Tafuta

Papa Francisko: Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu Papa Francisko: Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu 

Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu

Mapadre wanakumbushwa kwamba, wao ni vyombo vya huduma ya upatanisho. Wanapaswa kutambua umuhimu wa kipindi cha Kwaresima katika maisha na utume wao; madhara ya dhambi ndani ya Kanisa pamoja na toba na wongofu wa ndani kama sehemu ya mchakato wa kukumbatia hija ya utakatifu wa maisha. Kwaresima ni kipindi cha sala, sadaka na huduma ya upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 7 Machi 2019 amekutana na kuzungumza kwa faragha na wakleri wa Jimbo kuu la Roma, kama sehemu ya mapokeo ya mwanzo wa kipindi cha Kwaresima. Baba Mtakatifu ameongoza Ibada ya Toba kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano pamoja na kuwaungamisha baadhi ya mapadre. Katika tafakari yake, amewakumbusha mapadre kwamba, wao ni vyombo vya huduma ya upatanisho kati ya Mungu na wanadamu, umuhimu wa kipindi cha Kwaresima katika maisha na utume wa wakleri; madhara ya dhambi na kwa namna ya pekee, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa na umuhimu wa toba na wongofu wa ndani kama sehemu ya mchakato wa kukumbatia hija ya utakatifu wa maisha. Kwaresima ni kipindi cha sala, sadaka na huduma ya upendo!

Baba Mtakatifu anasema, Ibada ya Upatanisho ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia huruma, upendo na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, waamini wanakirimiwa tena maisha mapya baada ya kuanguka dhambini na kupoteza ile neema ya utakaso waliyopewa wakati wa Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya upatanisho, Kanisa linazidi kukua na kupanuka, kwa kumfuasa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa. Huu ni mwaliko wa kujitakasa kwa kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuzungumza kutoka katika undani wa maisha ya watu, ili kweli wakleri waendelee kuwa ni vyombo vya huruma na upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Katika maisha na utume wa kipadre, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza!

Kwaresima ni kipindi cha neema na mwaliko wa kuanza tena upya safari ya maisha ya kiroho, kwa kutambua kwamba, kama binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanayo mambo mengi yanayowatofautisha, lakini hata katika tofauti zao msingi, bado wanaunganishwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na wanawakuwa wamoja katika maisha na utume wa kikuhani. Ibada ya Upatanisho iendelee kuimarisha umoja na mshikamano kati ya wakleri pamoja na waamini katika ujumla wao, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa pamoja na familia ya binadamu! Kwaresima ni kipindi cha kumwilisha Injili ya upendo kwa watu wote bila ubaguzi anasema Baba Mtakatifu.

Wongofu wa kichungaji Jimbo kuu la Roma ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2025, mwaliko wa kutoka na kumwendea Mungu, ili aweze kupyaisha maisha yao kwa neema na uwepo wake endelevu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kwenye Agano la Kale. Ni watu waliokuwa na shingo ngumu, lakini, daima waliendelea kuonja huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa kuwapatia faraja yake. Kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu, kusamehe na kupatana ni mwanzo wa utakatifu wa maisha! Sakramenti ya Upatanisho ni chombo madhubuti katika kuimarisha umoja na mshikamano wa kidugu, kwa kutambua kwamba, hata katika mapungufu yao ya kibinadamu, bado Mwenyezi Mungu anawakirimia nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili kuendelea na safari ya kuwatakasa watu wa Mungu.

Tabia ya mtu kutaka kujiamini kupita kiasi, mara nyingine inaweza kumtumbukiza katika upweke hasi na hali ya kujikatia tamaa. Wakleri wakumbuke kwamba, bila ya uwepo wa Mungu kati pamoja nao, wao si mali kitu! Mapadre wawe na ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu pale wanapoanguka dhambini kwa kuelemewa na ubinafsi na uchoyo katika maisha. Mwenyezi Mungu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho; nyakati zote ni zake. Kwa kutambua, kukiri, kutubu na kuongoka, mapadre wanapyaisha tena maisha na utume wao kama vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maadhimisho ya mafumbo mbali mbali ya Kanisa! Mwenyezi Mungu alijifunua mbele ya Mtumishi wake Musa kuwa ni Mungu ambaye ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema na kweli; mambo msingi yaliyomwezesha Mwenyezi Mungu kuambatana daima na watu wake, licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu!

