Papa Francisko anawataka wataalam kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo katika utume wao sehemu mbali mbali za dunia! Papa Francisko anawataka wataalam kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo katika utume wao sehemu mbali mbali za dunia! 

Papa Francisko: Wataalam shuhudieni tunu msingi za Kikristo!

Mtakatifu Martin de Porres alikubali na kupokea hali yake, kwa unyenyekevu mkubwa unaong’ara upendo. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa; akawa akiwapatia tiba na dawa, utaalam aliokuwa amejifunza hapo awali katika kuhangaika na maisha. Akafariki dunia mwaka 1639. Mwaliko kwa wataalam kushuhudia tunu msingi za Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kamati ya Chama cha vinyozi wa Mtakatifu Martin de Porres, Mtawa inayoundwa na wanakamati 230, kutoka sehemu mbali mbali za Italia, Jumatatu, tarehe 29 Aprili 2019 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hija hii ni sehemu muhimu sana katika kukuza na kudumisha imani ya Kikristo na mwelekeo wa kidini unaofumbatwa katika chama hiki cha vinyozi. Ni chama ambacho kiko chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Martin de Porres, Mtawa kutoka Peruvia, aliyejipatia mahitaji yake msingi kwa kujifunza kazi ya kunyoa watu, ushauri alioupata kutoka kwa Mama yake mzazi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kuhusu wasifu wa Mtakatifu Martin de Porres kwa kusema kwamba, kutokana na hali na mazingira ya wakati ule, haikuwa rahisi sana, kwa watu wenye asili ya Kiafrika kupokelewa katika maisha ya kitawa. Ni Shirika la Wadominican lililompokea na kumkubali kuwa ni sehemu ya utawa wa watatu, hali ambayo ilipata upinzani mkubwa kwa watu wa nyakati zile. Lakini, Mtakatifu Martin de Porres alikubali na kupokea hali yake, kwa unyenyekevu mkubwa unaong’ara upendo. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa; akawa akiwapatia tiba na dawa, utaalam aliokuwa amejifunza hapo awali katika kuhangaika na maisha.

Martin De Porres akafariki dunia mwaka 1639. Kunako mwaka 1837 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Gregori XVI na hatimaye kutangazwa kuwa Mtakatifu kunako mwaka 1962 na Mtakatifu Yohane XXIII. Mtakatifu Paulo VI akamtangaza kuwa msimamizi wa vinyozi duniani, changamoto na mwaliko kwa waamini kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kikristo katika taaluma zao. Vinyozi anasema Baba Mtakatifu Francisko wanapaswa kuwahudumia wateja wao kwa wema na ukarimu, wakiwapatia maneno ya faraja na kuwatia shime, daima wakijitahidi kukwepa kishawishi cha kutumbukia katika “umbea” kwani matokeo yake ni kuchafua kazi nzuri inayotekelezwa na vinyozi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, vinyozi hawa kila mtu kadiri ya utaalam wa kazi yake, atajitahidi kutenda kazi kwa unyoofu, huku akijaribu kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi ndani ya jamii. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume, akiwaombea mapaji ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao! Amewaomba hata wao, kuendelea kumkumbuka katika maisha na utume wake, kwa njia ya sala na sadaka zao!

Papa: Martin De Porres
29 April 2019, 16:35