Papa Francisko: sala ya Yesu imefikia kilele chake katika mateso na kifo cha Msalaba, lakini akawa na nguvu ya kusamehe watesi wake! Papa Francisko: sala ya Yesu imefikia kilele chake katika mateso na kifo cha Msalaba, lakini akawa na nguvu ya kusamehe watesi wake! 

Papa Francisko: Sala ya Yesu katika mateso na kifo cha Msalaba!

Waamini wajifunze kujisadaka na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu wakati wa mateso na mahangaiko ya ndani, kwa njia ya sala! Waamini waombe nguvu ya msamaha, ili waweze hata wao kuwasamehe wale wanaowakosea. Kutoa na kupokea msamaha ni mambo yanayokamilishana anasema Papa Francisko. Sala ya Yesu kilele chake ni Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Juma kuu ni wakati muafaka wa kusali, kutafakari na kumsindikiza Kristo Yesu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu! Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu akiwa amezungukwa na Mitume wake, alisali akimwambia Baba yake wa mbinguni kwamba, saa yake imefika na kumwomba, ili aweze kumtukuza, na hatimaye, Mwana aweze kumtukuza Baba, Kama vile alivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba, wote aliopewa waweze kupata uzima wa milele.

Hii ni sala ambayo Yesu anaitumia kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wake. Mwenyezi Mungu alijifunua kwa watu wake kwa kuwakomboa kutoka utumwani Misri, akawaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini, akaendelea kujifunua miongoni mwa Manabii wake watakatifu na kwamba, utukufu wake, uling’aa na kuliambata Hekalu la Yerusalemu. Kwa namna ya pekee, Mwenyezi Mungu ameonesha utukufu wake kwa njia wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu!

Utukufu wa Mungu ni upendo wake usiokuwa na kifani, wala mawaa kiasi kwamba unapita uelewa na ufahamu wa kibinadamu! Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wana mwilisha Sala ya Yesu, ili waweze kumwona na kumpokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kama Baba na chemchemi ya upendo! Ni mwaliko wa kuondokana na mawazo ya kumwona Mungu kuwa ni Baba mkatili, hakimu asiyekuwa hata na chembe ya huruma. Lakini, Mwenyezi Mungu ni Mkombozi, mwingi wa huruma na mapendo. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, anajifunua katika hali ya unyenyekevu na katika upendo unaodai kujibiwa kwa upendo wa dhati, kwa kufikiri na kutenda kama anavyotaka Mwenyezi Mungu.

Huu ni muhtasari wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatano, tarehe 17 Aprili 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ufunuo wa kweli wa Mwenyezi Mungu ni upendo wake unaowapatia watu maisha na uzima wa milele. Ni upendo unaojikita katika ndiyo ya kweli katika maisha, kwa kuondokana na ubinafsi, ili kutoa nafasi kwa jirani waweze kuonekana na kustawi kama Mtende wa Lebanoni. Katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu anamtukuza Mwanaye mpendwa Kristo Yesu ambaye pia anamtukuza Baba yake wa mbinguni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kushuhudia utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kuwa tayari kutoa kuliko kupokea! Baada ya Karamu ya mwisho, Yesu “alijichimbia” Bustanini Gethsemane ili kusali na kumwomba Baba yake wa mbinguni. Ilikuwa ni fursa ya kujiaminisha na kujiachilia mikononi mwa Baba yake wa mbinguni! Alionja usaliti mkubwa, dharau na kejeli, mateso na uchungu mkali uliopenya katika moyo wake. Fundisho kuu anasema Baba Mtakatifu kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, hata katika mateso na majaribu makubwa, daima wakimbilie katika sala, ili kupata tena nguvu ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Sala ni chemchemi ya faraja, ni hali ya kujiaminisha mbele ya Mungu ni bandari salama katika maisha ya mwamini! Katika mahangaiko yake yote, Yesu daima aliendelea kuambatana na Baba yake wa mbinguni, mwaliko kwa waamini kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wanapokuwa katika shida na mahangaiko na wakashindwa kujiaminisha kwa Mungu, hapo watambue kwamba, wanajichimbia shimo kubwa na anguko lao ni kubwa, kwani wanaweza kumezwa na upweke hasi, alama ya mateso, mahangaiko na hata kifo. Matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha, lakini jinsi ya kupambana nazo huo ndio mwanzo wa hekima! Jambo la kwanza ni kujikita katika sala, ili kujenga mahusiano na kujiaminisha kwa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu akiwa Bustanini Gethsemane alipambana sana, mwaliko kwa kila mwamini kuingia katika Gethsemane ya maisha yake, ili kuanza mapambano kwa njia ya Sala ya Baba Yetu! Mwishoni, Kristo Yesu anasali na kuwaachia urithi mkubwa wa sala ya kuombea msamaha akisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”. Lk. 23: 34. Hii ni sala iliyokuwa inabubujika wakati Kristo Yesu akiwa ametundikwa Msalabani, wakati miguu na mikono yake ikifungwa kwa misumari. Ni katika mazingira haya, upendo wa Kristo unafikia kilele chake kiasi hata cha kusamehe na kusahau mateso yake makali. Msamaha unavunjilia mbali ubaya wa moyo!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaposali, waombe neema ya kuishi katika utukufu wa Mungu, kwa kuambata upendo katika maisha yao. Wajifunze kujisadaka na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu wakati wa shida, mateso na mahangaiko ya ndani, kwa njia ya sala! Waamini waombe nguvu ya msamaha, ili waweze hata wao kuwasamehe wale wanaowakosea. Kutoa na kupokea msamaha ni sawa na chanda na pete, ni mambo yanayokamilishana anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Papa: Sala ya Yesu
17 April 2019, 16:20