Tafuta

Wosia wa Kitume "Vive Cristo, esperanza nuestra" yaani "Muishi Kristo, Tumaini letu": Chimbo lake na asili yake ni katika matamanio ya Mama Kanisa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana! Wosia wa Kitume "Vive Cristo, esperanza nuestra" yaani "Muishi Kristo, Tumaini letu": Chimbo lake na asili yake ni katika matamanio ya Mama Kanisa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana! 

Wosia wa Kitume: Sinodi ya Vijana 2019: chimbuko na asili yake!

Wosia wa Kitume, "Vive Cristo, esperanza nuestra" yaani "Muishi Kristo, Tumaini letu" unapata chimbuko na asili yake katika matamanio ya Mama Kanisa kuboresha maisha na utume wake miongoni mwa vijana kwa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa! Vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, tarehe 25 Machi 2019 ametiamkwaju kwenye Wosia wa Kitume baada ya Sinodi ya Maaskofu unaoongozwa na kauli mbiu “Vive Cristo, esperanza nuestra” yaani “Muishi Kristo, Tumaini letu” ambao kwa mara ya kwanza umeandikwa kwa lugha ya Kihispania. Wosia huu ni safari ndefu iliyoanza kunako mwaka 2017 Baba Mtakatifu alipowaandikia vijana barua, kukafuatia semina ya kimataifa kuhusu hali ya vijana duniani; Mwezi Machi 2018 vijana waakaadhimisha utangulizi wa Sinodi uliohitimishwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Kijimbo.

Mwezi Juni, 2018 kukachapishwa hati ya kutendea kazi na Mwezi Oktoba, 2018 maadhimisho na hatimaye, Mababa wa Sinodi wakatoa hati baada ya Sinodi. Januari, 2019, Kanisa likaadhimisha Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani na tarehe 25 Machi 2019, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Vive Cristo, esperanza nuestra” yaani “Muishi Kristo, Tumaini letu” ukatiwa mkwaju rasmi! Kwa ufupi, huu ndio utajiri unaofumbatwa katika Wosia wa Kitume uliotiwa mkwaju na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Machi 2019, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Kupashwa Habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu! Wosia huu umeandikwa kwa mtindo wa barua inayoelekezwa kwa vijana, kuwakumbusha kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wao ni kito cha thamani sana katika maisha na utume wa Kanisa, ndiyo maana Baba Mtakatifu akaitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana iliyoongozwana kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito!

BARUA YA BABA MTAKATIFU FRANCISKO KWA VIJANA 2017

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujihusisha kikamilifu katika maandalizi ya Sinodi hii kama sehemu ya mchakato unaowapatia nafasi ya kutafakari wito wao kama ilivyokuwa kwa Mzee Abramu, Baba wa imani aliyeamriwa na Mwenyezi Mungu kutoka katika nchi yake, jamaa na nyumba ya baba yake aende katika nchi atakayomwonesha! Vijana wanahamasishwa kutoka ili kujiandaa kwa ajili ya maisha wasiyoyafahamu bado, lakini kwa kujenga mahusiano salama kwani Mwenyezi Mungu ndiye anayewasindikiza. Huu ni mwaliko wa kusikiliza sauti ya Mungu inayosikika nyoyoni mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu.Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu alipomwambia Abramu “Ondoka” hakumtaka kukimbia ulimwengu, bali huu ulikuwa ni mwaliko wa wito wa kuacha yote na kwenda mahali ambapo Mwenyezi Mungu angemwonesha! Na kwa vijana mahali hapa ni Jamii inayosimikwa katika haki na udugu, jambo ambalo vijana wengi wanalitamani kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Lakini, kwa bahati mbaya neno “Ondoka” linapata maana mpya katika ulimwengu mamboleo ni kuondokana na tabia ya kutenda mabaya, ni kutoka katika hali ya ukosefu wa haki na zaidi ya hayo ni kutoka katika vita!

Kuna umati mkubwa wa vijana unaojikuta ukiogelea katika “mtutu wa bunduki” na wengi wao wanalazimika kuzikimbia kutoka katika nchi walikozaliwa! Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kilio chao kinasikika hadi mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli. Huu ni mwaliko wa kumwendea Yesu na kuona mahali anapoishi ili kuweza kushinda pamoja naye kama walivyofanya wale Mitume wa Yesu. Mwaliko huu bado unaendelea kusikika masikioni mwa vijana wengi ili hatimaye, kuweza kushiriki katika furaha ya kweli. Jambo hili linawezekana kwa kuanza hija ya mang’amuzi ili kutambua mpango wa Mungu katika maisha yao! Hii ni safari yenye milima na mabonde, kuna kusimama na kuanguka chali kama mende! Lakini Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, atawanyooshea mkono na kuwainua tena! Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini Poland aliwauliza ikiwa kama mambo yanaweza kubadilika na wao kwa jeuri wakamjibu wakisema “Ndiyo”. Kilio hiki kinapata chimbuko lake kutokana na ukosefu wa haki na kamwe hakiwezi kushikishwa adabu na utandawazi pamoja na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kusikiliza sauti ya Mungu kutoka katika undani wao bila kuogopa kwani yupo pamoja nao ili kuwalinda na kuwategemeza! Ulimwengu bora unajengwa na kudumishwa kutokana na mchango wa vijana wa kizazi kipya wanaoonesha ukarimu kwa kutaka mabadiliko, changamoto ni kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu na dhamiri nyofu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kumfuasa Kristo, Bwana na Mwalimu. Kanisa linataka kuwasikiliza vijana, kuguswa na unyenyekevu, imani; mashaka na “madongo” yao! Baba Mtakatifu anawataka vijana kupaaza sauti zao kwenye Jumuiya kiasi hata cha kuwafikia viongozi wa Kanisa, ili kabla ya kufanya maamuzi muhimu ya maisha, vijana nao wapate nafasi ya kutoa maoni yao, kwani mara nyingi Mwenyezi Mungu anawapatia vijana suluhu bora zaidi. Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuwaambia kwamba, Kanisa linataka kuwa chombo cha furaha ya vijana na anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwashika mkono na kuwaongoza kwenye chemchemi ya furaha timilifu na ukarimu!

