Waraka: Kujitoa Kikamilifu: Mtazamo wa Kikristo kuhusu Michezo Waraka: Kujitoa Kikamilifu: Mtazamo wa Kikristo kuhusu Michezo 

Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu!

Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatambua na kuthamini kwamba, michezo ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Mashindano ya Baiskeli Nchini Italia ni tukio ambalo limekuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki na wapenda michezo ndani na nje ya Italia. Mashindano haya yanajulikana kama “Giro d’Italia” ambayo kwa mwaka 2019 yanahitimishwa tarehe 28 Mei 2019. Huu ni mchezo unaowawezesha washiriki kujionea wenyewe uzuri na utamaduni wa watu wa mahalia na kwamba, hiki ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya imani na michezo; tunu msingi zinazokamilishana katika hija ya maisha ya watu. Kunako mwaka 1949 Papa Pio XII alimtangaza  Bikira Maria wa Ghisallo kuwa ni msimamizi wa wapanda baiskeli duniani.

Kilima cha Ghisallo ni eneo takatifu, na limekuwa likitumika sana kwa ajili ya masindano makubwa makubwa ya Baiskeli nchini Italia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ni Msimamizi wa Wapanda Baiskeli nchini Italia tangu mwaka 2014. Mabingwa wa mashindano kutoka dini mbali mbali wamepata pia fursa ya kumshukuru Bikira Maria wa Ghisallo, matendo makuu ya Mungu! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipewa kadi ya uanachama kunako mwaka 2007. Viongozi wengine waliowahi kupewa kadi ya uanachama ni pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa Yohane Paulo I, Mtakatifu Yohane XXIII, Mtakatifu Paulo V pamoja na Papa Pio wa XII.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi  mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha!

Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.

Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Dhana ya Michezo katika Kanisa
09 March 2019, 15:14