Vatican News
Papa Francisko anawapongeza wanamichezo kwa kudumisha: uadilifu, uthabiti wa moyo na maisha ya kujisadaka! Papa Francisko anawapongeza wanamichezo kwa kudumisha: uadilifu, uthabiti wa moyo na maisha ya kujisadaka! 

Papa Francisko: Michezo: Uadilifu, uthabiti wa moyo na sadaka!

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza sana wapanda baiskeli kwani wengi wao wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika michezo na maisha kutokana na uadilifu na uthabiti wa maisha kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika michezo ya wapanda baiskeli. Anasikitishwa sana na ubinafsi, uchu wa mali na faida kubwa; rushwa, ufisadi na matumizi haramu ya dawa za kuongeza nguvu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Kanisa na Michezo na kumekuwepo na historia ya mahusiano na mafungamano ya muda mrefu na kwamba, mahusiano haya yanaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka. Michezo ni chachu inayowawezesha wanamichezo kujitoa kikamilifu ili kuweza kufikia malengo katika maisha. Michezo inawasaidia watu kujenga udumifu, sadaka na majitoleo binafsi. Michezo inahitaji mazoezi na nidhamu ya hali juu kabisa katika maisha na kwamba, hii ni chachu inayokoleza ari na moyo wa kusonga mbele pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, baada ya kutekeleza na kuanguka au baada ya kupata majeraha na kuanza kuchechemea!

Mashindano ya wapanda baiskeli si lele mama, kwani ni kati ya michezo inayofumbatwa katika mchakato wa uvumilivu, ujasiri, tabia ya kuwajali wengine na ujenzi wa moyo wa kufanya kazi kwa pamoja kama timu! Ni mashindano yanayowashirikisha wapanda baiskeli wenyewe pamoja na wasaidizi wao. Mara nyingi watu hawa hawana budi kujisadaka kwa ajili ya wenzao katika mashindano. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika maisha, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa ajili ya wengine pamoja na kujenga jumuiya, ili kuwasaidia kusonga mbele wale watu ambao wanaonekana kubaki nyuma, ili hata wao waweze kusonga mbele na hatimaye, kufikia malengo yanayokusudiwa!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Mkutano wa Wapanda Baiskeli Barani Ulaya kwa mwaka 2019, alipokutana nao siku ya Jumamosi, tarehe 9 Machi 2019 mjini Vatican Mwaka huu, Chama cha Wapanda Baiskeli Italia kinawakarimia pia wajumbe kutoka Afrika. Baba Mtakatifu amewapongeza sana wapanda baiskeli kwani wengi wao wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika michezo na maisha kutokana na uadilifu na uthabiti wa maisha kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika michezo ya wapanda baiskeli.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika taaluma yao, wamebahatika kuunganisha fadhila ya nguvu na utashi ili kuweza kufikia ushindi; kwa kudumisha mshikamano, furaha ya maisha na ushuhuda kwamba, wao ni binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, wanapenda kumwilisha uzuri huu kwa kuishi vyema na wengine! Wanamichezo wanayo bahati kubwa ya kuweza kuwashirikisha watu wengi zaidi, lakini hususan vijana tunu msingi za maisha pamoja na ari ya kutaka kumwilisha tunu hizi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa jirani zao!

Waswahili wanasema, eti katika msafara wa Mamba, Kenge hawakosekani! Kinyume cha tunu msingi katika michezo, kwa bahati mbaya, michezo imegeuka kuwa ni chombo cha kudumisha ubinafsi; kuwageuza watu wengine kuwa ni vyombo vya huduma, ili kujipatia faida kubwa na matokeo yake ni matukio ambao yanachafua kwa kiasi kikubwa tasnia ya michezo duniani. Baba Mtakatifu anasema, matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, rushwa na ufisadi; na hatimaye, wanamichezo kukoseana heshima na adabu ni mambo yanayochefua tasnia ya michezo duniani!

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mchezo wa wapanda baiskeli miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, hali inayoweza kusababisha “patashika nguo kuchanika” kwa vikongwe wa mchezo huu ambao bado wanaoongozwa na mapokeo. Kanisa limejizatiti kuwasikiliza vijana, kuwasaidia kutekeleza matamanio yao halali ambao ni msaada mkubwa hata kwa wapanda baiskeli. Ni vyema wanamichezo wakongwe na wazoefu kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya, kwa kuendelea kujikita katika kuimarisha mapokeo na tamaduni njema zinazowaambata na kuwasindikiza mabingwa wengi wa mchezo wa wapanda baiskeli!

Wapanda Baiskeli
09 March 2019, 15:46