SEMINA YA KIMATAIFA KUHUSU HALI YA VIJANA DUNIANI 2017

Kanisa linapenda kuandamana na kushibana na vijana bega kwa bega ili kuwasikiliza kwa makini, kuwafunda kutoka katika undani wao na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Maadhimisho ya Sinodi ya Vijana ilikuwa ni nafasi ya pekee kwa Maaskofu kuwasikiliza vijana kwa makini ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana wa kizazi kipya! Semina ya Kimataifa Kuhusu Hali ya Vijana iliyofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 11-15 Septemba 2017, ilikuwa ni nafasi kwa vijana kuweza kupembua kwa kina na mapana mada mbali mbali zinazohusu maisha yao, ili hatimaye, kuweza kuwachagua vijana watakaowawakilisha katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, Mwezi Oktoba, 2018. Hii ilikuwa ni semina elekezi iliyojadili kuhusu: vijana na utambulisho wao; miradi inayoweza kutekelezwa na vijana; vijana na teknolojia; vijana na maisha ya kiroho. Hata wale “vijana wa zamani” wanaopenda kushiriki walikaribishwa sana.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia sana utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea matumaini ya kuweza kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Vijana kati ya umri wa miaka 16 hadi 29 wakahamasishwa kushirikisha maoni yao kwa njia ya mtandao, ili kwamba, baada ya maoni yao kuchambuliwa, Sekretarieti kuu ya Sinodi iweze kuandaa “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi”. Semina hii ya kimataifa iliwashirikisha wataalam wa utume wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Sekretarieti kuu ya Sinodi ikaendelea kukusanya maoni kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani, Makanisa ya Mashariki pamoja na majibu yaliyotolewa na vijana kwenye mtandao wa Sinodi ya Vijana. Vyama vya kitume kwa ajili ya vijana vilihamasishwa pia kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa utume wa vijana katika parokia zao.

Sinodi iliwashirikisha pia vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ua Kikristo, ili kwa pamoja waweze kuwa na mbinu mkakati wa utambulisho wa vijana. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kutembea na kuandamana na vijana wa kizazi kipya, bega kwa bega; kwa kuwasikiliza kwa makini; ili kuwaandaa vijana hawa kuweza kutekeleza dhamana na utume wao ndani na nje ya Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, vijana wako tayari kusikiliza ushauri wa wahenga, ili waweze kutoka kufua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa!

UTANGULIZI WA MAADHIMISHO YA SINODI YA VIJANA 2018

Vijana waliokuwa wanashiriki Maadhimisho ya Awali ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kuanzia tarehe 19-25 Machi 2018, Jumapili ya Matawi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani katika ngazi ya Kijimbo, wamewasilisha “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” kwa Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wametumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia shime kuzungumza, kusikiliza na kushirikisha mawazo yao. Vijana wanakiri kwamba, kweli wameonja umoja, upendo na mshikamano wa kidugu licha tofauti zao za kidini, kiimani, kitamaduni na kwamba, umekuwa ni mkutano unaolenga ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wengi. Vijana wanasema, Hati ya Utangulizi wa Sinodi” si tu ni muhtasari wa mambo msingi waliyojadili, kwa hakika ni muhtasari wa maisha na matamanio halali yanayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Ni matumaini ya vijana kwamba, Mama Kanisa ataendelea kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana na kwamba, hati hii itakuwa ni mwanga wa majadiliano kwa Mababa wa Sinodi na familia ya Mungu katika ujumla wake katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa katika ujumla wake, kutumainia sala ya vijana! Vijana wanatamani kuona Kanisa likitekeleza dhamana na utume wake katika misingi ya ukweli na uwazi; upole na unyenyekevu, kiasi hata cha kuthubutu kukiri makosa na mapungufu ya watoto wa Kanisa pale yanapojitokeza. Vijana wanatamani kuwa na mashuhuda watakaowasindikiza katika maisha na miito yao, watakaowasaidia kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha vijana kwamba, wazee wana ndoto, lakini vijana wana maono! Vijana wanataka kuona Kanisa linalojikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu, mchakato wa upyaisho, utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini.

HATI YA UTANGULIZI WA SINODI YA VIJANA 2018

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwezi Oktoba, 2018 yataongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na mang’amuzi ya Miito”. Maandalizi haya tayari yameanza kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kutoa Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya XV ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hati hii ni mwaliko wa kumfuasa Yohane, mwanafunzi aliyependwa zaidi na Kristo Yesu. Hati inaangalia hali ya vijana duniani: utambulisho na ushiriki wao; mambo rejea binafsi na taasisi pamoja na mchakato wa kuunda vijana wa kizazi kipya wanaoshikamana zaidi. Sura ya pili inajikita katika imani, mang’amuzi na wito kwa kuzingatia umuhimu wa imani na wito katika maisha ya vijana; zawadi ya kufanya mang’amuzi ya miito ili kutambua, kutafsiri na kuchukua maamuzi ya maisha. Sura ya tatu inapembua kwa kina na mapana shughuli za kichungaji kuhusu miito kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kufanya hija na vijana katika maisha yao, ili hatimaye waweze kutoka, kuona na kuitikia wito wa kumfuasa Kristo Yesu.

