Papa Francisko amewahimiza wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kujikita zaidi katika kutetea uhai, utu na heshima ya binadamu! Papa Francisko amewahimiza wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kujikita zaidi katika kutetea uhai, utu na heshima ya binadamu! 

Papa Francisko: Waandishi wa habari: lindeni uhai na utu wa watu

Baba Mtakatifu anasema kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kutendeka duniani dhidi ya haki ya mtu kuishi na kwamba, utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika dhana ya kifo laini au Eutanasia, unazidi kuenea sana! Pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kupanuka, kiasi cha kukosekana usawa wa kijamii pamoja na kushindwa watu kushirikishwa katika maiisha ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 4 Aprili 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani pamoja na Kanisa la Kiinjili nchini Ujerumani; wanaoendeleza majadiliano ya kiekumene katika vipindi vya Televisheni nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa hatua hii inayojikita katika majadiliano yanayowasaidia kufahamiana, kwa kushirikishana habari, maoni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu! Juhudi zote hizi ni kwa ajili ya mafao ya familia ya Mungu nchini Ujerumani.

Baba Mtakatifu anawahimiza wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete katika mapambano dhidi ya habari za kughushi, “fake news”, kwa kuzingatia utafiti unaofumbatwa katika ukweli badala ya kukimbilia kwenye “vichwa vya habari” ambavyo haviendani na ukweli unaotangazwa! Baba Mtakatifu anasikita kusema kwamba, kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kutendeka duniani dhidi ya haki ya mtu kuishi na kwamba, utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika dhana ya kifo laini au Eutanasia, unazidi kuenea kwa kasi ya ajabu!

Pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kupanuka, kiasi cha kukosekana usawa wa kijamii pamoja na kushindwa watu kushirikishwa katika maiisha ya jamii. Kuna uvunjwaji mkubwa wa utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na uhuru wa dhamiri ambao wengi wanashindwa kuuheshimu. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, ni wajibu na dhamana ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kuchukua msimamo ili kulinda na kudumisha uhuru wa binadamu. Katika dhamana hii, Makanisa yataendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji wa shughuli zao na kama sehemu ya umwilishaji wa Agizo la Kristo Yesu, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele!

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kazi na mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika shughuli zao za kila siku hapataweza kukosekana Habari Njema, inayopaswa kusimuliwa, ili kuchochea matumaini. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia wajumbe hawa baraka zake za kitume, ili waweze kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Amewaomba wao pia kumkumbuka katika sala zao!

Papa: Makanisa Ujerumani
04 April 2019, 15:31