Vatican News
Papa Francisko: Kanisa kuu la Notre dame: Utambulisho, Ushuhuda wa imani, historia na kito cha thamani! Mahali pa sala na watu kukutana katika umoja na tofauti zao! Papa Francisko: Kanisa kuu la Notre dame: Utambulisho, Ushuhuda wa imani, historia na kito cha thamani! Mahali pa sala na watu kukutana katika umoja na tofauti zao!  (AFP or licensors)

Janga la Moto Kanisa kuu la Notre Dame: Kito na Utambulisho!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, moto umetikisa alama na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao. Kanisa kuu la Notre Dame, ni kito cha thamani, mahali pa watu kukutana katika matukio mbali mbali. Kanisa hili limekuwa ni ushuhuda wa imani na mahali pa sala kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris Ufaransa anasema, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu anasikitika sana kuungua kwa Kanisa kuu la Notre Dame, kielelezo na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa katika umoja na utofauti wao! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, baada ya ukarabati, Kanisa kuu la Notre Dame litaendelea kuwa nyumba ya wote, alama ya imani, amana na utajiri wa kihistoria na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni utajiri wa familia ya Mungu nchini Ufaransa, lakini pia ni kwa ajili ya binadamu wote!

Baba Mtakatifu anapenda kuungana na familia ya Mungu nchini Ufaransa katika kipindi hiki kigumu, ili kuwatia shime na faraja! Maadhimisho ya Juma kuu, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Janga hili la moto limesababisha uharibifu mkubwa katika Kanisa hili la kihistoria! Moto umetikisa alama na utambulisho wa wananchi wa Ufaransa unaofumbatwa katika umoja na tofauti zao. Kanisa kuu la Notre Dame, ni kito cha thamani, mahali pa watu kukutana katika matukio mbali mbali. Kanisa hili limekuwa ni ushuhuda wa imani na mahali pa sala kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Paris, Ufaransa.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja na familia ya Mungu nchini Ufaransa kwa njia ya sala katika kipindi hiki kigumu baada ya Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kuteketea kwa moto mkali, Jumatatu, tarehe 15 Aprili 2019. Maafa haya makubwa yawe ni chanzo cha matumaini ya ujenzi wa Kanisa kuu la Notre Dame! Baba Mtakatifu, amepokea kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa za kuungua kwa Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Hili ni Kanisa ambalo limekuwa ni alama na kielelezo cha Ukristo na wananchi wa Ufaransa katika ujumla wao. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala na sadaka yake, wale wote waliojisadaka kuzima moto na kuokoa baadhi ya mali zilizokuwepo ndani ya Kanisa hili.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa limesikitishwa sana na maafa yaliyotokea kwenye Kanisa kuu la Notre Dame, kiasi cha kuacha kilio na simanzi kubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia! Maaskofu Katoliki Ufaransa wanapenda kuchukua nafasi hii, kumhakikishia Askofu mkuu Michel Aupetit, uwepo wao wa karibu katika kipindi hiki kigumu cha historia, maisha na utume wa Jimbo kuu la Paris. Maaskofu wanatambua fika kwamba, umaarufu, amana na utajiri wa Kanisa kuu la Notre Dame unavuka mipaka ya Jimbo na nchi ya Ufaransa katika ujumla wake. Ni Kanisa ambalo limekuwa ni kielelezo cha imani ya Kanisa Katoliki, mahali ambapo waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema zaidi ya milioni 13 kila mwaka hupata nafasi ya kutembelea na kusali ndani ya Kanisa hili.

Limekuwa ni kivutio kikuu cha imani, utalii, utamaduni na historia kwa kukumbuka kwamba, lilijengwa kunako karne ya 13 na iliwachukua muda wa miaka mingi kuweza kulikamilisha na hatimaye, kuanza kutumika kama nyumba ya Ibada. Janga hili la moto limachomoza wakati huu ambapo Kanisa linaingia kwa kishindo katika maadhimisho ya Juma kuu. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linawaalika waaamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mawe hai katika maisha na utume wa Kanisa wakati huu, wanapoadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa wengi! Kanisa la Notre Damu anasema Askofu Eric de Moulins, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwamba, limekuwa ni alama ya imani, uzuri, matumaini na amani; mambo yaliyowaambata watu wote pasi na ubaguzi.

Kuungua na kuteketea sehemu kubwa ya Kanisa hili ni hasara kubwa si tu katika maisha na utume wa Kanisa, bali katika medani mbali mbali za maisha ndani na nje ya Ufaransa. Salam za rambi rambi zimetolewa pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia CEI, linalosikitika kuona historia ya miaka 800 ya Kanisa kuu la Notre Dame, ikiteketea kwa moto. Maaskofu Katoliki Italia, wanaungana kwa sala na familia ya Mungu nchini Ufaransa katika kipindi hiki kigumu cha historia, maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Paris.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana, anasema, wanaungana na familia ya Mungu nchini Ufaransa kusali na kuwaombea kutokana na janga hili ambalo limesababisha hasara kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa pamekuwa ni mahali ambapo watu mbali mbali waliweza kupata nafasi ya kukutana na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Salam za rambi rambi, upendo na mshikamano kutoka kwa viongozi mbali mbali wa serikali zimetumwa kwa Kanisa nchini Ufaransa pamoja na Serikali ya Ufaransa nchini ya Rais Emmanuel Macron ambaye amesikika akisema, kuungua kwa Kanisa kuu la Notre Dame, kuna maanisha pia kuungua kwa sehemu muhimu sana ya maisha ya wananchi wa Ufaransa.

Hii ni alama na utambulisho wa utamaduni na historia ya wananchi wa Ufaransa na Ulaya katika ujumla wake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya pamoja na Rais Donald Trump wa Marekani wametuma ujumbe wa rambi rambi pamoja na mshikamano kwa familia ya Mungu nchini Ufaransa.

Papa: Notre Dame
16 April 2019, 15:13