Walengwa wakuu ni vijana wote pasi na ubaguzi; Jumuiya inayojihusisha na malezi ya miito pamoja na kuwa na watu ambao ni mfano bora wa kuigwa. Shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito zinatekelezwa katika maisha ya kila siku sanjari na ushiriki mkamilifu katika masuala ya kijamii. Hati inachambua maeneo maalum ya shughuli za kichungaji bila kusahau ulimwengu wa mitandao ya kijamii, ambamo vijana wengi wanapenda kuogelea huko. Lugha, elimu makini na mikakati ya Uinjilishaji; ukimya, tafakari na sala ni mambo ambayo pia yanapewa kipaumbele cha pekee kwenye hati ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018. Mwishoni, Hati hii inamwangalia Bikira Maria aliyehifadhi, akatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake, ili aweze kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha ya miito yao! Kuna maswali dodoso yatakayosaidia kuandaa Hati ya Kutendea Kazi, maarufu kama “Instrumentum Laboris”, kwa kuangalia hali ya kila bara. Namna ya kukusanya takwimu, kuzitafsiri na kuzifanyia kazi.

Katika utangulizi wake, Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 inatoa mwaliko kwa vijana wote ili waweze kupata utimilifu wa furaha ya maisha, kwani Kanisa limekabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili. Huu ni mwaliko wa kuwasaidia vijana ili kupata mang’amuzi kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa kama: watu wa ndoa, watawa na mapadre, ili kwa njia ya mwanga wa imani, wawe tayari kushuhudia utimilifu wa furaha katika miito yao! Kanisa linatambua na kuthamini nguvu ya furaha inayobubujika kutoka kwa vijana ambao kimsingi ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Baada ya hati hii kuchapishwa, sasa Kanisa limeanza rasmi mchakato wa kupata ushauri kutoka ndani na nje ya Kanisa ili hatimaye kuliwezesha Kanisa kupata mawazo makuu yatakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana wanahamasishwa kufuata mfano wa Mtakatifu Yohane na wenzake waliojitaabisha kwenda kumtafuta Yesu, wakamwona, akawakaribisha na kujenga nao uhusiano wa urafiki wa kudumu, mwaliko kwa vijana pia kuwa kweli ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu!

Sura ya kwanza: Hali ya Vijana Duniani! Sura hii inapembua hali ya vijana duniani ili kugusa undani wa maisha ya vijana kimaadili na kiroho, tayari kufanya mang’amuzi ya maisha na wito wao. Kuna hali ya kutojaliana, idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa; tamaduni na mapokeo ya imani ya Kanisa toka nchi moja hadi nchi nyingine. Bado kuna ubaguzi kati ya watoto wa kike na wavulana. Vijana wanaojadiliwa ni wale wenye umri kati ya miaka 16- 29 lakini pia umri huu unategemea na mahali walipo vijana. Dunia inabadilika kwa kasi kubwa jambo ambalo linahitaji kuwa na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa muda mrefu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa za ajira; kuna athari za mabadiliko ya tabianchi; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji lakini pia wapo vijana wachache wanaofaidika na ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Pamoja na maendeleo yote haya lakini kuna vijana wengi bado wanajikuta wakiwa wametumbukia katika upweke hasi na hali ya kukata tamaa kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya mahitaji ya watu wachache na kwamba, kuna uharibifu mkubwa wa mazingira hali inayotishia usalama na maisha ya kizazi kijacho!

Vijana wa kizazi kipya wana mwelekeo mpya, matamanio na jinsi ya kujenga mahusiano yao na wengine mambo ambayo yanaathari zake katika mchakato wa mafungamano ya kijamii na utambulisho wa vijana wa kizazi kipya. Kuna mwingiliano mkubwa wa tamaduni za watu kutokana na sababu mbali mbali kama vile changamoto ya wahamiaji, wakimbizi pamoja na elimu. Vijana wanakumbana na hali ngumu ya maisha, ujinga, umaskini, magonjwa na hali ya kubaguliwa. Baadhi yao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi; ni wahanga wa utumwa mamboleo; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, kuna baadhi yao wanatumbukizwa katika uhalifu wa magenge na ujambazi.

Kimsingi vijana wengi wanataka kuwa wadau wakuu katika mchakato wa mageuzi ya kijamii, lakini kwa bahati mbaya wanakosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha kutokana na kukosa elimu, ajira, ujuzi au maarifa; hali ambayo inawapelekea vijana wengi kukosa imani na matumaini katika maisha yao. Vijana wanataka kuona mifano ya watu na taasisi ambazo zitakuwa ni mfano bora wa kuigwa katika hija ya maisha yao. Hawa wanaweza kuwa ni wazazi, walezi na taasisi ambazo iko karibu sana na watu. Kutokana na mwelekeo huu, vijana wengi wanajikuta wanashindwa kushiriki katika maisha ya kiimani! Ni vijana wanaojifunza kuishi bila ya uwepo wa Mungu, Injili na Kanisa kwa kujidanganya kwamba, wanaweza kujiokoa wao wenyewe na matokeo yake ni kutumbukia katika ubinafsi! Vijana wa kizazi kipya wanaunganishwa kwa kiasi kikubwa na mitandao ya kijamii ambayo ina faida na hasara zake kwani kuna kiasi kikubwa cha mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema.

Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga utamaduni unaokidhi maisha na wito wa vijana. Vijana wanapaswa kufanya maamuzi magumu na machungu katika maisha yao kwa kujikita katika ujasiri na kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Vijana wakati mwingine wanashindwa kufanya maamuzi magumu kutokana na ukosefu wa fursa za ajira, hali mbaya ya kiuchumi na ukosefu wa ujuzi; hali mbaya ya maisha ya familia pamoja na tabia ya vijana wengi kutengwa kutokana na sababu mbali mbali: za kiuchumi, kijamii na kidini. Hata hivyo, vijana wengi wanaweza kupata fursa ya maisha bora zaidi kwa kuwa na sera na mikakati mipya ya maendeleo.

Sura ya pili: Imani, Mang’amuzi na Miito! Mama Kanisa katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anataka kukutana, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana pasi na ubaguzi ili kweli vijana waweze kupata utimilifu wa maisha kwa kutambua kwamba maisha na imani ni zawadi ya Mungu. Ili kuwahudumia vyema vijana anasema Baba Mtakatifu Francisko kunahitajika: wema, upole na majitoleo ya dhati kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu, mtu mwenye haki, jasiri na mchapakazi; aliyeonesha huruma na upendo. Kuna uhusiano wa pekee kati ya imani na wito, kwani hapa vijana wanajisikia kupendwa na kuthaminiwa. Imani inawasaidia vijana kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati, tayari kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, matokeo ya majadiliano ya kina katika dhamiri nyofu! Wito na mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, umesheheni furaha na majitoleo ya dhati ambayo yanapaswa kutakaswa, kuwekwa huru ili kutambua jambo jema na kulitenda. Vijana wanapaswa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kusoma alama za nyakati na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika historia; kwa kung’amua kilicho chema na kukifuata, ili kupata utimilifu wa maisha. Mkazo ni kutambua, kutafsiri na kuchagua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka katika maisha ya kijana!

Mchakato wa mang’amuzi ya wito ni hija ndefu katika maisha yenye milima na mabonde kama ilivyokuwa kwa Abramu, Baba wa imani. Wito daima unaambatana na utume unaopaswa kupokelewa kwa uchaji, ari na moyo mkuu, tayari kujisadaka na kuchukua Msalaba wako, ili kumfuasa Kristo Yesu. Hapa kuna haja ya kuondokana na ubinafsi tayari kuambata tunu msingi za Kiinjili kuelekea ukomavu katika wito. Katika mchakato wa kuwasindikiza vijana katika mang’amuzi ya wito wao. Ikumbukwe kwamba vijana hawa wanapaswa kutenda kadiri ya mwanga wa imani kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani mwao; kwa kusikiliza kwa makini wanaweza kung’amua wito wao, lakini wakumbuke kwamba, dhambi daima itaendelea kumwandama mwanadamu, kumbe, hapa kijana anapaswa kufanya maamuzi magumu katika maisha yake. Vijana wajenge utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu kwa makini; wajenge mahusiano ya dhati na Kristo Yesu kwa kuimarisha na kudumisha maisha ya kiroho: kwa njia ya Tafakari ya Neno, Ibada ya Kuabudu, Matendo ya huruma na ushuhuda makini wa tunu msingi za maisha ya Kikristo pasi na woga. Vijana wanapaswa kusindikizwa kwa njia ya sala na kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu anayeangaza na kuwaongoza waja wake.

Sura ya Tatu: Mikakati ya shughuli za kichungaji: Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana inapaswa kujielekeza mahali waliko vijana katika maisha yao ya kila siku, ili kuwasaidia kujenga historia ya maisha yao. Yesu apewe nafasi ya kuweza kutembea na vijana hatua kwa hatua ili aweze kusimama na kuwaangalia kwa jicho lenye huruma na upendo, ili kwa kufunga safari na vijana, Jumuiya nzima ya waamini iweze kujengwa na kuimarishwa. Vijana wapewe nafasi ya kuonesha na kushirikisha kipaji chao cha ugunduzi; kwa kuwa na mwono na mwelekeo mpya na mpana zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa, Mama Kanisa anakazia mambo makuu matatu: kutoka, kuona na kuitwa! Utume kwa vijana ni mchakato unaopaswa kuwashirikisha vijana wote pasi na ubaguzi kwa kutambua kwamba, Jumuiya ya waamini nayo inawajibika barabara katika malezi, makuzi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana kwa kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa linawataka wazazi, walezi na familia; viongozi wa Kanisa pamoja na walimu kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana inapaswa kujikita katika uhalisia wa maisha ya vijana na utekelezaji wa majukumu yao katika jamii. Vijana wanapaswa kujifunza kutumia vyema rasilimali muda, fedha, mali na mahusiano binafsi na ya kijamii. Vijana wawe na vipaumbele katika maisha, ili hatimaye kuwa na mwelekeo wa kuweza kufanya maamuzi magumu na machungu katika maisha. Imani ya kweli ni nyenzo msingi inayoweza kumsaidia kijana kufanya maamuzi mazito katika maisha yake hasa pale anapokabiliana na kinzani na magumu ya maisha. Hapa kuna haja ya kujenga mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini, tayari kushiriki katika mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Sera na mikakati shughuli za kichungaji itaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani na katika maadhimisho yanayofanywa katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Parokia ni mahali muafaka pa shughuli za kichungaji kwa vijana wakati wa maandalizi ya kupokea Sakramenti za Kanisa; kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa mahalia pamoja na vituo vya michezo vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa. Vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na shule ni sehemu muafaka pa kumwilisha utume wa vijana sanjari na ushiriki wa vijana katika shughuli mbali mbali za kijamii; vyama vya kitume! Seminari na nyumba za malezi ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha mang’amuzi ya miito ndani ya Kanisa bila kusahau pia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, mahali ambako vijana wengi wanapenda kuogelea huko kwa raha zao wenyewe!

