Tafuta

Vatican News
Mfuko wa Missionzentrale der Franziskaner, Ujerumani unaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wa Injili ya upendo na mshikamano duniani! Mfuko wa Missionzentrale der Franziskaner, Ujerumani unaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo na utume wa Injili ya upendo na mshikamano duniani! 

Papa Francisko: Dumisheni, upendo na mshikamano wa Kiinjili!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni katika muktadha huu, Kituo cha Missionszentrale der Franziskaner tangu mwanzo kimekuwa ni mtandao wa kimataifa wa upendo, mshikamano na udugu. Mtakatifu Francisko wa Assisi katika mahangaiko ya ujana wake, alisikia sauti ya Kristo Yesu, ikimtaka kwenda kumjengea nyumba yake iliyokuwa inageuka kuwa magofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Missionszentrale der Franziskaner ni Kituo cha Wamisionari wa Kifranciskani kinachowaunganisha: Watawa, waamini walei pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaotaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sehemu mbali mbali za dunia. Kituo hiki kinapania kuwajengea watu leo na kesho iliyo bora zaidi mintarafu Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Kwa sasa kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake!

Kituo hiki cha Kifranciskani, hiki kinatekeleza dhamana na utume wake, chini ya Parokia ya Bonn-Bad Godesberg iliyoko nchini Ujerumani. Kituo hiki kwa muda mrefu kimekuwa chini ya uongozi wa Padre Andreas Mùller ambaye amejitahidi kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyekubali kuguswa kwa namna ya pekee, na umaskini wa watu wa Mungu. Na kwa njia hii, akabarikiwa kupata amani iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu na hatimaye, akawa ni mwamini aliyebahatika kumwilisha katika maisha yake, neema ya Mungu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Aprili 2019 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Kituo cha Wamisionari wa Kifranciskani kutoka Ujerumani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni katika muktadha huu, Kituo hiki, tangu mwanzo kimekuwa ni mtandao wa kimataifa wa upendo, mshikamano na udugu. Mtakatifu Francisko wa Assisi katika mahangaiko ya ujana wake, alisikia sauti ya Kristo Yesu, ikimtaka kwenda kumjengea nyumba yake iliyokuwa inageuka kuwa magofu!

Mtakatifu Francisko wa Assisi licha ya udhaifu na mapungufu ya Kanisa la wakati wale, akajifunga kibwebwe kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, katika ukweli na uwazi. Hata leo hii, bado Kanisa linapambana na changamoto za udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu na mwaliko wa Kristo Yesu ni kuisikiliza sauti yake tayari kupyaisha na kuyatakatifuza malimwengu! Dhamana hii inaweza kutekelezwa ikiwa kama waaamini wataweza kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini na kumwachia nafasi ya kupyaisha, ili kushikamana na kuendelea kutekeleza mema pamoja naye. Changamoto mamboleo zinapaswa kuvaliwa njuga kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni katika mazingira haya, Kituo hiki cha Wamisionari wa Kifranciskani kitaendelea kuchangia amana na utajiri wake, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu anawatakia wajumbe wote maadhimisho mema ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kituo hiki. Iwe ni Jubilei ya furaha na imani ya Kifranciskani. Anawataka wadumishe maendeleo kwa wote sanjari na kulinda mazingira nyumba ya wote.

Papa: Injili ya Upendo
06 April 2019, 15:37