Mungu katika maisha yao, liwe ni kikolezo cha mawasiliano ya kijamii. Kimsingi, Neno la Mungu liwe ni chachu ya uhuru wa kidini, chemchemi ya furaha, amani na utakatifu wa maisha!

Papa: Dei Verbum
29 April 2019, 10:23