Tafuta

Papa Francisko: Siku ya Michezo Duniani: Chemchemi ya furaha na shule ya tunu msingi za kiutu na kijamii na ni lugha ya kimataifa! Papa Francisko: Siku ya Michezo Duniani: Chemchemi ya furaha na shule ya tunu msingi za kiutu na kijamii na ni lugha ya kimataifa! 

Papa Francisko: Siku ya Michezo Duniani 2019: Ujumbe!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo ni lugha ya kimataifa inayowaambata wote. Michezo ni chemchemi ya furaha, ari na mwamko mkubwa; ni shule ambamo tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii zinakuzwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi wa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake! Anawataka watu wenye mapenzi mema kuchangamkia maisha kama michezo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 3 Machi 2019, ameyaelekeza mawazo yake kwenye Siku ya Michezo Duniani kwa ajili ya amani na maendeleo fungamani iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa. Baba Mtakatifu anasema, michezo ni lugha ya kimataifa inayowaambata na kuwakumbatia wote. Michezo ni chemchemi ya furaha, ari na mwamko mkubwa; ni shule ambamo tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii zinakuzwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi wa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, watu wengi zaidi watajizamisha kwenye maisha ya kawaida kama ilivyo katika michezo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kwamba, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja kuwa na upendeleo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili.

Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamemekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Siku ya Michezo Duniani 2019
03 April 2019, 16:08