Papa Francisko: Madonda Matakatifu ya Yesu ni chemchemi ya amani, furaha ya kweli na utume wa Kanisa! Papa Francisko: Madonda Matakatifu ya Yesu ni chemchemi ya amani, furaha ya kweli na utume wa Kanisa! 

Papa Francisko: Zawadi ya Kristo Mfufuka: Amani, Furaha na Utume

Madonda Matakatifu ya Yesu ni amana ya huruma ya Mungu na gharama aliyolipia kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Zawadi ya Kristo Mfufuka ni amani, furaha na utume wa kutangaza na kushuhudia habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kukimbilia kwenye Madonda Matakatifu ya Yesu; chemchemi ya amani, furaha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, mwanadamu amekirimiwa zawadi ya amani na upatanisho na Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yesu ameshinda dhambi na mauti. Mitume walioguswa na kutikiswa sana na kashfa ya Msalaba, iliyowazamisha kwenye hofu na woga, walihitaji amani na utulivu wa ndani. Kristo Mfufuka, alisimama kati kati yao, akawaonesha Madonda yake Matakatifu yaliyobaki kwenye mwili wake mtukufu na kuwakirimia amani, tunda la ushindi wake. Wakati huu alikuwepo Tomaso aitwaye Pacha, ambaye hapo awali alikataa katu katu kuamini kwamba, Kristo Yesu alikuwa amefufuka kwa wafu kwa kutaka kuhakikisha mwenyewe kwa kuziona kovu na kutia mkono wake kwenye ubavu wa Yesu!

Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena na Tomaso pamoja nao, Kristo Yesu, akawatokea na kumtaka Tomaso atazame madonda yake  na kutia mkono ubavuni mwake. Madonda Matakatifu ya Yesu ni chemchemi amani na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ameshinda dhambi na mauti. Kwa wale wote wasiokuwa na amani wala utulivu wa ndani, wanaalikwa na Kristo Mfufuka kugusa Madonda yake Matakatifu! Haya ndiyo matatizo na changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Madonda Matakatifu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, ambayo imeadhimishwa na Mama Kanisa, tarehe 28 Aprili 2019. Huruma ya Mungu inawaambata na kuwakumbatia wote na kwamba, watu wote wametindikiwa na hivyo wanahitaji huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya huruma ya Mungu.

Madonda Matakatifu ya Yesu ni amana ya huruma ya Mungu na gharama aliyolipia kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu, yuko mbele ya Baba yake wa mbinguni akiwaombea waja wake. Zawadi ya pili kutoka kwa Kristo Mfufuka ni furaha kubwa iliyotanda miongoni mwa wafuasi wake kwa kumwona tena Kristo Mfufuka. Kwa wale wote wanao ogelea katika dimbwi la huzuni na hali ya kukata tamaa, wakimbilie kwenye Madonda Matakatifu ya Yesu, humo watakirimiwa furaha ya kweli!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, zawadi ya tatu kutoka kwa Kristo Mfufuka ni utume wa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwanzo mpya unaofumbatwa katika upendo, wenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika maisha ya mwanadamu, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kumwendea Kristo Yesu kwa imani, kwa kumfunulia nyoyo zao ili awakirimie: amani, furaha na nguvu ya utume wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha. Hatimaye, Baba Mtakatifu amewaweka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa mbingu na nchi!

Papa: Amani, Furaha na Utume
29 April 2019, 16:17