Tafuta

Vatican News
Papa Francisko kwa heshima na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, amewapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini akiomba amani ya kudumu kwa ajili ya watu wao! Papa Francisko kwa heshima na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa, amewapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini akiomba amani ya kudumu kwa ajili ya watu wao! 

Papa Francisko awapigia magoti viongozi wa Sudan akiomba amani!

Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni kielelezo cha kilio cha ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu anayeguswa na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kutokana na vita, njaa na magonjwa pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu mambo yanayoendelea kusababisha maafa na majanga makubwa nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Baada ya kipindi cha sala, tafakari na upatanisho kwa ajili ya amani kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2019, Baba Mtakatifu Francisko alipiga magoti kwa unyenyekevu na heshima kubwa na kuanza kubusu miguu ya viongozi wa Sudan ya Kusini, wanaotarajia kuanza utekelezaji wa muundo wa Serikali ya mpito, hapo tarehe 12 Mei 2019. Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni kielelezo cha kilio cha ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu anayeguswa na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kutokana na vita, njaa na magonjwa!

Ni kitendo kinachovuka protokali za kidiplomasia, lakini kinaeleweka kwa watu wanaotambua mateso ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao wanakiu ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Sudan ya Kusini kushinda kishawishi cha utengano, kinzani, mipasuko na vita na kuanza kukumbatia na kuambata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Katika kipindi hiki cha mpito, matatizo na changamoto kamwe haziwezi kukosekana, lakini jambo la muhimu ni kutambua kwamba, wao ni wananchi na waasisi wa Sudan ya Kusini, wanaotegemewa kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu anasema, Injili ya amani inasimikwa katika kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watambue kwamba kama viongozi wanawajibika mbele ya Mungu na mbele ya raia wao wanaotamani kuona haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa vikitawala tena Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani inawezekana Sudan ya Kusini, kinachotakiwa kwa sasa ni utashi wa kisiasa unaofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Sudan ya Kusini.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Sudan ya Kusini, kusikiliza kilio cha maskini na watu wanaoteseka, kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi inayotoka kwa Mungu lakini inamwajibisha binadamu kuitafuta, kuitunza na kuiendeleza, ili kukuza: haki, umoja na udugu. Amani inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano, msamaha na upatanisho wa kweli, ili hatimaye, viongozi hawa wa Sudan ya Kusini, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anawasihi kutafuta na kuambata yale yanayowaunganisha; kuvuka vikwazo vya yale yote yanayowagawa na kuwasambaratisha!

Viongozi watambue kwamba, wananchi wa Sudan ya Kusini, wamechoka na vita ambavyo vimewasababishia majanga na maafa makubwa katika maisha yao. Wananchi wanatamani leo na kesho iliyo bora zaidi, inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na upatanisho! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana pamoja na viongozi wengine wa Makanisa wataweza kutembelea Sudan ya Kusini, kama kielelezo cha uekumene wa sala na huduma ya upendo na mshikamano wa dhati, ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini nchini Sudan ya Kusini, watakuwa kweli mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa. Ushuhuda huu unapaswa kufumbatwa katika sala, maongozi ya maisha ya kiroho na huduma makini, kielelezo cha imani inayofumbatwa katika matendo!

Papa: sudan ya Kusini
12 April 2019, 07:52