Papa Francisko anasema: Madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea ni kielelezo cha matumaini katika maeneo ya vita! Papa Francisko anasema: Madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea ni kielelezo cha matumaini katika maeneo ya vita! 

Nia za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Aprili 2019: Maeneo ya vita!

Papa Francisko: Faraja kubwa ni kuona uwepo wa madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea wanaojisadaka bila ya kujibakiza hata wakati mwingine, kwa kuhatarisha maisha yao wenyewe, ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia na mipasuko mbali mbali ya kijamii! Uwepo wa watu hawa katika maeneo ya vita ni alama ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Aprili 2019 anapenda kuyaelekeza mawazo yake kwa madaktari, wahudumu wa sekta ya afya pamoja na watu wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia watu wanaoteseka kwenye maeneo ya vita, ghasia na kinzani mbali mbali za kijamii. Baba Mtakatifu anasema, amani ni tema muhimu sana miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani kutokana na ukweli kwamba, leo hii, vitendo vya kigaidi na wongofu wa shuruti vinatishia amani, kiasi hata cha kuzua vita, machafuko na mipasuko ya kijamii.

Ukosefu wa amani unajidhihirisha hata katika kuta za kifamilia, maeneo ya kazi, kwenye mashirika, vitongojini na hata katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, binadamu kamwe haonekani kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na matokeo yake, anakuwa ni sababu ya uhasama, chuki na hasira na vita! Amani ya kweli inasimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili, changamoto kwa watu wote ni kujenga na kudumisha Injili ya amani na huduma ya upendo miongoni mwa watu wa Familia ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Aprili, 2019 katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anayaangalia mateso na mahangaiko ya watu walioko kwenye maeneo ya vita! Faraja kubwa ni kuona uwepo wa madaktari, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea wanaojisadaka bila ya kujibakiza hata wakati mwingine, kwa kuhatarisha maisha yao wenyewe, ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia na mipasuko mbali mbali ya kijamii! Uwepo watu wa hawa katika maeneo ya vita ni alama ya matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wenye hekima, jasiri na wema, wanaotekeleza dhamana, wajibu na wito wao katika maeneo na mazingira magumu na hatarishi! Mtandao wa utume wa sala kimataifa, unaendelea kusamba ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa njia ya video, ili kuwashirikisha waamini na watu wenye mapenzi mema, mahangaiko na mateso yanayogusa kwa namna ya pekee maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia! Ukiuupata ujumbe huu, mshirikishe pia jirani yako, ili kujenga mtandao mpana zaidi wa utume wa sala!

Papa: Nia Mwezi Aprili

 

10 April 2019, 11:43