Tafuta

Vatican News
Papa Francisko. Kwaresima ni kipindi cha kukazia mambo msingi katika maisha ya kiroho! Papa Francisko. Kwaresima ni kipindi cha kukazia mambo msingi katika maisha ya kiroho! 

Papa Francisko: Dumisheni misingi ya maisha ya kiroho!

Kwaresima iwawezeshe waamini kukazia mambo msingi katika maisha ya kiroho yaani: kusali kunakowaunganisha na Mungu; sadaka ikoleze upendo kwa jirani na kufunga kusaidie kurekebisha vilema. Kwaresima iwasaidie waamini kumwangalia Mungu kwa njia ya Sala na jirani kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kuondokana na maisha ya ubatili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha kumrudia Mwenyezi Mungu kwa toba na kufunga, kwa kurarua mioyo ili kukazia mambo msingi ya maisha, tayari kupyaisha maisha ya kiroho. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kukuza na kudumisha mapambano ya maisha, ili kuweza kufikia lengo linalokusudiwa, bila kuridhika kwa mafanikio yaliyofikiwa hadi wakati huu! Mwenyezi Mungu ndiye lengo kuu la Mfungo wa Kwaresima, mwaliko na changamoto kwa waamini kumrudia Mungu, safari inayoanza kwa Jumatano ya Majivu, waamini wanapopakwa majivu, ili kukumbushwa ukweli kwamba wao ni mavumbi na mambo yote wanayobeba, hakuna litakalosalia hata moja!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe 6 Machi 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, baada ya kufanya maandamano ya toba kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi, ili kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, tukio linalotanguliwa na Kipindi cha Kwaresima. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, waamini walipakwa majivu na Kardinali Joseph Tomko ndiye aliyempaka majivu Baba Mtakatifu Francisko, alama ya toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia mambo msingi katika maisha ya kiroho!

Baba Mtakatifu anasema, Kwaresima ni wakati muafaka wa kuondokana na utamaduni wa mwonekano wa nje, unaowafanya waamini kuelea katika ombwe na maisha ya kufikirika. Waamini wanapaswa kuwa ni moto wa kuotea mbali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wala si majivu; wanapaswa kujielekeza zaidi katika maisha ya uzima wa milele na wala si katika mambo mpito ya dunia hii. Wanapaswa kufikiri na kutenda kama watoto wa Mungu na wala si kama watumwa wa mambo! Kwaresima iwe ni fursa kwa waamini kufanya tafakari ya kina ili kuangalia wao wako upande gani? Je, wako hai kama moto wa kuotea mbali, au tayari wamezimika na kusahaulika kama majivu?

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kwaresima inawawezesha waamini kukazia mambo msingi katika maisha ya kiroho yaani: kusali kunakowaunganisha na Mungu; sadaka inakoleza upendo kwa jirani na kufunga kunasaidia kurekebisha vilema; mambo msingi ambayo waamini wanapaswa kuwekeza huko zaidi. Kwaresima iwasaidie waamini kumwangalia Mungu kwa njia ya Sala na jirani kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kuondokana na maisha ya ubatili. Mfungo uwasaidie waamini kuchunguza vyema dhamiri zao ili kuondokana na tamaa ya malimwengu! Sala, Matendo ya huruma na Kufunga ni amana na utajiri unaodumu daima; kumbe, inalipa kuwekeza huko!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujiwekea hazina mbinguni kwa kuwa hazina yao ilipo, ndipo utakapokuwapo moyo wao na kamwe wasikubali kuwa ni watumwa wa mambo mpito kama vile: fedha na utajiri; kazi na starehe! Waamini watafute na kuwekeza katika mambo yanayodumu, yatakayowawezesha kuuweka moyo huru kutokana na mambo ya ubatili. Kwaresima ni kipindi cha kuganga na kuponya mambo yanayowafanya waamini kuwa tegemezi, ili kujizatiti zaidi na mambo yanayodumu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Msalaba wa Kristo Yesu ni dira na mwongozo wa maisha unaowaelekeza watu njia ya kwenda mbinguni. Hapa, waamini wanaweza kuonja umaskini wa mbao, ukimya wa Kristo Yesu, mateso, dharau na nyanyaso mambo yanayoonesha maisha ya kawaida, huru na ambayo hayafungwi na mambo mengi sana! Kristo Yesu, Msalabani anawafundisha waja wake, ujasiri wa kujikatalia: ulaji wa kupindukia, ubinafsi na tamaa isiyokuwa na kikomo, tayari kufungua malango ya nyoyo zao ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Kristo Yesu, Msalabani anawataka wafuasi wake, wawe ni mashuhuda wa upendo!

Kipindi cha Kwaresima kinaanza kwa kupakwa majivu, lakini, kitahitimishwa kwa Moto wa Pasaka, pale, Kristo Yesu atakapofufuka kwa wafu. Waamini wakimrudia Mungu kwa sala, sadaka na kufunga, hata wao watapewa maisha yasiyokuwa na mwisho!

Papa: J5 Majivu
07 March 2019, 11:02