Vyombo vya umwilishaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji vinapaswa kuzingatia lugha katika mazingira ya Kibiblia, Kiliturujia, Kisanaa, Katekesi na njia za mawasiliano ya jamii, kwa kugundua na kuthamini mchango wa vijana. Kuna haja ya kusaidiwa kukua na kukomaa katika uhuru kamili kwa kuzingatia elimu makini. Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika haki, huduma, upendo, umoja na mshikamano ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya vijana. Jumuiya ya wakristo inahamasishwa kuwasikiliza na kuwakumbatia wale wote wanaotaka kuonana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao. Vijana wanaweza kufanya mang’amuzi ya miito yao kwa kujenga na kudumisha utamaduni ukimya, tafakari ya kina na sala ili kujenga urafiki aminifu na dumifu na Kristo Yesu. Kanisa linapenda kuuweka mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyehifadhi, akatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake, ili kila kijana aweze kujifunza kutoka kwa Bikira Maria mtindo wa kusikiliza, ujasiri wa imani, mang’amuzi ya maisha na sadaka katika huduma, daima wakijitahidi kujiaminisha mbele ya Mungu.

Mwishoni, Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018 inatoa maswali dodoso ya jinsi ya kukusanya takwimu; kusoma na kutafasiri takwimu za vijana wanaohudhuria maeneo ya Kanisa, wale ambao wako nje au wale wanaojisikia kuwa ni wageni kabisa katika maeneo ya Kanisa. Maswali ya utume kwa vijana kuhusu miito; walezi na waalimu na mwishoni maswali msingi kwa kila bara pamoja na kushirikisha wengine takwimu zilizopatikana yamekaziwa kwa wote! Katika kipindi cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, 2018, Kanisa limejenga na kuimarisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya, tayari kujibu matamanio yao halali, yatakayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamejitahidi kutembea kwa pamoja huku wakisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu aliyeendelea kuwashangaza kwa karama na mapaji mbali mbali pamoja na nguvu ya kuwapatia walimwengu matumaini!

HATI YA MABABA WA SINODI KWA AJILI YA VIJANA 2018

Mababa wa Sinodi wamesafiri pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakafanya kazi kwa umoja, huku wakizingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha kujisikia kuwa ni fumbo la mwili mmoja, unaoteseka na kufurahia, ili kwa njia ya neema ya Mungu, Kanisa liweze kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Vijana wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Kanisa limeonekana kuwa ni jukwaa la majadiliano na shuhuda wa udugu. Hali hii ni sehemu ya mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Kumekuwepo na utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi, maswali na majibu dodoso kutoka kwa vijana kwa njia ya mitandao ya kijamii, hati ya kutendea kazi na sasa Mababa wa Sinodi wametoa Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Mapendekezo yote yamepigiwa kura na hatimaye kupitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kukabidhiwa naye ameamuru kwamba, hati hii ichapwe, ili iweze kuwa ni dira na mwongozo wa Kanisa kwa sasa na kwa miaka ijayo! Huu ni muhtasari wa kile ambacho Mababa wa Sinodi wamekitambua, wakakitafsiri na kuamua kukichagua kwa mwanga wa Neno la Mungu. Haya ni matunda ya tofauti msingi zinazofumbatwa katika umoja unaokamilishana, baada ya kujadiliana na kusikilizana kwa muda wa miaka miwili.

Hati hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo  zimejikita katika mawazo ya Injili yanayowaonesha wale wafuasi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu; Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua; Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka. Hii ndiyo changamoto ambayo Mababa wa Sinodi wanayataka Makanisa mahalia kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, daima yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa na vijana, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

SEHEMU YA KWANZAYesu alikua akiandamana nao! Hapa Mababa wa Sinodi wanapenda kujikita kwa kupembua umuhimu wa Kanisa linalosikiliza kwa makini; mchango wa Sinodi tatu zilizotangulia; utambulisho na umuhimu wa mahusiano na manfungamano na vijana wa kizazi kipya! Hati inapembua kwa kina na mapana hali na mazingira ya maisha ya vijana, nguvu, udhaifu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao. Kanisa linataka kuwasikiliza kwa makini, katika hali ya unyenyekevu, uvumilivu na uwajibikaji, unaolisukuma kufanya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi pamoja na vijana, ili kujibu kilio na matamanio yao halali pasi na haraka ya kuwa na majibu yaliyotengenezwa kwenye maabara. Kwa hakika, vijana wanataka kusikilizwa, kutambuliwa, kuthaminiwa na hatimaye, kusindikizwa na wanataka sauti yao iweze kusikika na kufanyiwa kazi katika jamii na ndani ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, si nyakati zote, Kanisa limekuwa na mwelekeo kama huu, kwani wakleri na watawa wameonekana kuwa na mambo mengi kiasi cha kukosa muda wa huduma ya kuwasikiliza vijana. Umefika wakati wa kuwaandaa hata waamini walei watakaojisadaka kwa ajili ya kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya. Maendeleo ya sayanasi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yanaendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa vijana kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao na tasaufi, mambo ambayo yanaweza kutumiwa na Kanisa kama chachu ya kufufua imani miongoni mwa vijana! Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu pamoja na vituo vya michezo ni mahali muafaka pa malezi na makuzi endelevu na fungamani; ni mahali pa shuhuda za kiinjili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna mwingiliano wa pekee kati ya familia, kazi, ulinzi wa uhai pamoja na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.

