Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni muda wa kusali, kutafakari na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Papa Francisko asema, Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; ni muda wa kusali, kutafakari na kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Kwaresima ni muda wa sala, toba na wongofu

Kipindi cha Kwaresima, safari ya Siku 40 katika Jangwa la Maisha ya Kiroho: Ni muda wa kusali, kufunga, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika Injili ya upendo. Ni muda wa toba na wongofu tayari kurejea tena nyumbani kwa Baba baada ya kutopea katika dhambi na ubaya wa moyo! Ni muda wa kukimbilia: huruma, upendo na msamaha wa Baba mwenye huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, safari ya Siku 40 katika Jangwa la Maisha ya Kiroho: Ni muda wa kusali, kufunga, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika Injili ya upendo: kiroho na kimwili! Huu ni muda wa toba na wongofu wa ndani; ni muda wa kurejea tena nyumbani kwa Baba baada ya kutopea katika dhambi na ubaya wa moyo! Ni muda wa kutubu na kukimbilia tena huruma, upendo na msamaha wa Baba wa  milele kama ilivyokuwa kwa Mwana Mpotevu!

Huu ndio mwaliko ambao umetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 6 Machi 2019 kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hija ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2019 izae matunda yatakayowawezesha waamini kumfuasa Kristo Yesu kwa ukaribu zaidi, ili kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume, waweze kuthubutu kusema pamoja na Mtume Paulo kwamba, “Si mimi ninayeishi, bali Kristo anaishi ndani mwangu”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, alama ya majivu wanayopakwa waamini kichwani, iwasaidie kutambua kuwa wao ni wadhambi na kwamba, wanaelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia hii, waamini wanahamasishwa kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya nyoyo na akili zao, ili kutambua maana halisi ya maisha katika mwanga wa Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Papa: Jumatano ya Majivu
06 March 2019, 15:22