Tafuta

Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya michezo kurejesha hadhi ya michezo kwa kuzingatia umuhimu wake katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya michezo kurejesha hadhi ya michezo kwa kuzingatia umuhimu wake katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake! 

Papa Francisko: Michezo: Maskini, ukweli, uadilifu & maendeleo

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu mbali mbali. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anasema hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kwamba, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja kuwa na upendeleo kwa maskini. Huu ni ushauri uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika kampeni kuhusu umuhimu wa michezo, ambayo sasa imeandikiwa kitabu kijulikanacho kama “Sport una lettera alla volta” chenye kurasa 144 na kimechapishwa na Malcor D’ na kwa sasa tayari kiko kwenye maduka ya vitabu.

Lengo la kitabu na ushauri kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni kutaka kurejesha tena dhana ya michezo katika uhalisia wake! Hii inatokana na ukweli kwamba, sehemu nyingi kwa sasa michezo imekuwa ni uwanja wa “masumbwi” mahali pa kuonesha ubabe unaoongozwa na falsafa ya mwenye nguvu mpishe! Michezo imevamiwa na wimbi kubwa la ukiukwaji wa kanuni maadili na utu wema, na kugeuka kuwa kama “kichwa cha mwendawazimu” mahali pa kupandikizia mbegu za utamaduni wa kifo na ukoloni wa kiitikadi. Michezo imegeuka kuwa ni uwanja wa rushwa na ufisadi kiasi hata cha kupoteza maana ya ushindani kwani kuna baadhi ya watu wenye “vijisenti vyao” wanaopanga matokeo ili kuweka faida kibindoni! Ubadhilifu wa fedha na mali ya umma katika tasnia ya michezo ni jambo ambalo linadumaza na kufisha juhudi za kufufua na kuendeleza michezo!

Baba Mtakatifu anasema “SPORT”; Herufi “S” linasimama kwa ajili ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.  Herufi “P” ni kwamba, Michezo ni kwa ajili ya wote pasi na ubaguzi kwani hii ni sehemu ya maisha ya binadamu. Licha ya wanamichezo waliobobea na waalimu wao, lakini michezo pia inawashirikisha hata maskini, na hawa ndio wale “akina yakhe, pangu pakavu tafadhali tia mchuzi”. Baba Mtakatifu anasema, herufi “O” inasimama badala ya neno “Uaminifu, ukweli na uwazi”. Hii ni dhamana nyeti kwa wadau wa michezo kuhakikisha kwamba, tunu hizi msingi zinamwilishwa katika michezo kwa kuondokana na kashfa ya rushwa, ufisadi na matumizi haramu ya dawa za kuongeza nguvu katika michezo. Lengo ni kulinda, kudumisha na kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi na kwamba, matumizi haramu ya dawa ni hatari sana kwa vijana wa kizazi kipya, kwani linawatumbukiza katika umaskini wa maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu anasema, herufi “R” inasimama kwa ajili ya walemavu ambao mara nyingi wana baguliwa na kunyanyapaliwa, kwani hawa pia wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika michezo ili kuwapatia fursa ya kuonesha karama na vipaji vyao licha ya ulemavu wa viungo walio nao! Herufi “T” inasimama kama “Karama, kipaji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kukumbatia uchoyo na ubinafsi. Baba Mtakatifu hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di sè”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema kwamba, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum.

Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu.

Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili.

Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamemekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa Mwaka 2018 inasema, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu pamoja na vituo vya michezo ni mahali muafaka pa malezi na makuzi endelevu na fungamani; ni mahali pa shuhuda za kiinjili, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna mwingiliano wa pekee kati ya familia, kazi, ulinzi wa uhai pamoja na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Taasisi za elimu na michezo zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, ziwe ni mahali pa kujenga misingi ya imani, kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; ni mahali pa kukabiliana na changamoto za kisayansi na kiteknolijia kwa mwanga wa Injili na kwamba, mabadiliko ya kijamii yanapaswa kuratibiwa na haki jamii. Kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa kuhusu utume wa Parokia, ili kujenga ari na mwelekeo mpya wa kimisionari kwa kujikita katika katekesi ya awali na endelevu.

Papa Francisko: Michezo
23 March 2019, 16:44