Taasisi za elimu na michezo zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, ziwe ni mahali pa kujenga misingi ya imani, kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; ni mahali pa kukabiliana na changamoto za kisayansi na kiteknolijia kwa mwanga wa Injili na kwamba, mabadiliko ya kijamii yanapaswa kuratibiwa na haki jamii. Kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa kuhusu utume wa Parokia, ili kujenga ari na mwelekeo mpya wa kimisionari kwa kujikita katika katekesi ya awali na endelevu. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto katika ulimwengu mamboleo na wala si suala mtambuka! Kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi watoto wasioandamana na wazazi wala walezi wao! Hawa ni wale wanaokimbia: vita, nyanyaso na dhuluma; maafa asilia na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini na matokeo yake, wanaishia kutumbukia katika mikono dhalimu ya wafanyabiashara haramu ya binadamu; utumwa mamboleo; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na nyanyaso za kisaikolojia na kimwili.

Kanisa linaguswa sana na mahangaiko ya watu hawa, linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki zao msingi; kwa kuwapokea, kuwahifadhi, kuwalinda na kuwashirikisha, pale inapowezekana, waunganishwe na familia zao asilia. Wakimbizi na wahamiaji ni hazina na utajiri mkubwa katika maisha ya kiroho na kiutu kwa jamii inayowapatia hifadhi, kwani kwa njia ya ukarimu wanaweza pia kutajirishana. Mambo makuu ya kuzingatia ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha kama sehemu ya utamaduni unaofyekelea mbali maamuzi mbele, woga, uchoyo na ubinafsi! Maaskofu wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, haki ya watu kubaki nchini mwao inalindwa. Dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo zimegusiwa pia katika hati hii, mambo yanayopelekea uhamiaji wa nguvu na shuruti!

Dhamana na wajibu wa kupambana na: kashfa za nyanyaso; ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka, kwa kujizatiti katika ukweli na uwazi; kwa kuomba msamaha na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka. Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia inatekelezwa ili kashfa hizi zisijirudie tena ndani ya Kanisa, kwa kuzingatia uteuzi, malezi na majiundo ya majandokasisi pamoja na walezi wanaopewa dhamana na Mama Kanisa katika utume huu. Mababa wa Sinodi wanawapongeza wale wote waliokuwa na ujasiri wa kusema ukweli kuhusu nyanyaso walizotendewa, hali ambayo imelisaidia Kanisa kuamua na kutenda kwa ujasiri, kwa kuzingatia huruma na haki. Lakini, ikumbukwe kwamba, kuna umati mkubwa wa wakleri na watawa wanaojisadaka bila ya kujibakiza katika kuwahudumia watu wa Mungu, katika: ukweli na uaminifu na  kwamba, hawa wanaweza kuwa ni chachu ya mageuzi na upyaisho wa Kanisa katika mwelekeo huu.

Mababa wa Sinodi wanasema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali rejea pa vijana na jumuiya ya kwanza ya imani, changamoto na mwaliko kwa wazazi, walezi na wazee kusaidia mchakato wa elimu ya dini na urithishaji wa imani sanjari na kuendeleza dhamana na wajibu wa wanaume katika maisha na utume wa familia, dhana ambayo kwa sasa inakumbana na changamoto nyingi, kutokana na ukweli kwamba, malezi na makuzi ya watoto wengi yanatekelezwa na wanawake kutokana na familia kuwa tenge kwa sababu mbali mbali. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya kurithisha imani kwa vijana wenzao! Hati ya Sinodi ya Maaskofu imejadili kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa Kanisa na Jamii kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Ukosefu wa fursa za ajira, umaskini; dhuluma na nyanyaso; kutengwa na jamii kutokana na sababu mbali mbali; ubaguzi na ukabila; mambo yanayohitaji wongofu na mshikamano! Vijana waendelee kujisadaka kwa kujitolea, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kujihusisha kikamilifu katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, ili kusimama kidete: kulinda: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kudumisha haki jamii, changamoto ambayo vijana wanataka kuona Kanisa inalivalia njuga pasi na mzaha!

Mababa wa Sinodi wanasema, sanaa, muziki na michezo ni rasilimali kubwa katika sera, mikakati na shughuli za kichungaji kwa vijana, kwani zinasaidia katika mchakato wa: elimu, malezi na mafungamano ya kijamii. Muziki unaweza kusaidia pia katika maboresho ya liturujia ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kutakatifuzwa. Vijana wanataka kushirikishwa katika liturujia hai inayofumbatwa katika ukweli, furaha, ibada na uchaji wa Mungu, ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jumuiya ya waamini. Alama za liturujia, mahubiri yaliyoandaliwa vyema na ushiriki wa waamini ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Vijana wasaidiwe kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuthamini Liturujia ya Kanisa kwani hii ni kazi ya Kristo na Kanisa. Vijana wapewe nafasi ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; wawajibike pamoja na kushirikisha vipaji na karama zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa kujenga utamaduni wa: kusikiliza na kujadiliana na vijana.

