Vatican News
Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma kuu: Alhamis Kuu: Ekaristi, Daraja & Huduma; Ijumaa kuu: Mateso & Kifo; Jumamosi kuu: Mkesha: Sifa kuu ya Mshumaa wa Pasaka! Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma kuu: Alhamis Kuu: Ekaristi, Daraja & Huduma; Ijumaa kuu: Mateso & Kifo; Jumamosi kuu: Mkesha: Sifa kuu ya Mshumaa wa Pasaka!  (Vatican Media)

Juma kuu 2019: Matukio makuu ya Imani ya Kanisa Katoliki

Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Jumapili ya Matawi, tarehe 14 Aprili 2019, Kanisa limeadhimisha Siku ya 34 ya Vijana kwa ngazi ya Kijimbo mwaliko kwa vijana kusoma Wosia wa "Christus vivit"!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

JUMAPILI YA MATAWI: Baba Mtakatifu Francisko ameanza maadhimisho ya Juma Kuu kwa kuadhimisha Jumapili ya Matawi, 14 Aprili 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Jumapili ya Matawi, Kanisa limeadhimisha Siku ya 34 ya Vijana kwa ngazi ya Kijimbo. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha ukimya; kusali na kutafakari Neno la Mungu sanjari na kujinyenyekesha ili kushinda kishawishi ya kutaka kujikuza na kujitafuta mambo ambayo ni kazi ya Shetani, Ibilisi, hatari sana kwa maisha ya kiroho. Lengo ni kufikia wokovu katika Ufalme wa Mungu! Anawataka vijana: kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya utakatifu wa maisha pamoja na kujiaminisha kwake, kama njia ya kuelekea kwenye Ufalme wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” anawakumbusha vijana kwamba, katika Maandiko Matakatifu kuna vijana ambao wamejipambanua na kuwa kweli ni mfamo bora wa kuigwa tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya. Baba Mtakatifu anasema,  Kristo Yesu ni kijana milele; vijana ni leo ya Mungu wanayopaswa kuichangia na kuiboresha kwa kujikitaka katika matendo mema. Mbiu kuu kwa vijana ni kwamba, Mungu ni upendo unaoganga na kuponya; unaosamehe na kupatanisha. Vijana wanapaswa kukua na kukomaa kwa kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji. 

Baba Mtakatifu anawataka vijana kukita mizizi katika mambo msingi na kamwe wasikubali wajanja wachache kupoka furaha na matumaini ya ujana wao. Vijana ni wadau wa maisha yao, wanaitwa na kutumwa kwa ajili ya huduma ya kimisionari na katika miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Lakini wakumbuke kwamba, wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka vijana wajisadake bila kujibakiza pamoja na kutambua miito yao!

ALHAMIS KUU: Mama Kanisa anakumbuka Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi. Hii ni Sakramenti ya sadaka: Shukrani, sifa na utukufu kwa Baba wa milele; Ni Kumbukumbu ya mateso yaletayo wokovu na kwamba, hii ni sadaka ya uwepo wa Kristo kwa Neno na Roho wake Mtakatifu. Mama Kanisa anakumbuka pia Siku ya Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa kuwateuwa baadhi ya waamini na kuwaweka wakfu kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hawa ni Makuhani waoliopewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, katika Nafsi ya Kristo ambaye ni kichwa cha Kanisa lake! Hii ni Siku ambayo Kristo alikazia huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu, kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, tarehe 18 Aprili 2019, Saa 3:30 asubuhi kwa Saa za Ulaya, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kubariki mafuta ya Krisma ya Wokovu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu atabariki Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kama mapadre na maaskofu. Hii ni siku ambamo wakleri wanarudia tena ahadi za utii kwa Askofu mahalia.

Karamu ya Mwisho: Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu, Alhamisi jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Gereza la Velletri lililoko nje kidogo ya mji wa Roma pamoja na kuwaosha miguu wafungwa kumi na wawili watakaokuwa wameandaliwa! Huduma ya Kanisa kwa wafungwa ni kati ya mambo yanayopewa pia kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake!

IJUMAA KUU, yaani kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Aprili 2019, anatarajiwa kuanzia saa 11:00 jioni majira ya saa za Ulaya kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

NJIA YA MSALABA: Kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Njia ya Msalaba, mwishoni atatoa neno na kuwapatia waamini baraka zake za kitume. Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2019, imeandaliwa na Sr. Eugenia Bonet wa Shirika la Consolata ambaye pia ni Rais wa Chama cha Kiraia “Slaves No More”.

Kiini cha tafakari hii ni mateso, nyanyaso na dhuluma zinazojitokeza katika biashara ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watu milioni 45 ambao wametumbukizwa katika biashara hii inayozalisha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 32 kwa mwaka na hivyo kuchuana kwa karibu sana na biashara haramu ya silaha na dawa za kulevya duniani. Wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio walengwa wakuu katika biashara hii na wengi wao ni wale wanaotoka katika nchi za Amerika ya Kusini, Afrika na nchi za Ulaya Mashariki ambazo kwa miaka mingi zilikuwa chini ya utawala wa Kikomunisti. Biashara hii inapaswa kupigwa vita tangu kule wanakotoka waathirika hawa, nchi wanakopitia na hatimaye, nchi wanakopelekwa kutumikishwa.

JUMAMOSI KUU: KESHA LA PASAKA, tarehe 20 Aprili 2019,  majira ya saa 2:30 Usiku kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza “Kesha la Pasaka” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Atabariki moto wa Pasaka na kuongoza maandamano kuingia Kanisani na baadaye itaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu.

JUMAPILI YA PASAKA YA BWANA, tarehe 21 Aprili 2019 saa 4:00 Asubuhi majira ya saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye atatoa baraka zake za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “ Urbi et Oribi”. Vatican News itaendelea kushirikiana nawe ili kukujuza yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa. Ukiwa na haraka zako, “tinga” kwenye mtandao wetu na ujitahidi pia kuwashirikisha jirani zako matendo makuu ya Mungu yanayoendelea kufunuliwa kwa watu wa nyakati hizi!

Juma kuu 2019
15 April 2019, 09:05