Tafuta

Papa Francisko: Dini zinapaswa kuhusishwa kikamilifu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelebu ya Binadamu kwa kukazia utu na kanuni maadili Papa Francisko: Dini zinapaswa kuhusishwa kikamilifu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelebu ya Binadamu kwa kukazia utu na kanuni maadili 

Papa Francisko: Malengo ya Maendeleo Endelevu: Utu kwanza!

Maendeleo ni mchakato unaofumbatwa katika mafungamano ya kijamii, wongofu wa Kiekolojia; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Uchumi ni wito unaohitaji jibu muafaka na linalowajibisha! Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu unapaswa kujikita katika mchakato wa majadiliano, utashi wa kisiasa pamoja na kutoa nafasi ya ushiriki wa wananchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dini mbali mbali duniani ni sehemu muhimu sana katika kukoleza mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya binadamu. Dini ni mdau mkubwa  katika sekta ya: elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu. Dini zinachangia asilimia 50% kwenye maeneo yaliyoko chini ya Jangwa la Sahara na kwamba, zinachangia zaidi ya asilimia 12% ya rasilimali fedha katika sekta ya afya. Kumbe, dini zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko katika mtindo wa maisha, uzalishaji, biashara, ulaji pamoja na utunzaji bora wa taka.

Dini zinataka kuchangia kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya binadamu kwa siku za usoni. “Dini na Malengo Endelevu ya Binadamu” ndiyo kauli inayoongoza mkutano wa dini kimataifa ulioanza tarehe 7-9, Machi 2019 hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 8 Machi 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano kuhusu dini na Malengo Endelevu ya Binadamu. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa utekelezaji wa maendeleo endelevu na jumuishi; maendeleo fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, malengo yanafikiwa kwa kujikita katika majadiliano na utekelezaji wake kwa kutambua kwamba, mambo haya yote yanategemeana na kukamilishana. Utunzaji bora wa mazingira uzingatie pia upendo kwa jirani na kwa namna ya pekee kwa watu mahalia. Utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu unapaswa kuwa ni mchakato wa kusikiliza kwa makini kilio cha dunia pamoja na maskini. Hawa ndio wakimbizi na wahamiaji, vijana na watu mahalia, ili kwa pamoja waweze kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa maendeleo endelevu, fungamani kwa kuwa na ushiriki mpana zaidi.

Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa majadiliano ya kidunia na kielelezo cha mshikamano mpya wa kimataifa unaotekelezwa katika medani mbali mbali za maisha. Wachumi wanatumia Pato Ghafi la Ndani (GDP) kama kipimo hali ambayo imehatarisha kiasi kwamba, maendeleo kwa sasa yanaweza kufafanuliwa kutokana na vitu na matokeo yake ni matumizi mabaya ya rasilimali za dunia pamoja na nyanyaso dhidi ya watu wengine! Kipimo cha maendeleo endelevu na fungamani ya watu ni watu wenyewe katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Maendeleo ni mchakato unaofumbatwa katika mafungamano ya kijamii, wongofu wa Kiekolojia; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili.

Hii inatokana na ukweli kwamba, uchumi ni wito unaohitaji jibu muafaka na linalowajibisha! Utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na Jumuiya ya Kimataifa unapaswa kujikita katika mchakato wa majadiliano yanayomwilishwa katika utashi wa kisiasa kama sehemu ya utekelezaji wake; pamoja na kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki kikamilifu. Huu ni mchakato unaopaswa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na matumizi bora ya rasilimali na utajiri wa Kimataifa katika kiwango kipana zaidi, kwa kuunda masoko, kuunda masoko na kutunza mazingira nyumba ya wote. Utekelezaji wake unapaswa kufumbatwa katika kanuni maadili, sera na mikakatio ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni wajibu kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza sauti ya viongozi wa kidini kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema amana na utajiri wao wa maisha ya kiroho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ustawi wa wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu unategemea na kufungamana na masuala kama udugu, haki na uaminifu kati ya watu. Umoja wa Mataifa unakazia mambo makuu matano: Watu, Mazingira, Ustawi, Maendeleo na Ushirikishwaji!

Malengo ya kiuchumi na kisiasa hayana budi kufumbatwa katika kanuni maadili na utu wema; wongofu wa kiekolojia na kwamba, dini zina mchango wa pekee sana katika utekelezaji wa sera na mikakati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Watu wanapaswa kutubu na kuongoka, ili kuweza kujipatanisha na jirani, mazingira pamoja na Muumba wao. Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na fungamani ifikapo mwaka 2030 uzingatie pia kanuni maadili; upendo kwa Mungu, jirani na mazingira.

Wananchi asilia ambao wanafikia asilimia 5% ya watu wote duniani, lakini wana uwezo wa kutunza: tamaduni na mazingira kwa asilimia 22%.  Hawa ni watu wanaothamini utakatifu wa kazi ya uumbaji. Kumbe, kuna haja ya kusikiliza kilio cha Dunia Mama pamoja na maskini wa dunia hii ili kujibu changamoto changamani zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Dini zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa sera na mikaka ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kutambua kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo na hii ni njia pekee ya kupambana na ukosefu wa haki katika uso wa dunia!

Papa: Maendeleo
08 March 2019, 16:02