Tafuta

Vatican News
Papa Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 ametuma salam na matashi mema kwa viongozi wa Italia, Ufaransa na Hispania. Papa Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Morocco, Jumamosi, tarehe 30 Machi 2019 ametuma salam na matashi mema kwa viongozi wa Italia, Ufaransa na Hispania. 

Hija ya Papa Francisko Morocco 2019: Viongozi wa Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema kwa familia ya Mungu nchini Italia, amemwambia Rais Sergio Mattarella kwamba, anakwenda nchini Morocco ili kukutana na Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki, ili kusali na kujenga umoja; sanjari na kuwatia shime kuendeleza majadiliano ya kidini nchini Morocco

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake ya 28 ya kimataifa nchini Morocco kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 inayoongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”, Ijumaa asubuhi, tarehe 29 Machi 2019 alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kujikabidhi na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, wakati wote wa hija yake ya kitume! Akiwa njiani kuelekea Rabati, Morocco, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa Sergio Mattarella, Rais wa Italia, Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa pamoja na Mfalme Felipe VI wa Hispania.

Baba Mtakatifu katika salam na matashi mema kwa familia ya Mungu nchini Italia, amemwambia Rais Sergio Mattarella kwamba, anakwenda nchini Morocco ili kukutana na Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki, ili kusali na kujenga umoja; sanjari na kuwatia shime kuendeleza majadiliano ya kidini nchini Morocco. Baba Mtakatifu amewahakikishia sala zake, ili Italia iweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha kiroho na kiutu; kwa kujikita katika utulivu na maridhiano, daima mshikamano wa kidugu ukiwa ni njia ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

Baba Mtakatifu katika salam zake kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, anapenda kuitakia familia ya Mungu nchini Ufaransa amani na utulivu na kwamba, anawaombea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko alipokua anaingia katika anga la Hispania, ameitakia heri na baraka familia ya Mungu nchini Hispania, ili iweze kudumu katika ustawi, maendeleo na amani!

Papa: Salama na Matashi Mema
30 March 2019, 16:52