Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka Mtakatifu Katarina wa Siena, Mtawa, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka Mtakatifu Katarina wa Siena, Mtawa, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. 

Kumbu kumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, 29 Aprili 2019

Mtakatifu Katarina wa Siena alijisadaka sana kwa ajili ya umoja wa Kanisa, akasali na kujitosa kwa moyo wake wote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwomba Mtakatifu Katarina wa Siena ili aweze kuombea umoja wa Kanisa na kuisaidia Italia katika kipindi hiki kigumu cha historia yake, bila kulisahau Bara la Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 29 Aprili, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Katarina wa Siena, Bikira na Mwalimu wa Kanisa. Katarina kwa Kigiriki maana yake ni “Mwanamke asiyekuwa na mawaa”. Huyu alikuwa ni mtawa wa Shirika la Wadominikani, mwanataalimungu mahiri, mwanafalsafa wa kutupwa na mtu aliyekuwa na maono makubwa katika maisha. Alifariki dunia kunako tarehe 29 Aprili 1380 akiwa mjini Roma. Papa Pio II akamtangaza kuwa mtakatifu kunako mwaka 1461.

Na kunako tarehe 4 Oktoba 1970, Mtakatifu Paulo VI akamtangaza Katarina wa Siena kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Ilikuwa ni mwaka 1939 Papa Pio XII alipomtangaza kuwa ni Msimamizi wa Italia pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi, yaani miaka 80 iliyopita! Katika historia na maisha yake, anakumbukwa sana kama mjumbe wa amani, mshauri wa Mababa watakatifu waliolazimika kukimbilia uhamishoni kutokana na misigano ya kisiasa. Alikuwa kweli ni mwanamke wa shoka, aliyesaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani, unaosimikwa katika Injili ya upendo; amani na upatanisho wa kweli.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican, 29 Aprili 2019, mwanzoni mwa Ibada amemkumbuka, Mtakatifu Katarina wa Siena kama Msimamizi wa Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake. Ni Mtakatifu aliyejisadaka kwa ajili ya umoja wa Kanisa, akasali na kujitosa kwa moyo wake wote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kumwomba Mtakatifu Katarina wa Siena ili aweze kuombea umoja wa Kanisa na kuisaidia Italia katika kipindi hiki kigumu cha historia yake, bila kulisahau Bara la Ulaya.

Papa: Katarina wa Siena

 

29 April 2019, 14:56