Tafuta

Papa Francisko, tarehe 15 Aprili 2019 amemtembelea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ili kumtakia Heri na Baraza kwa Pasaka na Kumbu kumbu ya Miaka 92 ya kuzaliwa kwake! Papa Francisko, tarehe 15 Aprili 2019 amemtembelea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ili kumtakia Heri na Baraza kwa Pasaka na Kumbu kumbu ya Miaka 92 ya kuzaliwa kwake! 

Papa Francisko amtembelea Benedikto XVI na kumtakia Pasaka Njema

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 15 Aprili 2019 alikwenda kumtembelea Papa Mstaafu Benedikto XVI, ili kumtakia heri na baraka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Imekuwa ni nafasi ya pekee kwa Papa Francisko kumtakia: baraka, afya, imani na matumaini, Baba Mtakatifu Benedikto XVI ambaye, tarehe 16 Aprili 2019 anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 92 tangu alipozaliwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Jumuiya ya kwanza ya waamini iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; ikauendeleza katika Mapokeo ya Kanisa na kuthibisha kwa njia ya Maandiko Matakatifu hususan Agano Jipya. Wakristo hawa wakajitahidi kuutangaza na kuushuhudia kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka sanjari na Fumbo la Msalaba. Ni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumshikirisha maisha na uzima wa milele!

Ni katika muktadha huu wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 15 Aprili 2019 alikwenda kumtembelea Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae, ili kumtakia heri na baraka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Imekuwa ni nafasi ya pekee kwa Papa Francisko kumtakia heri na baraka, afya, imani na matumaini, Baba Mtakatifu Benedikto XVI ambaye, tarehe 16 Aprili 2019 anaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 92 tangu alipozaliwa. Taarifa hii imetolewa na Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa mpito mjini Vatican.

Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927 nchini Ujerumani, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 29 Juni 1951. Tarehe 28 Mei 1977 akawekwa wakfu kuwa Askofu na tarehe 27 Juni 1977 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Kardinali. Tarehe 19 Aprili 2005 akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na tarehe 28 Februari, 2013 kwa hiyari yake mwenyewe akaamua kung’atuka kutoka madarakani.

Benedikto XVI: Miaka 92
16 April 2019, 10:30