Papa Francisko: Sala baada ya Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo: Fumbo la Msalaba katika ulimwengu mamboleo! Papa Francisko: Sala baada ya Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo: Fumbo la Msalaba katika ulimwengu mamboleo! 

Ijumaa kuu 2019: Njia ya Msalaba: Fumbo la Msalaba ulimwenguni

Papa Francisko: Fumbo la Msalaba: Huu ni Msalaba wa watu wenye njaa ya upendo; watu pweke na waliotelekezwa hata na watoto pamoja na ndugu zao wenyewe. Ni Msalaba wa watu wenye kiuu ya haki na amani; waamini ambao hawajisikii kupata faraja katika imani! Huu ni Msalaba wanaokandamizwa chini kutokana na uzito wa umri na upweke hasi unaowaachia machungu moyoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa kuu usiku, tarehe 19 Aprili 2019 ameongoza Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Kwa mwaka 2019, imeandaliwa na Sr. Eugenia Bonetti wa Shirika la Consolata ambaye pia ni Rais wa Chama cha Kiraia “Slaves No More”. Kiini cha tafakari hii ni mateso, nyanyaso na dhuluma zinazojitokeza katika biashara ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Sr. Eugenia Bonetti anasema, kauli mbiu ya tafakari hii ni “Pamoja na Kristo na Wanawake kwenye Njia ya Msalaba” yenye Vituo 14 kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki.

Mara baada ya Njia ya Msalaba, Baba Mtakatifu ametoa Sala iliyogusa Fumbo la Msalaba katika ulimwengu mamboleo. Huu ni Msalaba wa watu wenye njaa ya upendo; watu pweke na waliotelekezwa hata na watoto pamoja na ndugu zao wenyewe. Ni Msalaba wa watu wenye kiu ya haki na amani; waamini ambao hawajisikii kupata faraja katika imani! Huu ni Msalaba wa wale wanaokandamizwa chini kutokana na uzito wa umri na upweke hasi unaowaachia machungu moyoni! Ni Msalaba wa wahamiaji na wakimbizi, wanaokumbana na “malango ya chuma” yakiwa yamefungwa kwa hofu zisizo na msingi pamoja na masilahi ya wanasiasa.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali kwa kusema, huu ni Msalaba wa watoto wadogo wasiokuwa na hatia, waliojeruhiwa katika utu na heshima yao; ni Msalaba wa watu wanaotembea katika giza la maisha yasiyokuwa na uhakika pamoja na utamaduni wa mambo mpito! Ni Msalaba wa wanandoa na familia waliogawanyika na kusambaratika kutokana na usaliti katika maisha yao; kwa kusongwa na vishawishi vya Shetani na Ibilisi, kwa mauaji ya kifamilia kutokana na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni Msalaba wa watawa wanaofanya hija yao sehemu mbali mbali za dunia, ili kuubeba Msalaba wa Kristo Yesu ili kuwapelekea walimwengu, lakini kwa bahati mbaya, wanajisikia kukataliwa, kudhihakiwa na kubezwa na watu. Huu ni Msalaba wa watawa waliowekwa wakfu katika safari yao, wamesahau ule upendo wa kwanza. Ni Msalaba wa watoto wa Mungu wanaomwamini na kutaka kuishi kadiri ya Neno lake, lakini wanajikuta wakiwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na familia pamoja na vijana wenzao.

Baba Mtakatifu anaendelea kutafakari Fumbo la Msalaba linalojidhihirisha katika udhaifu wa watoto wa Kanisa, unafiki, usaliti, dhambi pamoja na ahadi mbali mbali ambazo wameshindwa kuzitekeleza katika maisha yao. Huu ni Msalaba wa Kanisa ambalo ni aminifu kwa mchumba wake Yesu na Injili, lakini linapata taabu sana, kuwapelekea upendo watu wa Mungu hata wakati mwingine miongoni mwa Wabatizwa wenyewe! Ni Msalaba wa Kanisa linalojisikia kuvamiwa kutoka ndani na nje ya mipaka yake. Ni Msalaba wa mazingira nyumba ya wote, unaoendelea kuharibiwa mbele ya macho yao kutokana na ubinafsi, chuki, uhasama, uchu wa mali na madaraka.

Mwishoni mwa Sala ya Fumbo la Msalaba, Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Kristo Yesu, aweze kupyaisha matumaini kwa njia ya Fumbo la Ufufuko na kuonesha hatima ya ushindi wake dhidi  ya ubaya pamoja na aina mbali mbali za vifo! Katika maandamano ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Baba Mtakatifu Francisko alisaidiwa kubeba Msalaba na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, wanafamilia, mapadre kutoka Mashariki ya Kati watawa, wagonjwa, waamini walei pamoja na vijana.

Papa: Fumbo la Msalaba
20 April 2019, 08:13