Tafuta

Vatican News
Siku ya Furaha Duniani 2019: Papa Francisko anatoa kanuni kumi zinazomwezesha mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha yake! Siku ya Furaha Duniani 2019: Papa Francisko anatoa kanuni kumi zinazomwezesha mtu kuwa na furaha ya kweli katika maisha yake!  (Vatican Media)

Siku ya Furaha Duniani 2019: Papa: Kanuni za furaha!

Viashiria vya furaha duniani ni pamoja na uwezo wa kiuchumi, huduma bora za kijamii, matumaini, uhuru, upendo na ukarimu pamoja na kuwa na jamii isipekenywa na rushwa na ufisadi, mambo yanayodhalilisha utu na haki msingi za binadamu! Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake jadidi anataja mambo makuu kumi, yanayoweza kumpatia mtu furaha ya kweli katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa kunako tarehe 28 Juni 2012, ulianzisha Siku ya Furaha Kimataifa, inayopaswa kuadhimishwa na Nchi wanachama wote wa Umoja wa Mataifa, kila mwaka ifikapo tarehe 20 Machi. Umoja wa Mataifa unatambua ukweli kwamba, mwanadamu katika hija ya maisha yake, daima anatafuta cheche za maisha ya furaha, zinazoweza pia kusaidia kukuza na kudumish: uchumi, maendeleo endelevu na fungamani pamoja na mapambano dhidi ya umaskini. Maadhimisho haya yawasaidie watu kutambua na kudumisha furaha ya kweli katika maisha kama sehemu ya haki msingi za binadamu!

Umoja wa Mataifa unasema, viashiria vya furaha duniani ni pamoja na uwezo wa kiuchumi, huduma bora za kijamii, matumaini katika maisha, uhuru wa kweli, upendo na ukarimu pamoja na kuwa na jamii isiyopekenywa na saratani ya rushwa na ufisadi, mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake jadidi anataja mambo makuu kumi, yanayoweza kumpatia mtu furaha ya kweli katika maisha kwa: kuwajali wengine; kwa kuondokana na uchu wa mali, utajiri na madaraka, ili kukazia upendo na huduma makini kwa watu!

Baba Mtakatifu anawaalika watu kukuza na kudumisha kipaji cha ucheshi katika maisha Ili kupata furaha ya kweli anasema, kuna haja pia ya kuwa ni watu wa shukrani, kwani falsafa ya kushukuru ni kuomba tena! Watu wajifunze kusamahe na kusahau kama njia ya kujenga na kudumisha amani, furaha na utulivu wa ndani! Watu wajitafutie muda wa mapumziko, ili kupyaisha tena miili yao na kujichotea nguvu. Mapumziko haya yanaweza kuwa ni kwa njia mafungo ya kiroho au kwa mtu kujipatia muda wa kuwa nje ya shughuli za kawaida ili kujikita katika Heri za Mlimani na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wajipatie muda wa mapumziko kwa kuabudu na kutafakari mbele ya Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, sala na udugu ni chechemi ya furaha ya kweli katika maisha ya watu wa Mungu. Si rahisi sana kusali, yataka moyo, lakini, waamini hawana budi kujenga utamaduni wa kutenga muda wa sala, ili kuzungumza na Mwenyezi Mungu katika maisha yao: Kwa kushukuru, kuomba, kutukuza na kusifu. Katika shida na mahangaiko ya ndani, katika raha na karaha za maisha; mwamini ajifunze daima kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwani daima atamlinda kama mboni ya jicho lake! Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanadamu amezaliwa ili kufurahia maisha yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Yaani hadi raha!

Siku ya Furaha Duniani 2019

 

 

20 March 2019, 14:37