SEHEMU YA PILI: Yakafunguliwa macho yao nao wakamtambua. Mababa wa Sinodi wanakazia kuhusu Pentekoste mpya, zawadi ya ujana, fumbo la wito, utume wa kuwasindikiza vijana na sanaa ya kung’amua! Mwenyezi Mungu anazungumza na Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, kwa njia ya vijana, “majukwaa ya taalimungu”, mahali ambapo Kristo Yesu anapenda kujifunua kwa waja wake. Kutokana na sababu mbali mbali, vijana wa kizazi kipya wanaweza kuwa wamecharuka katika medani mbali mbali za maisha, kumbe, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwapokea, kuwaheshimu, kuwathamini na kuwasindikiza kama sehemu ya mchakato wa kulipyaisha Kanisa ambalo wakati mwingine, limekuwa likijikongoja. Mababa wa Sinodi wanamwona Kristo Yesu kuwa ni mfano kati pamoja na vijana, wanaosindikizwa pia kwa mifano na ushuhuda wa watakatifu ambao wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa katika ushuhuda wa kinabii unaoleta mageuzi katika maisha ya waamini!

Utume na wito miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni mwaliko kwa vijana kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kushirikisha furaha ya Injili katika ukweli na udumifu, huku Kristo Yesu akiwakirimia uhuru zaidi unaofumbatwa katika ukweli na upendo. Maisha ni wito unaojenga na kukuza mahusiano na Mwenyezi Mungu. Wito wa ubatizo ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Kila mwamini anapaswa kuishi vyema wito wake kadiri ya mazingira yake: kitaaluma, kifamilia, maisha ya kuwekwa wakfu, daraja takatifu na ushemasi wa kudumu ambao ni rasilimali inayopaswa kuendelezwa katika utimilifu wake! Kuwasindikiza vijana: familia pamoja na wadau mbali mbali wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao ili kuwasindikiza vijana kuweza kufanya maamuzi magumu katika maisha. Lakini, wazazi, walezi na viongozi wa maisha ya kiroho wanahitaji “kupigwa msasa” katika malezi, kwa kuwa na nyenzo na vigezo muhimu vinavyowaongoza vijana katika maisha yao. Hawa ni vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya maisha na wito wa kipadre; vijana wanaotaka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia.

Jumuiya ya waamini ni mahali muafaka wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kikanisa. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanaguswa, wanafundwa, wanagangwa na kuponywa na Kristo Yesu. Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa; upatanisho katika maisha ya kiimani na kwamba, huu ni mwaliko kwa wadau mbali mbali kuwasaidia vijana kwa njia ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kuwajibika barabara katika medani mbali mbali za maisha: kitaaluma, kisiasa na kiuchumi; kwa kuzingatia tofauti zinazofumbatwa katika umoja na mkamilishano unaojenga na kudumisha umoja katika udugu. Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa maisha ya sala na useja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu: kielelezo makini cha uhuru wa ndani, furaha, sadaka na unyenyekevu. Kabla ya vijana kufanya maamuzi magumu ya kujiunga na wito na maisha ya kipadre na kitawa, wanapaswa kusaidiwa na watu wenye sifa na ubora; wanaoweza kuwasikiliza, kuwasindikiza katika imani na sala; kwa kuangalia uwezo na mapungufu yao, ikiwa kama wanastahili kusonga mbele.

Wasahihishwe kwa upendo na udugu pale wanapokosea na kuondokana na tabia ya kutaka kuwamiliki vijana, hali ambayo wakati mwingine, imepelekea matumizi mabaya ya madaraka na hatimaye, nyanyaso mbali mbali! Mababa wa Sinodi wanahimiza umuhimu wa kukuza na kudumisha sanaa ya mang’amuzi katika maisha, inayofumbatwa kwa kukutana na kujenga mahusiano na Kristo Yesu. Ni mahusiano yanayoendelea kwa njia ya majadiliano kati ya kijana na mlezi wa maisha ya kiroho, hali inayopaswa kueleweka kuwa ni mfano wa sala unaohitaji ujasiri na mapambano ya maisha ya kiroho, changamoto katika maisha ya kijumuiya katika udugu na huduma kwa maskini. Vijana wanayo mang’amuzi mapana kuhusu “diakonia” yaani “dhana ya huduma”.

SEHEMU YA TATU: Wakatoka kwa haraka kwenda kutangaza kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani, amefufuka kwa wafu! Mababa wa Sinodi wanakazia ujana wa Kanisa, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha ari na mwako wa kimisionari; Sinodi kama hija ya pamoja inayotekelezwa kila siku ya maisha; upyaisho wa ari ya kimisionari pamoja na malezi fungamani! Mtakatifu Maria Magdalena, mfuasi mmisionari, aliyegangwa na kuponywa madonda yake na shuhuda wa ufufuko ni kielelezo makini cha ujana wa Kanisa. Machungu na madhaifu ya vijana, yanaliwezesha Kanisa kuboreka zaidi kutokana na changamoto zao, “madongo” ambao ni kama sauti ya Kristo inayolitaka Kanisa kutubu, kuongoka na kujipyaisha, kwani vijana wote ni muhimu sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa Kanisa kukumbatia na kuambata dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni ushuhuda wa tofauti zinazofumbatwa katika umoja na mkamilishano, changamoto kwa Mabaraza ya Maaskofu na Makanisa mahalia kuendeleza mchakato wa mang’amuzi, ili kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kukabiliana na matatizo na changamoto kwa Makanisa mahalia.

Dhana ya Sinodi ndiyo mwelekeo sahihi wa kimisionari unaolitaka Kanisa kutoka katika dhana ya ubinafsi na kuanza kujikita katika tunu msingi za maisha ya kijumuiya kwa kutambua changamoto changamani zinazotokana na mang’amuzi ya mahali wanakotoka watu pamoja na tofauti za kitamaduni, zawadi na karama kutoka kwa Roho Mtakatifu ili kusaidia mchakato wa maamuzi ndani ya Kanisa, kwa kuwashirikisha waamini walei katika kukuza na kujenga ari na mwamko wa kimisionari. Uongozi uangaliwe katika jicho la huduma sanjari na mwendelezo wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha vijana katika utume wa Kanisa. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki hayana budi kuanzisha Kurugenzi ya Utume na Miito kwa Vijana ili kusaidia malezi na  majiundo ya vijana. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa na Kimataifa yamepewa mkazo wa pekee kabisa, bila kusahau umuhimu wa vituo vya malezi na michezo kwa vijana.

Changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa digitali zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu na Mama Kanisa, ili kuwasaidia vijana kuwajibika barabara katika malezi, makuzi na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, mahali ambapo kumegeuka kuwa ni “vijiwe vya vijana”. Mitandao ya kijamii, ina faida na hasara zake, changamoto ni kuwajengea vijana uwezo wa kuwa kweli ni raia wanaowajibika katika ulimwengu wa digitali, ili wasitumbukie katika upweke hasi utakaowapelekea katika kifo; wasinyanyaswe wala kudhalilishwa, bali waimarishwe ili kweli mitandao ya kijamii iweze pia kutumika katika kutangaza na kushuhudia nguvu ya Injili inayookoa! Ni wakati wa kutamadunisha na kuinjilisha mitandao ya kijamii, kwa kuimarisha tovuti zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, ili kupambana na habari za kughushi “FAKE NEWS”, kielelezo cha utamaduni usiofumbata na kuambata ukweli. Ziwepo sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo katika tovuti. Kanisa liendelee kuwathamini, kuwaheshimu na kuwashirikisha wanawake katika maisha na utume wake, bila kusahau mchango wake katika jamii, kama sehemu ya upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika uongozi wa Kanisa na vikao mbali mbali vya maamuzi, kwa kuheshimu pia dhamana na wajibu wa wakleri waliopewa daraja, kwani hii ni sehemu ya haki inayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu.

Mababa wa Sinodi wanakazia umuhimu wa kuheshimu maadili na utu wema, kwa kuepuka picha za utupu zinazoendelea kuzagaa katika mitandao ya kijamii, utalii wa ngono pamoja na ukahaba wa kwenye mitandao. Vijana watambue na kuheshimu miili yao kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa liwasaidie vijana kutambua ukweli huu, ili kusaidiana na kukamilishana katika tofauti zao za kijinsia. Kanisa liwe na uwezo wa kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa tendo la ndoa, hali inayohitaji malezi na majiundo makini, kwa kukazia pia useja kama zawadi na sadaka katika maisha inayoweza kuwasaidia watu kufikia ukomavu katika miito mbali mbali. Sehemu hii inahitaji walezi makini wanaoweza kuwasaidia vijana kutambua uzuri na utakatifu wa miili yao, jambo linaloweza kufafanuliwa: kiutu, kitaalimungu na kichungaji kadiri inavyofaa, ili kupambanua: tofauti na uhusiano wa jinsia ya kiume na kike; umuhimu wa kuondokana na nyanyaso za kijinsia kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa mahusiano ya kijinsia. Watu wenye mielekeo ya mahusiano ya ndoa za watu wa jinsia moja, wasaidiwe kutambua uhuru na wajibu wao.

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa halina budi kutenga rasilimali fedha na watu kwa ajili ya kuwasindikiza vijana ili waweze kukua na kukomaa na hatimaye, kufanya mang’amuzi sahihi ya miito yao, kwa kuondokana na mazoea katika mazingira! Wanandoa wachanga waendelee kusindikizwa kwa njia ya ushauri na mifano ya familia bora za Kikristo, ambazo zinapaswa pia kushirikishwa kikamilifu katika malezi, majiundo na makuzi ya wanandoa wapya. Talaka na ndoa sugu ni kati ya matatizo makubwa yaliyobainishwa na Mababa wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwani kuna baadhi ya waamini ambao kwa makusudi mazima, wanafyekelea mbali sheria, kanuni na taratibu za Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia, tabia ambayo inawafanya waamini kama hawa kushindwa kuwajibika, na hivyo kuwa ni tatizo kubwa kwa jumuiya ya Kikristo! Mababa wa Sinodi wanahitimisha hati yao kwa kusema kwamba, waamini katika miito yao mbali mbali wanaitwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ili kuimarisha na kukuza utakatifu wa Kanisa, kwa kuendelea kuwa waaminifu na wadumifu kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kushuhudia furaha ya Injili hata katika madhulumu na nyanyaso, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kitume ndani ya Kanisa!

MAADHIMISHO YA SIKU YA VIJANA DUNIANI, PANAMA JANUARI 2019.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati leo ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utamaduni na sanaaa ya watu kukutana pamoja na kuwasikilisha vijana ni amana na urithi mkubwa wa Kanisa kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyohitimishwa hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuitikia wito unaowashirikisha leo ya Mungu ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwa na imani na ujasiri thabiti kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Anawashukuru na kuwapongeza vijana waliotikisa Panama kwa uwepo na ushuhuda wao! Kwa ufupi, huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 27 Januari 2019, kwenye Uwanja wa Metro Park, kwa bahari ya vijana waliokuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko nchini Panama.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee, leo ya Mungu iliyofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha yake ya hadhara. Amepakwa mafuta kuwahubiri maskini maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao pamoja na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Leo ya Mungu imemwilishwa katika Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; mtetezi na haki ya wanyonge. Leo ya Mungu anasema Baba Mtakatifu haikupokelewa kwa mikono miwili na watu wa Nazareti kutokana na mazoea yao, kiasi cha kumwona Kristo Yesu, kuwa “si mali kitu” bali mwana wa Yosefu, Seremala.

Chimbuko la Wosia
25 March 2019, 12:12