Tafuta

Kampeni ya Kipindi cha Kwaresima nchini Brazil kwa Mwaka 2019: Udugu na sera za umma! Kampeni ya Kipindi cha Kwaresima nchini Brazil kwa Mwaka 2019: Udugu na sera za umma! 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil

Waamini wakisukumwa na kuongozwa na kauli mbiu “Itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki”, pamoja na kufuafa mfano wa Mwalimu wao, Kristo Yesu aliyekuja duniani si kutumikiwa bali kutumikia, wanapaswa kujihusisha katika maisha ya kijamii kama kielelezo cha upendo kwa jirani unaowawezesha kujenga utamaduni wa udugu katika sheria na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, Jumatano ya Majivu, tarehe 6 Machi 2019 limezindua Kampeni ya 56 ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019. Tema ya mwaka huu ni “Udugu na sera za umma” na kauli mbiu ni “Itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil katika uzinduzi wa kampeni ya udugu nchini humo anasema, waamini katika Kipindi cha Kwaresima wanahimizwa kufunga, kusali na kutoa sadaka kama njia mahususi ya kujiandaa kwa ajili ya kusherehea Fumbo la Pasaka, yaani ushindi wa Kristo Yesu juu ya dhambi na mauti!

Baba Mtakatifu anasema, amana na utajiri huu vinapaswa kumwilishwa katika maisha ya mwamini mmoja mmoja na kama jumuiya ya waamini na kwamba, waamini nchini Brazil wanahamasishwa kujenga na kudumisha udugu katika sera za umma, ili kulinda, kutetea na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Familia ya Mungu nchini Brazil pamoja na taasisi zote zinapaswa kujisikia kuwa ni wadau wanaochakarika usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, zinakusudia katika kumuunda mtu mwadilifu. Mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa manufaa ya familia nzima ya mwanadamu.

Waamini wakisukumwa na kuongozwa na kauli mbiu “Itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki”, pamoja na kufuata mfano wa Mwalimu wao, Kristo Yesu aliyekuja duniani si kutumikiwa bali kutumikia, wanapaswa kujihusisha kikamilifu katika maisha ya kijamii kama kielelezo cha upendo kwa jirani unaowawezesha kujenga utamaduni wa udugu unaofumbatwa katika sheria na haki. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini walei kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanaitwa kuwa watakatifu, ili waweze kuwa kweli ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia, ili kujenga na kuimarisha malimwengu kadiri ya mpango wa Mungu.

Mama Kanisa tangu katika uongozi wa Papa Pio XII anawakumbusha wanasiasa kwamba siasa ni huduma ya upendo inayopaswa kutolewa kwa watu wa Mungu mintarafu maadili, tamaduni, daima wakionesha mshikamano katika matatizo na matumaini; wanasiasa wasimame kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi na kamwe, wasitoe kipaumbele cha kwanza kwa masilahi yao binafsi! Wasikubali kutishwa na nguvu ya fedha wala vyombo vya habari, bali wawe na uwezo pamoja na uvumilivu wa kukabiliana na changamoto changamani; kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kujadiliana kwa misingi ya kidemokrasia, ili haki na huruma viweze kushika mkondo wake!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko katika Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2019 katika mwanga wa sera za umma, familia ya Mungu nchini Brazil itaweza kufungua macho na nyoyo, tayari kuona na kuguswa na mahitaji ya ndugu zao maskini zaidi ambao kimsingi ni sehemu ya “Mwili wa Kristo” watu wanaopaswa kutambuliwa, kuguswa na kuhudumiwa kwa upendo na jirani zao. Nguvu mpya ya ufufuko wa Kristo isaidie kupyaisha Brazil, ili liweze kuwa ni taifa linalosimikwa katika udugu na haki. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil wakati huu wa Kampeni ya Kwaresima, kwa kuwaweka chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria wa Aparecida!

Papa: Kampeni Udugu: Brazil
07 March 2019, 14:46