Papa Francisko: Utume wa Kanisa kwa wakimbizi na wahamiaji: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha katika maisha ya jamii husika! Papa Francisko: Utume wa Kanisa kwa wakimbizi na wahamiaji: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha katika maisha ya jamii husika! 

Hija ya Papa Francisko Morocco 2019: Wakimbizi na wahamiaji

Utume wa Kanisa Katoliki kwa Wakimbizi na Wahamiaji unafumbatwa katika mambo makuu manne: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano!

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019, amekutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji wanaohudumiwa nchini Morocco, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa watu wote hawa! Hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali; wengi wao wanatumbukizwa kwenye mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na magenge ya uhalifu kimataifa! Watu wanapaswa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya kundi hili! Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji nchini Morocco. Amewataka kuendelea kujenga umoja na mshikamano kwa kuheshimu na kuthamini utu wao. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote kwa kujikita katika ukarimu, utayari, busara pamoja na kuwa na malengo ya muda mrefu, kila mdau kadiri ya uwezo na nafasi yake.

Baba Mtakatifu amekumbushia kwamba, hivi karibuni, huko Marrakesh, Morocco, Jumuiya ya Kimataifa ilitia mkwaju kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018 “Global Compact 2018”. Mkataba huu unapania kuhakikisha kwamba mchakato wa uhamiaji unajikita katika: usalama, uratibu pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni hatua kubwa kwani kwa mara ya kwanza katika historia, Jumuiya ya Kimataifa imeweza kuandika hati kuhusu usalama wa wahamiaji na wakimbizi katika ngazi ya kimataifa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Siku ya 105 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 itaadhimishwa Jumapili,  tarehe 29 Septemba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Si Wahamiaji peke yao”. Hii ni changamoto ya kulinda na kudumisha maisha, haki zao msingi, utu na heshima yao.

Ikumbukwe kwamba, maendeleo hayawezi kupimwa kwa kuangalia mafanikio ya maendeleo ya teknolojia na uchumi, bali na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hawa ndio “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanaobisha hodi kila siku wakiomba huduma ya upendo na mshikamano! Huu ni mwaliko wa kupambana na miungu watu, tabia ya kupenda anasa na starehe, kiasi hata cha kuwatumbukiza wengine katika majanga ya maisha! Hii ni alama ya Jumuiya ambayo haina moyo na kama mwanamke tasa! Wakimbizi na wahamiaji ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” ni muhtasari wa sera na mikakati ya Kanisa Katoliki katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama njia ya kujenga na kudumisha mafungamano na kundi hili badala ya kukaa kimya. Ni mwaliko wa kuwaokoa badala ya kuwatenga, ili kuwajengea uwezo badala ya kuwatelekeza. Watu wote wanahusika ili kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapatiwa maisha bora, wanahakikishiwa usalama pamoja na kuoneshwa mshikamano! Inafurahisha kuona kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanakuwa mstari wa mbele kuhudumiana. Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zinapaswa kulindwa na kudumishwa, wakimbizi  na wahamiaji wenyewe wakiwa mstari wa kwanza kutekeleza yote haya!

Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kuingia katika nchi husika kwa njia salama zinazozingatia sheria za nchi; kwa kutoa hati za kusafiria na kuwapatia wakimbizi na wahamiaji nafasi ya kuweza kukutana na kujiunga tena na familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya na Mashirika mbali mbali yatasaidia kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali tete zaidi. Jumuiya ya Kimataifa, kamwe isikubali kuridhia ufukuzaji wa wakimbizi na wahamiaji kwa makundi! Mchakato wa kuwapatia wakimbizi na wahamiaji vibali kwa kuishi hauna budi pia kuzingatia maisha ya kifamilia na watoto wasiokuwa na wazazi au walezi!

Kuwalinda maana yake ni kuhakikisha kwamba haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu inalindwa na kudumishwa, kwa kupatiwa huduma ya faraja; kwa kulinda na kutunza nyaraka na utambulisho wao; kwa kupatia fursa za haki, pamoja na huduma makini ya maisha; kwani kwa hakika, wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni hazina na amana kwa jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi. Mara nyingi wakimbizi na wahamiaji ni kundi ambalo linashuhudia mateso, unyonywaji na nyanyaso za kila aina, hasa watoto, wasichana na wanawake. Wote hawa wanapaswa kupewa huduma ya afya, kisaikolojia na kijamii; mambo ambayo pengine wameyapoteza wakati wakiwa njiani, ili kuwapatia tena matumaini mapya!

Kuwaendeleza wakimbizi na wahamiaji maana yake ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya inayowapokea na kuwakirimia inawapatia fursa ya kujiendeleza katika utimilifu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wapewe uhuru wa kuabudu na kuungama imani yao; fursa za kazi na ajira; nafasi ya kujifunza lugha na tamaduni za watu mahalia, ili kweli waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowapatia hifadhi. Wakimbizi na wahamiaji wanaweza kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ikiwa kama ubaguzi pamoja na chuki dhidi ya wageni vitafyekelewa mbali. Ustawi na maendeleo ya wakimbizi na wahamiaji unapaswa pia kukuzwa na kudumishwa katika nchi wanakotoka wakimbizi na wahamihaji hawa. Watu wana haki ya kuishi katika nchi zao wenyewe bila ya kuwa na sababu ya kuhama wala kuzikimbia nchi zao. Ili kukabiliana na changamoto hii, kuna haja ya kukuza na kudumisha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji wenyewe!

Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, hata katika mwingiliano wa tamaduni, mila na desturi, bado wakimbizi na wahamiaji watabakia na utambulisho wao, lakini wajenge madaraja ya kufahamiana na kuheshimiana, ili kujenga watu wa mila na tamaduni mbali mbali, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu! Mchakato huu unaweza kuendelezwa kwa haraka kwa kutoa vibali vya uraia na vibali vya kuishi kwa muda mrefu, daima utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana na kusaidiana ukipewa kipaumbele cha kwanza, ili kujenga mchakato wa kuwahusisha na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya jamii inayowahifadhi.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hili si jambo rahisi sana, lakini hakuna sababu ya kuwa na hofu zisizo na mashiko, changamoto na mwaliko wa kujenga jamii inayosimikwa katika ukarimu. Ni fursa ya kuheshimu na kuthamini tofauti kwa kukutana na wengine! Kanisa linatambua mateso na mahangaiko yao na kwamba, hata Kanisa linateseka pamoja nao! Kanisa linataka kuwa mwandani wa wakimbizi na wahamiaji ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kutambua kwamba, maisha ni haki msingi ya kila binadamu na kwamba, kila mtu anayo ndoto anayoweza kuimwilisha katika ulimwengu, nyumba ya wote! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wadau mbali mbali wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kumhudumia Kristo Yesu, anayebisha hodi malangoni mwao kama mkimbizi na mhamiaji.

Papa: Wakimbizi na Wahamiaji

 

 

 

31 March 2019, 12:23