Papa Francisko asikitishwa sana na maafa yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai kilichosababisha majanga nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe. Papa Francisko asikitishwa sana na maafa yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai kilichosababisha majanga nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe. 

Papa asikitishwa na maafa: Msumbiji, Malawi na Zimbabwe

Kimbunga cha Idai kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia. Wote hawa, amewaweka chini ya huruma na upendo wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Sala ya Baba Yetu wa Mbinguni, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano, 20 Machi 2019 aliyaelekeza mawazo yake, Barani Afrika ambako kimbunga cha Idai kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia. Wote hawa, amewaweka chini ya huruma na upendo wa Mungu!

Kimbunga kijulikanacho kama Idai, hivi karibuni kimesababisha mvua kubwa iliyopelekea maafa makubwa mjini Beira ambako inasemekana kwamba, walau asilimia 90% ya eneo lote limeharibiwa vibaya sana. Zaidi ya watu 84 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 1500 wamejeruhiwa vibaya sana. Idadi ya watu waliofariki dunia inatarajiwa kuongezeka maradufu. Nchini Zimbabwe, kimbunga hiki kimesababisha maafa makubwa kwenye Wilaya ya Chimanimani, kiasi kwamba, miundo mbinu ya usafiri imeharibiwa sana!

Nchini Malawi, zaidi ya watu 56 wamefariki dunia na wengine 577 kujeruhiwa na kwamba, kuna watu 3 hawajulikani mahali walipo. Zaidi ya familia 11, 000 hazina makazi malum kwa sasa katika Wilaya Nsanje. Maeneo yote yaliyokumbwa na kimbunga cha Idai yanahitaji msaada wa dharura, ili kuanza tena upya na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa waathirika wa majanga haya asilia!

Papa: Maafa Afrika
20 March 2019, 15:24