Cerca

Vatican News
Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018: Wosia wa Kitume: "Christus Vivit" yaani "Kristo anaishi" Umetiwa sahihi na Papa Francisko 25 Machi 2019 na Unazinduliwa tarehe 2 Aprili 2019 Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana 2018: Wosia wa Kitume: "Christus Vivit" yaani "Kristo anaishi" Umetiwa sahihi na Papa Francisko 25 Machi 2019 na Unazinduliwa tarehe 2 Aprili 2019 

Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2018: "Christus vivit"

Wosia huu wa kitume“Christus Vivit” yaani “Kristo anaishi” utazinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019, Mama Kanisa anapokumbuka siku ile Mtakatifu Yohane Paulo II, Muasisi wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani alipoaga dunia, mjini Vatican na kuzikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2005. Huu ni Wosia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa Mama wa Mungu, “Theotokos”, hapo tarehe 25 Machi 2019 ameweka mkwaju kwenye Wosia wa Kitume wa “Vive Crsito, esperanza nuestros”. Na kwa lugha ya Kilatini, Wosia huu utajulikana kama “Christus Vivit” yaani “Kristo anaishi”. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu kusikiliza mpango wa Mungu, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yake. Sehemu ya pili ni kung’amua, ili kushiriki katika mpango wa Mungu, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza. Sehemu ya tatu ni kuamua, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, aliyekubali kuwa ni Mama wa Mungu.

Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018 yaliongozwa na kauli mbiu “Vijana, Manga’amuzi na Miito”. Sinodi ya vijana ilikuwa ni mwendelezo wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, ndiyo maana, Baba Mtakatifu anakazia kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya utume wa familia na utume wa vijana. Kumbe, ni dhamana na jukumu la familia kuwarithisha vijana tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili waweze kuwa kweli ni watakatifu na raia wema, tayari kukuza na kudumisha: umoja, upendo, mshikamano na udugu! Wosia huu wa kitume“Christus Vivit” yaani “Kristo anaishi” utazinduliwa rasmi tarehe 2 Aprili 2019, Mama Kanisa anapokumbuka siku ile Mtakatifu Yohane Paulo II, Muasisi wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani alipoaga dunia, mjini Vatican na kuzikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2005.

Huu ni Wosia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake na wala si kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya peke yao! Mtakatifu Yohane Paulo II anakumbukwa sana na Mama Kanisa kutokana na mchango wake kwa utume wa vijana ndani na nje ya Kanisa. Ilikuwa ni Mwaka 1984 wakati wa kufunga Mwaka wa Ukombozi, Mtakatifu Yohane Paulo II alipowaalika vijana kuja Roma ili kushiriki maadhimisho ya Jubilei ya Vijana na zaidi ya vijana 300, 000 waliitikia wito na mwaliko wake, “wakatinga timu Roma”. Mtakatifu Yohane Paulo II akawaambia vijana, Kanisa linawapenda na kuwathamini sana vijana. Akawakabidhi Msalaba wa Vijana, alama ya Kristo Yesu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa walimwengu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, vijana wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu; furaha na matumaini kwa wale waliokata tamaa kutokana na sababu mbali mbali! Msalaba ni kielelezo cha upendo, huruma na hekima ya Mungu kwa mwanadamu. Ni alama ya ushindi na matumaini, umoja na mshikamano wa dhati kabisa. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anajiunga na wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; watu ambao hawana tena nguvu ya kupiga kelele; hasa watu wasiokuwa na hatia wala ulinzi madhubuti; familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao katika maisha; wanaowalilia watoto wao waliotumbukia katika utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu!  

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Yesu anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi. Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na ubainfsi, rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani ulioneshwa na viongozi wa Kanisa. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele!

Fumbo la Msalaba ni kielelezo makini cha upendo ambao unapenya katika mapungufu na dhambi za mwanadamu kiasi cha kumkirimia msamaha; upendo unaopenya katika taabu na mahangaiko ya binadamu kiasi cha kumjalia nguvu ya kuweza kuyabeba na kuyavumilia; upendo umegusa hata mauti, na kuyashinda na hatimaye kumkirimia mwanadamu maisha na furaha ya uzima wa milele.  Yesu anawajalia wafuasi wake matumaini na maisha tele! Amegeuza ile kashfa ya Msalaba ulioonekana kuwa ni chombo cha: kutisha, chuki na uhasama, anguko na kifo, kuwa ni alama ya ushindi na maisha. Hakuna Msalaba mdogo wala mkubwa katika maisha, bali ni uwepo endelevu wa Kristo anayetaka kushiriki na kuwamegea wafuasi wake maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu anasema, Msalaba ni mwaliko wa Kristo kwa wafuasi wake ili waweze kuguswa na upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba.

Hii ni changamoto ya kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo; hasa zaidi kwa wale wanaoteseka; watu wanaohitaji msaada; ni jukumu la kila mwamini kujitoa katika ubinafsi wake ili kuwaendelea na kuwanyooshea mikono tayari kuwasaidia wengine. Ni matumaini ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwamba, vijana wataendelea kuwa vyombo na mashuhuda wa Injili kati ya vijana wenzao. Tangu mwaka 1986 Siku ya Kwanza ya Vijana Kimataifa iliadhimishwa mjini Roma na kwa mwaka 2019 maadhimisho haya yamefanyika nchini Panama kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko!

Christus Vivit
26 March 2019, 10:16