Cerca

Vatican News
Papa Francisko. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu na umoja kati ya watu wa Mataifa! Papa Francisko: Majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu na umoja kati ya watu wa Mataifa!  (ANSA)

Papa: Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha amani

Papa Francisko anasema, majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama kwa Wayahudi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wana wajibu wa kulinda uhai, kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu pamoja na kujikita katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbali mbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Kizazi baada ya kizazi kinapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupendwa kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote.

Hii ndiyo changamoto endelevu iliyoko mbele ya waamini wa dini mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajenga nyumba na familia zitakazokuwa na upendo kwa Mungu pamoja na kuheshimu tunu msingi za maisha ya kiroho, kwa ajili ya ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 8 Machi 2019, alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Kamati ya Wayahudi wa Marekani inayoendeleza majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakatoliki.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 amekumbusha kwa kusema kwamba, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi duniani. Ni kundi ambalo limechangia sana kulinda na kuenzi uhai, kiasi hata cha kuthubutu kujisadaka. Wanawake ni walinzi wakuu wa amani duniani, inayobubujika kutoka katika maisha yao kama akina mama. Wanawake ni wenza wakuu wa maendeleo na wanabeba ndani mwao ile ndoto ya upendo! Wanawake wanayo ndoto ya leo na kesho ya amani, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanawake wanapewa nafasi.

Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na wimbi kubwa la vitendo vya kikatili, chuki na uhasama unaofumbatwa katika misimamo mikali ya kidini; maamuzi mbele mambo ambayo katika historia ya maisha ya mwanadamu yamechangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya kimbari kama yale yaliyotokea katika Shoah, kiasi cha kusababisha idadi kubwa ya Wayahudi Barani Ulaya kupoteza maisha yao. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Wayahudi na Wakristo, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wazazi wanawarithisha watoto wao upendo kwa Mungu na jirani pamoja na kuheshimiana kama binadamu, ili kukuza na kudumisha amani duniani, kwa kutumia “miwani ya akina mama”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama kwa Wayahudi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wa dini mbali mbali wanao wajibu na dhamana ya kulinda uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini pamoja na kujikita katika mchakato wa kutunza mazingira nyumba ya wote! Ikumbukwe kwamba, Wayahudi na Wakristo wanao utajiri na amana ya maisha ya kiroho pamoja na mambo mengi mazuri wanayoweza kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Waamini wa dini mbali mbali wajenge na kudumisha upendo kwa Mungu na binadamu; kwa kuhudumiana na kusaidiana kwa hali na mali. Wayahudi na Wakristo wanahamasishwa kusimama kidete kuwalinda maskini, wagonjwa, watoto na wazee bila kuwasahau wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma kwa binadamu, majadiliano ya kidini ni mambo msingi ambayo pia wanapaswa kushirikishwa vijana wa kizazi kipya, ili kung’amua mambo mapya katika maisha yao. Changamoto hii inakwenda sanjari na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya katika misingi ya majadiliano kati ya Wayahudi na Wakristo. Majadiliano ya kidini ni nyenzo msingi katika ujenzi wa amani!

Papa: Wayahudi
08 March 2019, 15:48