Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Katekesi ya Sala ya Baba yetu: Ufalme wako ufike! Muhtasari wa Injili! Papa Francisko: Katekesi ya Sala ya Baba Yetu: Ufalme wako ufike! Muhtasari wa Injili!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sala ya Baba Yetu: Ufalme wako ufike!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kipengele cha “Ufalme wako ufike”. Huu ni muhtasari wa Injili ilityotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu katika mateso, kifo na ufufuko wake. Huu ni ufalme wa haki, amani na furaha, changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu! Ukuu wa Mwenyezi Mungu unajionesha karibu na kati na watu wake wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sala ya Bwana au “Baba Yetu” ni muhtasari wa Injili yote; ni “roho na uzima” na kwamba, ni sehemu ya utume wa Fumbo la Mwana na wa Roho Mtakatifu. Hii ni sehemu ya Liturujia ya Kanisa inayowaunganisha waamini kuwa wamoja katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hii ni Sala ya wokovu. Baba Yetu ni sala inayoonesha unyenyekevu, utakaso, ushirika, tamaa ya kutaka kufanana naye; imani na matumaini ni mambo msingi katika Sala ya Bwana! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Machi 2019 amesema, baada ya kutafakari kuhusu kipengele cha “Baba Yetu” kinachoonesha: Ukuu, utakatifu, upendo na uwamo mmoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na baadaye kutafakari kipengele cha “Uliye Mbinguni na Jina lako Litukuzwe” amegeukiwa kipengele cha “Ufalme wako ufike”.

Huu ni muhtasari wa Injili ilivyotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu katika mateso, kifo na ufufuko wake. Huu ni ufalme wa haki, amani na furaha, changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu hataki wongofu wa shuruti, bali anatangaza na kushuhudia umuhimu wa kutubu na kuiamini Injili, kwani ukuu wa Mungu unajionesha karibu na kati ya watu wake, kwani Mwenyezi Mungu ni Baba na anawapenda wote na anataka watoto wake watembee katika njia ya utakatifu wa maisha. Alama za uwepo wa Ufalme wa Mungu ni pamoja na kuganga na kuwaponya wagonjwa: kiroho na kimwili; kusamehe na kuwaondolea watu dhambi zao; kuwajali na kuwathamini hata wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; kufufua na kuwarejeshea tena watu uzima mpya!

Kristo Yesu ni kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu. Lakini ujio wake, bado unaathiriwa na dhambi; mateso na mahangaiko ya watu; nyanyaso na dhuluma! Vyote hivi ni vielelezo kwamba, ushindi wa Kristo bado haujakamilika barabara miongoni mwa watu kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuwa na mioyo migumu! Ni kutokana na changamoto hizi kwamba, waamini wanamwita Mwenyezi Mungu “Ufalme wako ufike”, kuonesha kwamba, wanahitaji uwepo wa Mungu na Kristo Yesu! Ufalme wa Mungu unakua pole pole kama ngano na wakati mwingine unasongwa na magugu, ili kuonesha unyenyekevu na uvumilivu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Ufalme wa Mungu una nguvu kubwa ajabu, lakini si kadiri ya vigezo vya ulimwengu huu! Ufalme wa Mungu ni sawa na chachu inayotiwa katika unga ili uweze kuumuka wote; ni sawa na punje ya haradali. Kristo Yesu ni kielelezo makini cha Ufalme wa Mungu, chembe ya ngano iliyoanguka ardhini, ikafa Ijumaa kuu na kuzaa matunda ya Ufufuko, Jumapili ya Pasaka, mwanga wa matumaini ya watu wa Mataifa. Mbegu ya Ufalme wa Mungu inapaswa kupandikizwa kati ya watu, katika dhambi na udhaifu wao. Ni zawadi inayopaswa kutolewa kwa watu waliokata tamaa, wale wanaoelemewa na ugumu wa maisha; watu ambao wameonja chuki na uhasama badala ya huruma na upendo; watu ambao wamepoteza dira na mwongozo wa maisha pasi na kufahamu.

Ufalme wa Mungu utolewe kwa wale wote wanaosimama kidete kupigania haki; mashahidi wa historia; watu waliojizatiti kupigania utakatifu, lakini wakakuta kwamba, dunia imesheheni ubaya wa moyo na dhambi! Sala ya Baba Yetu ni Sala ya matumaini ya ujio wa Kristo Yesu kati ya watu wake!

Ufalme Wako Ufike
06 March 2019, 15:44