Ni Mungu ambaye aliwakomboa kutoka utumwa huko Misri kwa mkono wenye nguvu. Waisraeli katika maisha yao walipata mang’amuzi ya uwepo wa dhambi na ubaya wa moyo pamoja na huruma na msamaha wa Mungu kwa ajili yao. Kutubu dhambi kunawawezesha waamini kuonja huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kwaresima ni kipindi cha neema, kinachowapatia waamini fursa ya kukimbilia tena huruma na msamaha wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wakumbmuke kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kama ilivyokuwa kwa Mtumishi wa Mungu Musa, wao pia wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya upatanisho kati ya Mungu na binadamu, tayari kuwaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa Mungu.

Hawa ni watu wa Mungu katika utakatifu na mapungufu yao kama binadamu! Mapadre wanao wajibu na dhamana ya kuwaungamisha na kuwaondolea watu dhambi zao bila kusahau kuwaombea kama kielelezo cha imani kwa Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo! Baba Mtakatifu amewaambia Mapadre kwamba, haipendezi hata kidogo, kila wakati Mapadre kupeleka litania ya malalamiko ya waamini wao kwa Maaskofu mahalia! Daima wajitahidi kuiona ile sura ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kama Musa, wataweza kupata neema na baraka ya kuwa ni marafiki wapenzi wa Mungu kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya watu wao kiroho na kimwili.

Mapadre wasisahau kuwakumbuka na kuwaombea watu wao neema na baraka kama ilivyokuwa kwa Musa! Baba Mtakatifu anawataka Wakleri kujifunua na kujiachia wazi mbele ya Mungu anayewafahamu fika hadi undani wa maisha yao! Lakini hata katika utupu wa maisha na utume wao, bado Mwenyezi Mungu amediriki kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo, msamaha na upatanisho. Ni kwa njia ya mikono yao iliyowekwa wakfu kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kuwatumia ili kuwakomboa watu wake. Dhambi inaharibu uhusiano na Mungu pamoja na jirani. Inachafua maisha na utume wa Kanisa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo imelichafua sana Kanisa hata kama ni kazi ya Ibilisi, Shetani! Kristo Yesu kwa kutakasa Kanisa lake, anataka viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kutambua kwamba, wao ni mavumbi!

Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, kuna dhambi mbele yao, kumbe wanapaswa kuwa makini, wanapoelemewa na udhaifu pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu, wawe na ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho. Sadaka na majitoleo yao, toba na wongofu wa ndani yawasaidie waamini kuonja huruma na upendo wa Mungu na kwao uwe ni mwanzo wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Mapadre katika maisha, wito na utume wao wanakabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali na hata wakati mwingine, wanakumbana na dhuluma pamoja na nyanyaso. Pale ambapo Mapadre hawasutwi na dhamiri zao kuhusu ubaya wa dhambi; pale Neno la Mungu linapokosa nguvu katika maisha na utume wao; pale Mapadre wanapowadharau na kuwakejeli maskini na hasa pale ambapo Mapadre wanamezwa na malimwengu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huo ndio mwanzo wa kulitumbukiza Kanisa katika kashfa nzito!

Pamoja na mapungufu yote haya, Mapadre ni vyombo vya huduma ya upatanisho. Ibada mbali mbali za Upatanisho zitakazoadhimishwa na Mapadre sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, iwe ni nafasi kuomba msamaha kwa Mungu na watu wake, kwa dhambi ambazo zimechafua maisha na utume wa Kanisa; dhambi ambazo zimetishia umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu; dhambi ambazo zimefifisha ari na moyo wa kimisionari ndani ya Kanisa. Kwa njia ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, Mapadre wawe na ujasiri wa kuungamishana wao kwa wao, kwa kutambua kwamba, hata wao wanahitaji uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake kwa kuwataka mapadre wawe mstari wa mbele kuwaombea msamaha watu wao, pale wanapotumbukia dhambini na katika ubaya wa moyo, kwani hizi ni dalili za unyenyekevu, tayari kutubu, kuongoka na kuambata mchakato wa utakatifu wa maisha. Ni kwa njia hii tu, Mapadre wataweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake ambao watatambua uwepo wa Mungu kati pamoja nao!

Papa: wakleri Roma 2019
08 March 2019, 16:56